Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CCM yalaani kada kuchomewa mali

Dk. Mohamed Said Dimwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk. Mohamed Said Dimwa

Wed, 11 Sep 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimelaani kitendo cha kuchoma moto mali za mwanachama wake mpya kutoka ACT-Wazalendo, Salum Mohamed Juma, katika shehia ya Wingwi Mapofu, Wilaya ya Micheweni, Pemba.

Kutokana na kitendo hicho, kimelitaka Jeshi la Polisi kuchukua hatua za kisheria kwa watu wote waliohusika na vitendo. 

Pia kimesema baadhi ya wanachama wapya wa CCM wameanza kutishwa na kufanyiwa vitendo vya hujuma na wengine kujeruhiwa na kuharibiwa mali zao hali inayotakiwa kudhibitiwa na vyombo vya ulinzi na usalama.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk. Mohamed Said Dimwa, alisema hayo jana baada ya kuweka jiwe la msingi katika Maskani ya CCM Mjini Kiuyu, Jimbo la Kojani, katika mwendelezo wa ziara ya kikazi ya kuimarisha chama ya Wajumbe wa Sekretarieti ya Kamati Maalum ya NEC  Zanzibar katika wilaya ya Wete Kichama. 

Watu wasiojulikana, juzi  walivamia makazi ya Salum na kuingia nyumbani kwake kisha kuchoma moto godoro, vitambulisho, nguo na bendera ya CCM hatimaye  kukimbia baada ya wananchi kujitokeza kuzima moto uliokuwa umeanza kuchoma makazi yake. 

Dk. Dimwa ametoa pole kwa mwanachama huyo na wengine wanaopata vitisho na kauli za ubaguzi ambapo amewahakikishia kuwa watakuwa na usalama wa mali na maisha yao ya kila siku.  

Kutokana na tukio hilo, alisema CCM inatarajia vyombo vya ulinzi na usalama vitachukua hatua za haraka kwa kuhakikisha watu wote waliohusika bila kujali, cheo, chama cha kisiasa na umaarufu wanafikishwa katika vyombo vya sheria.

Amesema Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliundwa kwa dhamira ya kumaliza siasa za chuki na visasi ili kuweka nchi katika hali ya amani na utulivu na kuhakikisha nchi inapiga hatua kimaendeleo na wananchi wanaishi kwa amani. 

Alisema ni muhimu kila chama kikajielekeza katika kufanya siasa za ushindani wa sera kwa kueleza na kutekeleza masuala ya maendeleo ili wananchi wavutiwe na sera kisha wajiunge na chama wanachoona kinafaa bila kulazimishwa.

Dimwa pia alisema Zanzibar ni nchi inayoongozwa kwa misingi ya sheria na kuheshimu demokrasia, hivyo kila mwananchi ana haki ya kuwa mwanachama wa chama chochote cha kisiasa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: