Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtandao wa kutengeneza dawa feki za binadamu wanaswa Dar

Tbcpicc Mtandao wa kutengeneza dawa feki za binadamu wanaswa Dar

Sun, 16 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Kanda ya Mashariki likishirikiana Jeshi la Polisi wanamshikilia William Mwangile anayedaiwa kuzalisha na kusambaza dawa bandia kwa mfumo wa makopo.

Mkaguzi wa Dawa wa TMDA, Jafari Mtoro, amesema Mwangile amekamatwa jana Ijumaa Aprili 14, maeneo ya Kipawa jijini Dar es Salaam baada ya msako kufanyika.

Jafari amesema kitendo hiki ni kinyume na kifungu cha 76 cha Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba, sura ya 19.

Mtoro amesema kutafutwa kwa Mwangile kulitokana na baadhi ya dawa alizozisambaza, akishirikiana na washirika waliokamatwa na TMDA awali. Amesema katika mtandao huo aliyebaki ni Mwangile aliyedakwa jana.

“Tumefanya upekuzi nyumbani kwake na kubaini lebo mbalimbali za dawa 537 ambazo zimeshaandikwa. Mfano wa hizo lebo ni dawa za Quinine Sulphate na Erythromycin na aina nyingine mbalimbali.

“Tulikuta viroba vitatu vya malighafi zinazotumika kutengenezea dawa, pia makopo 12 yanayofungasha dawa. Baada ya kukamilisha upekuzi nyumbani kwa Mwangile, tulienda kwa nyumbani kwa wazazi wake na kubaini mifuko ya carpsule aina ya ampricosi,” amesema Mtoro.

Mtoro amesema katika upekuzi nyumbani kwa wazazi wa Mwangile walibaini uwepo wa lebo 142. Amesema Mwangile ataunganishwa na watuhumiwa waliokamatwa awali ili kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

“Dawa bandia ni uhalifu kwa binadamu ni unyama na ukatili wa hali ya juu, kwa sababu mtu anatumia dawa hizi anategemea atapona, lakini anakutana na dawa bandia na uwezekano wa kupoteza maisha ni mkubwa,” amesema Mtoro.

Mtoro ametumia nafasi hiyo kutoa onyo kwa watu wanaojihusisha na biashara hiyo, akisema ni haramu na Mwangile alikuwa akitafutwa kwa muda mrefu, lakini alikuwa akikimbia kimbia.

“Alidhani hatakamatwa, lakini haikuchukua muda mrefu vyombo vya dola vimemkamata, haya mambo yanafanyika katika mitaa, kata zetu, wananchi toeni ushirikiano kwa Serikali na TMDA,” amesema.

Kwa mujibu wa Mtoro, sehemu kubwa ya dawa zimekamatwa kwa Mwangile zinazalishwa lakini zinapelekwa maeneo ya vijijini na nchi jirani.

Mtoro amesema mtandao umeenea maeneo mbalimbali hasa mikoani, lakini kupatikana kwa Mwangile hakuna atakayebaki salama, kila aliyehusika kwa namna moja au nyingine ikiwemo kusambaza au kuzalisha, atakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Mjumbe wa Shina Namba Sita la Mtaa wa Matembele, Mary Mambo ametoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano na uongozi wa TDMA kwa kutoa taarifa.

“Huu ni uharibifu wa mwili wa binadamu tunaomba adhabu kali kwa mhusika, ikitokea tunamuona mtaani…,” amesema Mambo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: