Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mganga mbaroni tuhuma kusababisha kifo cha mtoto

MANDE PILI Ed Mganga mbaroni tuhuma kusababisha kifo cha mtoto

Tue, 11 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jeshi la Polisi mkoani Lindi linamshikilia mganga wa kienyeji, mkazi wa Kata ya Rutamba, Manispaa ya Lindi, Jalina Juma (45) kwa tuhuma za kusababisha kifo cha mtoto Yusufu Salum (9).

Mtoto huyo alifariki juzi katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Lindi (Sokoine), alikolazwa kwa ajili ya kupatiwa matibabu kutokana na majeraha ya moto aliyodaiwa kuyapata kwa mganga huyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, Pilli Mande na Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Alexander Makalla, wamethibitisha kutokea kifo cha mtoto huyo Julai 8.

Dk. Makalla alisema mteja wao alifikishwa hospitalini Julai Mosi mwaka huu, akiwa na majeraha makubwa eneo la mgongoni yaliyotokana na kuunguzwa moto.

Alitaja kilichosababisha kifo cha mtoto huyo ni kuenea moto huo ndani ya mwili wake. Ngozi yake ilikuwa haijakomaa.

“Ni kweli mtoto huyo alifikishwa hapa Julai Mosi mwaka huu, akiwa na jeraha kubwa eneo la mgongoni mwake,” alisema kiongozi huyo wa hospitali na kubainisha tayari mwili wa mtoto huyo umeshakabidhiwa kwa wazazi wake kwa ajili ya mazishi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, Pilli, alisema mtoto huyo alifikishwa nyumbani kwa mganga huyo na wazazi wake kwa ajili ya kumpatia huduma za matibabu kutokana na ugonjwa wa degedege uliokuwa unamsumbua.

Alidai kuwa baada ya kumfikisha huko, mganga huyo alimpokea na kumlaza juu ya kitanda kisichokuwa na godoro. Uvunguni aliweka nyasi zilizokuwa zinawaka moto na kumuunguza mtoto huyo mgongoni.

Kamanda Pilli alisema wanamshikilia mganga huyo kwa mahojiano ya kina. Wanatarajia kumfikisha mahakamani. Akawataka waganga wa jadi kutumia taaluma zao kwa uangalifu. Waepuke matatizo kama la mganga huyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: