Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtumishi wa Serikali auawa nyumbani kwake Kilosa

Mtumishi Picd Mereciana Calvin enzi za uhai wake.

Wed, 19 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mtumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa idara ya maendeleo ya jamii Mereciana Calvin (42) ameuawa nyumbani kwake eneo la Mamboya wilayani humo huku shingoni akionekana kuwa na majeraha ya kukatwa na kitu chenye makali.

Akitoa taarifa ya mauaji hayo kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro Hassan Omary amesema kuwa uchunguzi unaonesha mtumishi huyo aliuawa Julai 17 majira ya saa 3:30 usiku na mwili ulikutwa sebuleni kwake leo majira ya asubuhi.

Amesema kuwa pamoja na mtumishi huyo kuuawa lakini pia vipo viashiria vya wizi katika nyumba yake na amevitaja vitu vilivyoibiwa kuwa ni Televisheni, godoro na simu ya mkononi aliyokuwa akitumia marehemu enzi za uhai wake.

Kufuatia tukio hilo kaimu kamanda huyo amesema kuwa jeshi la polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi wa usalama wilaya na mkoa wanaendelea na uchunguzi ikiwa ni pamoja kuwasaka waliohusika kutekeleza mauaji hayo.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya hiyo ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo Shaka Hamdu Shaka amesema kuwa tukio hilo ni la kusikitisha na lazima vyombo vya ulinzi na usalama vifanye kazi usiku na mchana ili kubaini chanzo Cha mauaji hayo na wote waliohusika ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao.

"Ni tukio baya ambalo haliwezi kufumbiwa macho, nina imani na vyomba vya vyetu vya ulinzi na usalama najua kupitia wataalamu wao watachunguza vizuri na watatoa majibu kuhusu tukio hili ambalo linaonekana wazi kuwa ni la kupanga," amesema Shaka.

Amewatoa hofu wananchi na watumishi wa halmashauri hiyo na taasisi nyingine kwa kusema kuwa Serikali iko makini na vyombo vya ulinzi vinafanyakazi ili kuhakikisha wilaya hiyo inakuwa salama wakati wote.

Naye Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Kisena Mabuba amesema kuwa baada ya tukio hilo mwili wa marehemu Mereciana ambaye pia alikuwa mratibu wa ukimwi wa halmashauri umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro huku taratibu za maziko zikifanywa.

"Wazazi wa marehemu wanaishi Morogoro mjini na tayari kama ofisi tumeshafanya taratibu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuhifadhi mwili hospitali na kwa sasa tunasubiri maelekezo kutoka kwa familia ambao wao ndio watapanga wapi watakapomzika mpendwa wao," amesema Mabuba.

Alieleza namna walivyogundua mauaji hayo Mkurugenzi huyo amesema kuwa siku ya jana Mereciana ambaye kwa sasa ni marehemu hakuonelana kazini na hata hakuweza kupatikana kwenye simu hivyo jitihada za kumtafuta zulifanyika na ndipo mwili wake ulipokutwa sebuleni kwake ukiwa na majeraha shingoni.

Amesema kuwa Mereciana alikuwa akiishi peke yake kwenye nyumba hiyo hivyo polisi wanaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha mauaji hayo.

"Kwa kweli mpaka sasa kama watumishi watujui chanzo cha mauaji haya, tunaliachia jeshi la polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ili tuweze kijua nini kilimpata mwenzetu," amesema Gladys Mapeka mmoja wa watumishi waliokuwa wakifanyakazi na Mereciana.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: