Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtoto adaiwa kuunguzwa makalio na mjomba

Mikono Moto Kuchomwa (600 X 332) Mtoto adaiwa kuunguzwa makalio na mjomba

Tue, 5 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mtoto mwenye umri wa miaka mitatu, anadaiwa kufanyiwa ukatili na mjomba wake kwa kumuunguza na maji ya moto katika makalio na kumfanyia kipigo katika kijiji cha Msowero, Kilosa mkoani Morogoro.

Mtoto huyo kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya Mtakatifu Joseph, Dumila tangu Agosti 27, mwaka huu, huku ikidaiwa kuwa mjomba anayedaiwa kufanya kitendo hicho amekimbia.

Caroline Makemo, aliyejitolea kumlea mtoto huyo baada ya kufanyiwa ukatili huo, ambaye ni mkazi wa kijiji cha Dumila, alisema jana kuwa mtoto huyo amemtoa kijiji cha Msowero akiwa amefanyiwa kitendo hicho.

Alisema alipigiwa simu na Mtendaji wa Kata ya Msowero kwa ajili ya kumchukua mtoto huyo Agosti 27, mwaka huu, na kumjulisha kuwa amechomwa na moto kwenye makalio na miguu na mlezi wake huyo.

Makemo alisema alijulishwa hali ya mtoto si nzuri kwa sababu bado hajapatiwa matibabu na kumwomba aende kumchukua.

“Kwa vile mimi ni mlezi wa watoto nina kituo cha watoto yatima, nilikwenda kumchukua mtoto huyo kwa barua niliyopewa na ofisa mtendaji. Ilinibidi nimuulize mtendaji mtoto huyo imekuwaje ikabidi tumtafute mjomba ambaye ni mlezi wake nikajulishwa kuwa amekimbia.

“Nikauliza shangazi yuko wapi nikajulishwa yupo nikamwona na nikafanya naye mahojiano. Nilimuuliza mtoto amefanyaje akaniambia ameungua akiwa ameondoka kwenda kuchuma mboga na alivyorudi alimkuta amelowa na kwamba aligundua baada ya saa tatu kupita,” alisema.

Makemo alisema shangazi huyo alidai aliuliza kwa watoto wenzake mbona amelowa akajulishwa ameungua akachukua jukumu la kumvua nguo na kumpaka tope kama huduma ya kwanza.

“Nilimwambia shangazi unanidanganya. Haiwezekani mtoto aungue na moto kwa madonda haya ukae masaa matatu usijue ukiwa kama mlezi. Yule shangazi akaniambia aliipua viazi na kuweka chini na watoto walikuwa wanakunywa chai, hivyo wakati wanarudisha vikombe akaangukia viazi alivyokuwa ameweka chini,” alisema.

Makemo alisema alimjulisha maelezo aliyompatia hayajamridhisha kwa sababu ya ukubwa wa kidonda alicho nacho mtoto asijue maumivu yake yametokana na nini.

Alisema kwa kuwa lengo lake ni kumsaidia mtoto huyo, alimchukua na kumpeleka katika hospitali hiyo kwa kuwa kidonda kilikuwa kinatoa harufu, usaha na kuwapo uvimbe makalioni.

Hali hiyo, alisema ilimpa picha kuwa mtoto huyo hakupelekwa hospitalini na alipouliza alimjulisha hajapelekwa na aliishia katika duka la dawa. Pia alisema kwa sasa mtoto huyo amefanyiwa matibabu na dalili ni nzuri hata harufu aliyokuwa nayo haipo na maumivu yamepungua.

“Huyu mtoto alikuwa na maumivu makali hata usiku sikulala tulivyokuwa hapa hospitalini. Kwa sasa hali inaenda vizuri hata ile harufu aliyokuwa nayo haipo,” alisema Makemo.

Makemo alisema aliuliza mama wa mtoto akajulishwa amepatwa na tatizo la akili na baba yake hajulikani aliko. Alisema hadi sasa bado hajawapata ndugu wa mtoto huyo na mjomba wake aliyekuwa anamlea amekimbia amejiuliza kwa nini akimbie.

Makemo ameiomba serikali iwasaidie wale ambao wanaibua matukio hayo ili mtuhumiwa akamatwe na kuchukuliwa hatua iwe fundisho na kwa wengine.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk. Yunfa Hezron, alisema wamempatia mtoto matibabu na kwa sasa hali yake inaendelea vizuri ikilinganishwa na awali.

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka, alisema analaani vikali kitendo hicho cha kusikitisha kinachoonyesha mtoto huyo amepitia madhila makubwa.

“Wakati tunamjulia hali na kumuangalia kilichomsibu inaonyesha amemwagiwa maji ya moto katika maeneo yake ya makalio na kuathiriwa baadhi ya maeneo yake ya mwili. Nimezungumza na mtoto anaeleza bahati nzuri mtoto ukimfanyia ubaya anajua amenieleza aliyemfanyia hilo tukio ni mjomba wake,” alisema.

Shaka alisema serikali itasimamia matibabu ya mtoto huyo kama inahitajika kupelekwa hospitali kubwa zaidi ili arudi katika afya yake. Alisema hata baada ya matibabu serikali itaendelea kumwangalia kuhakikisha anapata haki zake za msingi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: