Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Nchi za EAC ziungane kuzuia vifo, mauaji

Mauaji Shahidi Nchi za EAC ziungane kuzuia vifo, mauaji

Tue, 1 Feb 2022 Chanzo: www.habarileo.co.tz

‘Bomu laua 10 kwenye Daladala’ na abiria takribani 10 wamekufa na wengine kujeruhiwa baada ya gari la abiria maarufu matatu (daladala) kukanyaga bomu lililokuwa limetegwa kwenye Barabara Kuu ya Arabia-Mandera jijini Nairobi, Kenya.

Tukio hilo la jana limetokea huku mara kadhaa kukiwa na taarifa za mashambulizi yenye sura za ugaidi katika nchi hiyo na nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Miongoni mwa nchi za EAC ambazo kumekuwa kukisikika taarifa za mashambulizi ‘yasiyoeleweka’ ni Uganda, huku mengine yakifanywa kama matokeo ya uhalifu katika jamii.

Nchini Tanzania, kumeripotiwa mfululizo wa matukio ya mauaji ya kikatili yakiwamo yanayohusisha ndugu wa familia moja. Mbali na hayo, kumekuwa na taarifa nyingi katika nchi za EAC kuhusu vifo na majeruhi kutokana na ajali za barabarani ambazo mara nyingi zinatajwa na mamlaka husika kuwa kwa kiasi kikubwa hutokana na uzembe na makosa ya binadamu.

Ajali nyingine ambazo zimekuwa kero katika nchi za EAC katika siku au miaka ya karibuni, ni zile zinazotokana na matukio ya kuzuka kwa moto katika majengo yakiwamo ya watu binafsi na kuporomoka kwa majengo yaliyo katika hatua za ujenzi huku ‘ugonjwa’ wa watu kujichukulia sheria mikononi ukichangia pia mauaji katika jamii.

Sisi tunasema, umefika wakati sasa watu wa nchi wanachama wa EAC ndani ya nchi na ndani ya kanda, kushirikiana kuchunguza, kubaini, kufichua na kuzuia dalili au mipango yote inayoweza kusababisha vifo au mauaji vikiwamo vitendo vya kigaidi, mauaji ya kikatili miongoni mwa jamii, ajali na hata majanga ya asili kama mafuriko.

Watu wa EAC waungane kutoa elimu sahihi na taarifa kuhusu dalili za kufanyika vitendo vya uhalifu, watoe taarifa kuhusu mwendo wa vyombo vya usafiri unaotishia usalama wa raia na mali zao na pia watoe taarifa kwa mamlaka husika kuhusu ujenzi usiozingatia viwango kwani nao unahatarisha usalama wa raia na mali zao.

Tunasema ushirikiano baina ya nchi na nchi katika EAC uimarishwe ili wahalifu wakiwemo magaidi wasipate upenyo wa kuingia nchi yoyote maana kama jirani yako hayuko salama, ni wazi hata wewe hauko salama.

Katika nchi zote urudishwe na kuanzishwa utaratibu wa kila mgeni katika kila kaya kutambulishwa katika mamlaka na jamii ya eneo husika. Watu wasiojulikana katika makazi ya watu au dalili za watu porini zianikwe hadharani.

Ukaguzi wa vyombo vya usafiri au majengo usifanywe popote kwa lengo la kuongeza kipato, bali kuzuia madhara na kubwa zaidi, maadili na utu vitiliwe mkazo tangu ngazi ya familia kwa watoto. Ndio maana tunasema, nchi za EAC ziungane kuzuia vifo, mauaji.

Columnist: www.habarileo.co.tz
Related Articles: