Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mama: Mtoto wangu alilawitiwa na jirani

Mtoto Wangu Alilawitiwa Na Jirani Mama: Mtoto wangu alilawitiwa na jirani

Thu, 13 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Alipopata majibu kwa daktari kwa mara ya kwanza, Martha Jumanne (siyo jina lake halisi), alipata shinikizo la damu na kuanguka, alikuwa mzito kuamini mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka sita ni mwathirika wa ulawiti kwa miaka miwili.

Vitendo hivyo vilikuwa vinafanywa na mtoto wa jirani yake mwenye miaka 27 na alianza kumfanyia kitendo hicho kipindi cha likizo baada ya mlipuko wa ugonjwa wa Uviko-19, mwaka 2020, mtoto huyo alipokuwa na miaka minne.

“Nilipokea majibu ya daktari kwa mshtuko nikajikuta nimeanguka baada ya presha kushuka, haikuwa rahisi na sikutegemea mtoto wa kiume anaweza kufanyiwa kitendo hicho,” anasema mama huyo mkazi wa Olasiti jijini Arusha.

“Huwa nasikia lakini sikuwa naamini vitendo vinafanyika, nilidhani ni maigizo, lakini ilipomtokea mtoto wangu niliumia sana na niliamini kweli matukio hayo hutokea.”

Martha anasema baada ya kuona mabadiliko kwa mtoto wake wa kiume mwenye miaka sita aliyekuwa darasa la kwanza, ikiwamo kutokwa na haja kubwa kila mara, ndipo alipombana kwa maswali kwa nini hali hiyo.

“Mtoto akaniambia amekuwa akifanyiwa ukatili huo wa kingono na kijana mmoja ambaye ni jirani yetu,” anasimulia Martha.

Anasema baada ya kuelezwa hayo alikwenda kituo cha polisi kisha kumpeleka mtoto wake Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru na baada ya vipimo, aligundulika amelawitiwa.

Martha anasema polisi walimkamata mtuhumiwa akafunguliwa kesi na mwanzoni mwa mwaka huu, amehukumiwa kifungo cha maisha jela.

Ukatili ulivyoanza

Mama huyo anasema halikuwa tukio la kwanza kwa kijana kutekeleza ukatili huo, kwa sababu tayari inadaiwa alishafanya kwa watoto kadhaa mtaani hapo, lakini wazazi walikubali kumalizia kesi nyumbani.

“Baadhi yao walikuwa wanapewa hadi Sh700,000 na wanahama hapa, lakini mimi nikasema sitapuuzia, kesi ikapelekwa hadi mahakamani licha ya mama yake kutaka tuyamalize nyumbani kama wazazi, hatukukubaliana,” anasema mama huyo.

“Ninatoa wito kwa wazazi wenzangu wasije kukubali kesi hizi za ukatili zikaishia nyumbani, matukio ya namna hii tukiendelea kupindisha sheria hayataisha, tuache ichukue mkondo wake,” anasema mama huyo.

Hivi karibuni ripoti za matukio ya ulawiti na ubakaji zimeendelea kutawala vichwa vya vyombo vingi vya habari na mitaani.

Na sasa vinadaiwa kufanyika hadi sehemu zinazodhaniwa ni salama kwa watoto, ikiwamo shuleni, nyumbani na hata kwenye nyumba za ibada, hali inayozidisha hofu kwa jamii.

Baadhi ya sababu zinazotajwa kuchangia vitendo hivyo vya ukatili kwa watoto ni mmomonyoko wa maadili.

Hata hivyo, inaelezwa sababu nyingine ni pamoja na baadhi ya wazazi na walezi kushindwa kuwajibika katika ulinzi wa watoto, imani za kishirikina na migogoro ya ndoa inayosababisha wazazi kutengana na watoto kukosa uangalizi wa karibu.

Sababu nyingine zinazotajwa kuchangia kuongezeka kwa vitendo hivyo ni walimu kutokusimamia malezi kwa kiwango kikubwa, badala yake kuangalia namna ya kufundisha tu.

Ukiangalia kwa upande wa baadhi ya shule binafsi watoto wamekuwa wakichukuliwa mapema na kuzunguka kupitia wanafunzi wenzao, hivyo umakini unapaswa kuongezeka ili wawe salama pindi wanapokuwa kwenye magari kuelekea shule.

Kwa mujibu wa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Doroth Gwajima anasema kati ya Januari hadi Desemba mwaka 2021 matukio ya ukatili kwa watoto yaliyoripotiwa polisi ni 11,499, kati ya hayo ulawiti yakiwa ni 1,474.

Hivi karibuni kulisambaa video mtandao ikimuonyesha mtoto wa darasa la tatu Arusha akisimulia namna alivyofanyiwa ukatili na mwalimu wake, lakini Dk Gwajima anasema hatua zimechukuliwa dhidi ya mtuhumiwa.

Kupitia mtandao wake wa kijamii wa Twitter, Dk Gwajima anaandika: “Shtaka la mtuhumiwa lipo polisi RB namba ARS/RB/3429/2023. Wako watoa huduma ambao wamevaa vazi la kondoo kumbe ni wanyama wakali dhidi ya watoto.

Wazazi semeni na watoto msisubiri tukio limkute, sema naye sasa hivi hapo ulipo kuwa mwanangu marufuku mtu kuleta agenda za kugusa mwili wako wala kukuita pembeni na kukueleza lolote na kukuambia usiseme wala asikutishe ukanyamaza, piga kelele toa taarifa.”

Hii imeonekana pia kwenye ripoti ya haki za binadamu mwaka 2021 iliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), inayoonyesha mikoa mitano inayoongoza kwa matukio ya ukatili dhidi ya watoto mwaka 2021, kati ya matukio 11,499, yaliyoripotiwa polisi ni 2,993 sawa na asilimia 26, yaliripotiwa mikoa ya Arusha, Tanga, Shinyanga, Mwanza na mkoa wa kipolisi Ilala (Dar es Salaam). Katika ripoti hiyo miongoni mwa sababu zinazotajwa kusababisha kushamiri kwa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto ni familia za waathirika kuzungumzia kesi za ukatili katika ngazi ya familia, watoto kuachwa peke yao nyumbani kwa muda mrefu, malezi duni, ulevi, ugumu wa maisha, ndoa za utotoni, wazazi kutengana na imani za kishirikina.

Wadau wanena

Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Arusha, Dennis Mgiye anasema katika kipindi cha mwaka 2020/21 matukio ya ulawiti katika ngazi ya mkoa yalikuwa 195, huku kati ya hayo, 145 yakiripotiwa kutoka Jiji la Arusha.

Mgiye anasema mwaka 2021/22 matukio hayo yaliongezeka na kufikia 204 kwa ngazi ya mkoa na kati ya hayo matukio 166 ni kutoka Jiji la Arusha.

Anasema asilimia 78 ya kesi za ulawiti Mkoa wa Arusha ni kutoka halmashauri hiyo.

Mgiye anasema vitendo vya ulawiti vinafanywa katika maeneo yote yaani nyumbani, shuleni na njiani.

Anataja kata zinazoongoza kwa vitendo hivyo katika halmashauri ya Jiji la Arusha ni Unga Limited, Daraja Mbili, Sokoni One na Ngarenaro.

“Miongoni mwa mikakati ya kudhibiti ukatili, hasa ulawiti ni pamoja na kuunda madawati ya ulinzi wa mtoto shuleni ili kuweza kupata taarifa za ukatili kwa haraka na kushirikiana katika Kampeni ya SMAUJATA kuhakikisha elimu ya ukatili inatolewa kwa jamii katika ngazi zote,” anasema Mgiye.

Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii Arusha, Isaya Doita anasema kutokana na kukithiri kwa vitendo vya ukatili, hasa ulawiti, adhabu za kupitiliza shuleni na kupinga vitendo viovu wameanzisha kampeni maalumu ya kupambana na vitendo hivyo jiji la Arusha.

Doita, ambaye ni Diwani wa Ngarenaro anasema kampeni hiyo iliyozinduliwa mwanzoni mwa mwezi huu, katika kata yake tayari wameshatembelea shule zote zilizopo kwenye kata hiyo na kuzungumza na wazazi, walimu na wanafunzi.

Anasema kampeni hiyo itafanyika katika kata zote 25 na mitaa 154 iliyopo Arusha.

“Mfano, mwenyekiti wa mtaa ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya mtaa, ana wajumbe wake, kuna mabalozi, watu waovu wanaofanya matukio yasiyofaa wanayaona lakini hawawezi kuyakemea, kwa hiyo kuna udhaifu wa baadhi yao,” anasema Doita.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Osunyai, Kimbwereza Makore anasema wameandaa klabu ya wanafunzi 60.

“Hao ndio mabalozi wa wenzao kule madarasani, kila wiki tunakutana na mabalozi kutueleza, wao ni rahisi kupata taarifa za wenzao lakini pia hao wanafunzi tumewapa mafunzo kwa kushirikiana na Shirika la CWCD linalotuwezesha kuwapa mafunzo namna ya kutambua, kuelezea na kutoa taarifa za ukatili.

“Kila wiki pia tunakutana na wanafunzi na walimu wote kupitia vipindi vya dini na tunaamini walimu pia wakiwa na hofu ya Mungu hawatafanya vitendo vya kikatili kwa wanafunzi. Hali si nzuri na hii siyo vita ndogo,” anasema Osunyai.

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati, Dk Solomon Massangwa anasema ni muhimu wazazi na walezi kuongeza nguvu zaidi kwenye malezi ya watoto ili kuwaepusha na vitendo hivyo.

“Ni kweli tunakimbizana kutafuta fedha, lakini mwisho wa siku malezi ya watoto wetu ni muhimu sana. Ulawiti ni laana na haya pia ni matokeo ya mmomonyoko wa maadili na matokeo ya kuacha kufuata maelekezo ya eneo la Mungu,” anasema Dk Massangwa.

Ni wajibu wa jamii kwa jumla kukemea uovu katika jamii na kuacha ubinafsi wa kila mmoja kulea watoto wake, tofauti na miaka ya nyuma, malezi jumuishi yalikuwa katika sehemu kubwa ya jamii ili kunusuru watoto wa kiume.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: