Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tumlinde Mzize, tujikumbushe ametoka kituo cha bodaboda

Clement Mzize X Maxi Mpia Nzengeli Tumlinde Mzize, tujikumbushe ametoka kituo cha bodaboda

Mon, 15 Apr 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Rafiki yangu mmoja tukiwa Afrika Kusini alikuwa ananiambia namna ambavyo hamkubali mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize. Nadhani ilichangia zaidi na hasira za namna ambavyo Mzize alikosa bao la wazi wakati pambano la Yanga na Mamelodi Sundowns likiyoyoma pale Pretoria.

Huenda watu wasingelikumbuka bao halali la Aziz Ki lililovuka mstari kama Mzize angefunga. Kama Mzize angefunga basi lingekuwa bao la kushangaza ambalo lingewapeleka Yanga katika hatua ya nusu fainali kwa mara ya kwanza katika historia yao.

Ambacho rafiki yangu amesahau na ambacho watu wengi wamesahau ni ukweli kwamba tayari Mzize ameshafanya jambo kubwa la kushangaza kuliko kukosa lile bao. Yeye tu kuwepo katika hiyo mechi, akacheza, akajikuta katika nafasi ile, ni jambo la kushangaza.

Muda si mrefu alikuwa anaendesha bodaboda pale Iringa. Leo ni mshambuliaji wa Yanga iliyoiva. Tofauti na washambuliaji wengi au wachezaji wengi wanaofika hizi timu kubwa tayari wanakuwa wamepita katika timu za Ligi Kuu. Iwe humu ndani au wale wanaotoka nje. Mzize amefikaje?

Mchezaji aliyejiandaa mwenyewe, mchezaji ambaye hajawahi kucheza Ligi Kuu halafu ameibukia timu ya vijana ya Yanga, kisha timu ya wakubwa, imekuwaje ameibukia Yanga? Sio kitu cha kawaida sana. Ni mchezaji ambaye amejiandaa zaidi mwenyewe.

Historia ya nyuma kabla ya kwenda Yanga, hata haijulikani. Lakini hizi timu katika miaka ya hivi karibuni zimejaribu kuchukua wachezaji wengi waliotamba Ligi Kuu na kuwaweka katika vikosi vyao hakuna aliyemfikia Mzize.

Kina Adam Salamba, Waziri Junior, Yusuf Mhilu na wengineo. Hawa walichukuliwa kukiwa na matumaini kwamba wangekuwa washambuliaji wa ndani ambao wangefuata nyayo za John Bocco. Hata hivyo, hawakufanikiwa. Walau Mzize huyuhuyu ameonyesha cheche na thamani kubwa kwa taifa kiasi cha kuitwa katika vikosi kadhaa vya timu ya taifa.

Katika zama hizi ambazo wageni wamekuwa wakitamba katika maeneo ya ushambuliaji usingeweza kufikiria kama Mzize angetoboa kwa namna ambavyo kumekuwa na upinzani mkubwa wa nafasi. Hata hivyo, amefanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Ilianzia kwa kuonekana mbadala wa Fiston Mayele pindi anapokuwa amechoka uwanjani. Lakini hapohapo alikuwa akipambana na kina Kennedy Musonda. Hata alipokuja Hafiz Konkoni ilionekana ni bora uwanjani uwe na Mzize kuliko staa huyo wa Ghana.

Ukweli ni kwamba hatujawekeza sana kwa Mzize na chochote anachofanya kwa sasa ni kama maajabu. Kuibukia katika kikosi cha kwanza cha Yanga ukilinganisha na mwanzo wake ulivyokuwa nadhani tunapaswa tu kumtia moyo.

Ana mambo mengi ya kujifunza katika soka kuliko kumbebesha lawama. Nadhani kosa pekee ambalo anafanya kwa sasa ni kuibukia katika kikosi cha kwanza cha timu ambayo ina mashabiki wengi nchini. Ghafla presha inakuwa kubwa kuliko hali halisi.

Hata hivyo, ukimtazama tu Mzize haraka haraka ukweli ni kwamba amefunga mabao mengi kuliko ilivyotakiwa. Tayari ametuachia kumbukumbu nyingine, ingawa kama angefunga dhidi ya Mamelodi basi ingekuwa kumbukumbu nyingine ya kusisimua kutoka kwa dereva wa bodaboda.

Mzize hadi sasa hivi yuko njia panda ya kuwa mchezaji hatari. Inabidi aendelee kupata makocha wa kumfua zaidi huku yeye mwenyewe akijibidiisha katika kukinoa kiwango chake. Wakati mwingine inabakia kuwa kazi ya mchezaji binafsi kuliko makocha.

Nani alimfikisha Mbwana Samatta kuwa mshambuliaji hatari? Kuna makocha wa Mbagala ambao walisababisha Samatta awe hatari sana kiasi cha kucheza Ligi Kuu ya England? Mbona makocha hawa hawatuletei wachezaji wengine hatari wakacheza Genk na England?

Suala hili ni la Mzize zaidi na inabidi tumtie moyo na sio kuanza kumlaumu na kumpuuza. Hili linatokea huku dunia ikiwa na upungufu mkubwa wa washambuliaji. Hata Tanzania yenyewe ina upungufu mkubwa wa washambuliaji, ndio maana kwa muda mrefu katika soka la ndani hatuna mshambuliaji mwenye mwendelezo wa ubora kama John Bocco na hata sasa hivi anaonekana ameisha bado hatujui nani atakuwa mrithi hasa wa Bocco.

Pamoja na hilo nafahamu kwamba Mzize amewapita kwa uwezo washambuliaji kibao barani Afrika. Ana nguvu, ana kasi, na anaweza kufunga ingawa analazimika kuongeza jicho la lango. Sio washambuliaji wengi tunaowasikia na kuwasifu wanaweza kufikia uwezo wake. Mfano ni bao alilowafunga Dodoma Jiji Jumatano usiku pale Dodoma.

Haikushangaza kuona kocha wa Mamelodi, Rulani Mokwena akimtaja kama mshambuliaji hatari wakati akimchambua mchezaji mmoja mmoja katika kikosi cha Yanga. Huu ndio ukweli ambao Watanzania hatuwezi kuukubali kwa haraka kwa sababu tumezoea kuvibeza vya kwetu.

Tuwekeze zaidi kwa Mzize kwa sababu katika soka la kileo, hata ukiachana na Mzize ni wazi utapata shida kupata mshambuliaji mwingine kiurahisi. Kwa mfano tu, hivi ambavyo Samatta na Simon Msuva wanavyoelekea mwisho katika maisha yao ya soka la kishindani unatazamia nani mwingine aongoze safu ya ushambuliaji ya Taifa Stars zaidi ya Mzize?

Unatazamia nani aongoze safu ya ushambuliaji kama tukifika AFCON pale Morocco? Na kama tukiendelea kuwekeza katika Mzize unatazamia nani aongoze safu ya ushambuliaji ya Taifa Stars katika michuano ambayo tutaandaa wenyewe mwaka 2017.

Mzize sio mchezaji wa kunyooshewa kidole sana. Tuwashukuru tu Yanga kwa kumlea ingawa amejilea zaidi mwenyewe na juhudi zake. Mchezaji ambaye hakucheza daraja lolote na kuonyesha makali ghafla anaibukia katika kikosi cha kwanza na kuonyesha makali yake, inatokea nadra sana kwa wachezaji wa zama hizi hasa linapokuja suala la timu kubwa.

Columnist: Mwanaspoti
Related Articles: