Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Miili ya wanawake wawili yaokotwa Dodoma

MAITI YAPOTEA Miili ya wanawake wawili yaokotwa Dodoma

Tue, 23 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Matukio ya kinyama yametokea dhidi ya wanawake wawili katika Mtaa wa Chinyika jijini Dodoma ambao miili yao imeokotwa huku mmoja ukionekana kujeruhiwa na kitu chanye ncha kali.

Kwa mujibu wa mashuhuda, mwili huo unaoonekana kujeruhiwa na kitu chenye ncha kali, umekutwa ukiwa umefungwa katika nailoni, boksi na kiroba.

Hata hivyo, juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Theopista Mallya zinaendelea baada ya simu yake kutopokewa mara kadhaa.

Akizungumzia tukio hilo leo Jumatatu, Julai 22, 2024, Kaimu Mwenyekiti wa mtaa huo, Aloyce Maswikwi amesema miili hiyo ilionekana kati ya jana na leo Jumatatu, huku mmoja ukiwa haujatambulika.

Amesema mwili mmoja ulionekana na mwanakijiji aliyekuwa katika shughuli za uchungaji mifugo ukiwa umefungwa mithiri ya zigo la nguo za mtumba.

Maswikwi amesema kuwa mwili huo uliokotwa katika korongo na mfugaji huyo aliyekuwa amepeleka ng’ombe kwa ajili ya kunywa maji eneo hilo  lililopo kwenye mtaa huo.

Kwa namna ulivyofungwa, amesema ilikuwa vigumu kubaini kama kuna mtu na mwanakijiji huyo alipomwita mwenzake kwa ajili ya kuangalia kilichomo, walilazimika kuchana na ndipo walipoiona miguu.

“Alipokwenda wakasema ngoja tufungue kuna nini, hali iliyowafanya kuchana, kumbe walikokuwa wamechana kulikuwa na miguu,” amesema.

Mwenyekiti huyo ameeleza wawili hao walichana kila kilichofungashwa na baada ya kubaini kulikuwa na mwili wa mwanamke, walipiga kelele zilizosababisha mkusanyiko wa watu.

“Wakatukaribisha tuangalie kama tuna mfahamu. Tulipanga foleni wanawake kwa wanaume, tukamwangalia yule dada (ana umri wa miaka kama 20) kwa kweli hatukumtambua. Kwa hiyo askari wakamchukua,” amesema.

Maswikwi amesema tukio la pili la Alice Ndondo lilitokea saa 12.00 asubuhi leo Jumatatu, baada ya kupigiwa simu na askari wa kata kuelezwa juu ya uwepo wa msiba katika moja ya familia za mwanakijiji.

“Nilipofika nikakuta kweli amelala katika mlango hapa, wamemfunika shuka watu wengi wanalia, nikauliza vipi, nikaambiwa kuwa wamemkuta wamemtupa hakuwa na nguo,” amesema.

Alipohojiwa mama wa marehemu, mwenyekiti huyo amesema alijibu mwanawe alitoroka muda kidogo na hakufahamu alipokwenda.

“Alinieleza alipokuwa ameenda (marehemu) hajui na wala ndugu zake hawakufahamu ila kuna rafiki yake anaitwa Mwache ambaye waliolewa wote Zuzu ndiye anayefahamu kama aliolewa na nani na ndiye anayetumiwa kuleta matumizi ya mtoto hapa,” amesema mwenyekiti.

Pamoja na kuuawa, Maswikwi amesema mwili wa mwanamke huyo haukuwa na jeraha lolote na kwamba hadi sasa chanzo cha kifo chake hakijafahamika.

Amesema matukio yote mawili yanaonekana kufanywa na watu wa nje ya mtaa huo. “Yule dada watakuwa wamemuua huko mbali, wakaona waje wamtupe hapa Chinyika. Inaonekana kama kuna ukatili fulani. Matukio haya ni mazito. Nitoe wito kwa polisi waongeze juhudi katika kazi yao. Na endapo hawa watu watabainika watoe adhabu zinazostahili,” amesema.

Mama wa Marehemu, Careen Ndondo amesema mwanawe aliondoka wiki nne zilizopita bila kumuaga anakoelekea lakini leo Jumatatu aliarifiwa na mjukuu wake kwamba ameonekana amelala na akiitwa haitiki.

“Tukainuka na kaka yake tukaenda pale na kumkuta kalala chali, tukasema msimshike mtafuteni mwenyekiti lakini alipokuja ndugu yake mwingine alimshika na kumtingisha. Hata hivyo alimkuta kakauka, nikasema huyu amekufa sio mzima,” amesema Careen.

Tangu mwanawe alipoondoka, amesema hawakuwa na mawasiliano yoyote. “Sijui kama walikuwa na mahusiano, rafiki yake anaweza kueleza vizuri kwa nini achukue fedha awe anamwita. Na jana alimwita mtoto wake yeye anasoma darasa la sita. Kwa kuwa alikuwa anamwita mtoto wake na kuzungumza naye, hatukuwahi kumtafuta,” amesema Careen.

Simulizi ya mtoto Naye mtoto wa marehemu (anayesoma darasa la sita), ambaye ndugu hawakutaka jina lake liandikwe, amesema mama yake alipoondoka hakumwambia anakwenda wapi, isipokuwa rafiki wa marehemu alimwita mara kwa mara na kumpa fedha za matumizi na wakati mwingine kuzungumza naye.

“Fedha ilipoisha nikaenda kumwambia fedha imeisha akanitumia fedha nyingine. Tukaja kuongea siku nyingine na mama akaniambia kuwa anaumwa na kuwa alitaka kurudi lakini anaumwa.

“Juzi jioni saa 11 nikaongea na Willy (anayedaiwa alikuwa na mama yake) akaniambia mama yangu anaumwa na juzi alikuwa hana fedha na kuwa atanitumia leo,” amesema.

Mtoto huyo amesema mwanamume huyo aliyemtaja kwa jina moja la Willy alimweleza alikuwa akimuwahisha hospitali mama yake. “Mara ya mwisho kuongea na mama yangu ilikuwa juzi (Jumamosi) akaniambia mwanangu mimi naumwa kikohozi,” amesema mtoto huyo.

Naye rafiki yake, Mwacheni Matonya amesema siku alipoondoka Alice, yeye alikuwa saluni na kumuomba namba ya simu kwa ajili ya kumtumia mtoto wake fedha za matumizi.

“Mara ya kwanza alinitumia Sh5,000 nikampatia mtoto lakini nikamuuliza mbona shoga yangu hurudi akasema nipo sokoni ninauza nyanya lakini baadaye nitakuja. “Baada ya hapo nikawa napiga simu haipatikani. Hadi jana (Jumapili) anakuja mtoto aniuliza mama yangu umeongea naye nikamwambia simu yake haipatikani,” amesema.

Hata hivyo, amesema hafahamu rafiki yake alipokuwa akiishi hadi jana alipoitwa kuona kwamba amefariki dunia.

Uongozi wa Hospitali Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dk Samwel Magesa amethibitisha kupokea miili ya wanawake hao wawili kati ya jana na leo.

Amesema jana saa 11 jioni walipokea mwili wa mwanamke ambaye jina lake halikufahamika lakini ulikuwa na majeraha katika sehemu mbalimbali yaliyosababishwa na kuchomwa na kitu chenye ncha kali.

“Huyu wa jana alikuwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili, ilionekana baadhi ya majeraha kidogo yalikuwa yameenda ndani. Sehemu za kichwa pia zilikuwa na majeraha,” amesema.

Pia, Dk Magesa amesema saa 3.40 asubuhi leo Jumatatu walipokea mwili wa mwanamke ambao haukuwa na jeraha lolote na hivyo walikuwa wanaendelea na uchunguzi ili kubaini nini hasa kimesababisha vifo hivyo.

Julai 17, 2024, mtoto Telesphore Mwakalinga aliuawa na watu wasiojulikana na mwili wake kukutwa karibu na nyumbani kwao Nyumba 300, Kata ya Nzuguni huku ukiwa umeondolewa sehemu za siri na mkono mmoja.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: