Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wananchi Ludewa wamkumbuka Deo Filikunjombe

Deo Filikunjombe E.jpeg Deo Filikunjombe enzi za uhai wake.

Wed, 21 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wananchi wa kijiji cha Nsele kata ya Kilondo tarafa ya Mwambao halmashauri ya wilaya ya Ludewa mkoani Njombe, wameiomba serikali kumalizia ujenzi wa zahanati iliyoasisiwa na aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Deo Filikunjombe (CCM) ili kunusuru uhai wao hasa wazee na wajawazito.

Filikunjombe wakati anaanzisha ujenzi huo mwaka 2015, alitoa mifuko 100 ya samenti, mabati, fedha za mafundi, mbao na madirisha huku wananchi wakichangia nguvu kazi kubeba mawe, tofali na kokoto lakini hadi sasa ikiwa imepita miaka zaidi ya saba, ujenzi haujakamilika.

Wakizungumza mwishoni mwa wiki, wakazi hao walisema wakati wa Filikunjombe akiwa mbunge wao mwaka 2015, aliitisha mkutano kijijiji humo akiwataka waanzishe ujenzi wa zahanati kwa nguvu zao kisha atachangia vifaa vya ujenzi lakini alipofariki mradi umetelekezwa.

Kileo Ignas mkazi wa Nsele alisema kijiji hicho hakijawahi kuwa na zahanati hivyo wananchi hutumia mitumbwi kwenda makao makuu ya kata umbali wa kilomita 10 kwenye Ziwa Nyasa kusaka huduma za afya huku akina mama wengi wanaojifungulia njiani wakipoteza maisha.

Ignas aliungwa mkono na Hawa Litembo mkazi wa Nsele ambaye alisema wanapopata ujauzito wanalazimika kuhama kwa muda kijijini humo kwenda kuishi kwa ndugu maeneo yenye huduma za afya ili kujinusuru na kifo.

“Wananchi wengi wamepoteza maisha, wengine wanapoumwa hukimbilia kwa waganga wa kienyeji, nguvu kazi nyingi zinapotea wengine wanahama kijiji baada ya kukosekana huduma za afya. Tumemuelezw mwenyekiti, Diwani na hata uongozi wa wilaya ili wamalizie ujenzi lakini bado hakuna kilichofanyika,” alisema Litembo.

Diwani kata ya Kilondo, Alex Mwakila alikiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kuongeza kuwa wagonjwa husafiri kwa mitumbwi kilometa 10 hadi makao makuu ya kata wengine wanaenda hadi hospitali ya Matema iliyopo Kyela kusaka tiba.

Hata hivyo, alisema ufumbuzi umepatikana umeanza kufanyika. “Juzi tulipewa Sh 12 milioni za mapato ya ndani kukamilisha ujenzi kwa kuweka madirisha, marumaru, milango, kupiga ripu yumba viwili,” alisema Mwakila.

Mwenyekiti wa halmaahauri ya wilaya ya Ludewa, Wise Mgina alisema Sh 12 milioni iliyotakiwa kununua dawa na vifaa tiba sasa inaenda kumalizia ujenzi huo ambao unatarajiwa kukamilika Agosti mwaka huu.

Alisema changamoto ya ukosefu wa zahanati si kwa Nsele tu, bali pia vijiji vingi havina kikiwemo cha Liunji ambacho kimetengewa Sh 34 milioni.

Mkurugenzi wa halmaahauri hiyo, Sunday Ndori alisema katika bajeti ya 2023/2024 inayoanza Julai mwaka huu kipaumbele kikubwa ni kumalizia ujenzi wa zahanati kwenye vijiji vyote.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: