Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Giza latanda mwanamke aliyedaiwa kujinyonga mahabusu

Mahabusuuu Mahabusiiiiiiiiiiiii.png Giza latanda mwanamke aliyedaiwa kujinyonga mahabusu

Fri, 22 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Uamuzi wa uchunguzi wa chanzo cha kifo cha Stella Moses, aliyefariki dunia akiwa mahabusu katika Kituo cha Polisi Mburahati, jijini Dar es Salaam, bado kizani baada ya Mahakama kutoutoa kwa mara nyingine.

Uamuzi huo ulipangwa kutolewa jana na Mahakama ya Korona katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Dar es Salaam, Kivukoni (Kinondoni) iliyoketi kufanya uchunguzi wa kifo hicho baada ya familia ya marehemu kufungua shauri la maombi ya jinai.

Hata hivyo, Mahakama hiyo ilishindwa kutoa uamuzi huo kutokana na Hakimu Mkazi Jackline Rugemalira, kutokuwepo.

Akiahirisha shauri hilo, Hakimu Mkazi Janeth Kaluyenda alisema Rugemalira, aliyehusika na shauri hilo hayupo kwa kuwa ana dharura na alipanga uamuzi huo kutolewa jana.

Hii ni mara ya pili uamuzi huo kuahirishwa, awali ulipangwa kutolewa Septemba 12, mwaka huu, lakini uliahirishwa kutokana na Mahakama hiyo kutokamilisha kuuandika.

Awali katika tarehe iliyopangwa kutolewa uamuzi, Rugemalira alisema hakuwa amekamilisha kuandika kutokana na matatizo ya kiafya yaliyomfanya akafanyiwa matibabu ya upasuaji nje ya nchi.

Stella alifariki dunia usiku wa Desemba 20, 2020, akiwa mahabusu kituoni hapo alikojisalimisha baada ya kupata taarifa kuwa alikuwa anahitajika, tukio ambao lilizua mvutano mkubwa baina ya Polisi na ndugu wa marehemu kwa kile wanachodai kuwa ni mazingira tata ya kifo hicho.

Katika tukio hilo lililoripotiwa kwa kina na Mwananchi katika toleo la Desemba 23, 2020, Jeshi la Polisi lilidai kuwa mwanamke huyo alifariki dunia baada ya kujinyonga akiwa mahabusu.

Ndugu wa marehemu walipinga taarifa hizo wakidai kuwa kulikuwa na utata wa mazingira ya kifo hicho, badala yake walitaka ufanyike uchunguzi huru ili kujua chanzo halisi cha kifo cha ndugu yao.

Baadaye familia ililazimika kufanya mazishi bila hata kupewa matokeo ya uchunguzi wa chanzo cha kifo hicho uliofanywa na Hospitali ya Muhimbili.

Miaka miwili baadaye ndugu wa marehemu walifungua shauri la maombi dhidi ya viongozi wa Jeshi la Polisi na uongozi wa Hospitali ya Muhimbili kwa kutokutimiza wajibu wao.

Shauri hilo lilifunguliwa na shemeji wa marehemu, Emmanuel Kagongo dhidi ya viongozi wa Jeshi la Polisi na Hospitali ya Taifa Muhimbili mahakamani hapo akiomba Mahakama hiyo iridhie kufanya uchunguzi huru.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: