Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chakula walichokula watoto watano waliofariki dunia chajulikana

Chakulapiic Data Chakula walichokula watoto watano waliofariki dunia chajulikana

Fri, 22 Jul 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Chakula cha mwisho walichokula watoto watano wa familia moja kinachodaiwa kuwapotezea maisha Kijiji cha Mswakini Chini, wilayani hapa Mkoa wa Arusha kimeelezwa kuwa ni ugali na maziwa ulioandaliwa nyumbani na wazazi wao.

Wakizungumza jana, ndugu wa familia hiyo walidai kuwa chakula hicho kinachoelezwa kukutwa na kiambata cha sumu kililiwa Julai Mosi na baadaye watoto hao walianza kuumwa tumbo.

Watoto watatu waliofariki dunia Julai 20 na mmoja jana wamezikwa jana. Mtoto aliyefariki dunia Julai 5 alizikwa wiki iliyopita.

Baba mdogo wa watoto hao, Kirong’a Mollel alisema Julai Mosi mmoja kati yao alionekana kuzidiwa zaidi hivyo alichukuliwa na kupelekwa hospitali binafsi, kabla ya kufariki dunia.

“Hawa wengine nao, wakaanza kuvimba tumbo na wakapatiwa matibabu nyumbani na baada ya hali kuwa mbaya, walipelekwa Hospitali ya Jeshi Monduli (TMA), walipotibiwa walipata nafuu, lakini wakati wanarudi nyumbani, hali ilibadilika, wakapelekwa Hospitali ya Mkoa Mount Meru ambako walifariki dunia,” alisema Mollel.

Hata hivyo, alisema ugali na maziwa ni chakula walichokuwa wakila siku zote wakitoka shuleni na kuchunga mifugo.

Advertisement “Hatuna chakula kingine pale nyumbani, ni ugali na maziwa tu, ndiyo maana tunaomba uchunguzi zaidi ufanyike kujua hiyo sumu ilitoka wapi,” alidai Mollel.

Mwanafamilia mwingine, Leseno Mollel alisema watoto hao walikuwa wakiishi na wazazi wao pekee na ni familia ya mke na mume mmoja na hawajawahi kushuhudia mgogoro ambao labda wangeweza kuuhusisha na vifo hivyo.

Alisema baba wa watoto hao, Nyangusi Mollel na mke wake, Nandoye Nyangusi walikuwa na watoto saba na mmoja bado ananyonya ambaye amesalimika.

“Tumejaribu kuuliza kama kulikuwa na ugomvi nyumbani au kwa majirani, tumeshindwa kujua ukweli nini chanzo cha watoto kuumwa matumbo na kuvimba,” alisema mwanafamilia huyo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mswakili, Nanga Karani alisema mtoto aliyesalimika ana miaka 12, hakula chakula hicho kwa kuwa alikuwa kwa bibi yake na mmoja ni mdogo ana miezi saba, bado ananyonya.

Miili yazikwa

Akizungumza wakati wa kuaga miili ya marehemu katika viunga vya chumba cha kuhifadhia maiti cha Hopitali ya Mount Meru juzi, Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Frank Mwaisumbe alisema uchunguzi wa awali umebaini watoto hao walikuwa wamekuwa chakula.

“Ninachoweza kusema sasa ni kuwa marehemu wamekutwa na viambata vyenye sumu kwenye miili yao na uchunguzi zaidi unaendelea kujua aina ya sumu hiyo,” alisema Frank.

Alisema wataalamu wa maabara wa hospitali hiyo wamechukua sampuli za marehemu kwa ajili ya kupeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ili kubaini sumu hiyo ni ya aina gani.

Wakati huo huo, mkuu huyo amepiga marufuku matumizi ya dawa za miti shamba zisizothibitishwa kitaalamu.

Alisema watoto hao walifariki kwa nyakati tofauti baada ya kuvimba matumbo na macho kuwa ya njano, jambo alilodai kuwa linaashiria huenda walikunywa dawa.

Mchungaji Christin Ndunguru wa Kanisa la Pentecoste Mission Arusha, alisema watoto wamepoteza maisha na jambo kubwa linalopaswa kufanywa ni kuwaombea kwa Mungu.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz
Related Articles: