Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yaomba muda kesi ya kumteka mwanamke Dar

Ceo D . Law Serikali yaomba muda kesi ya kumteka mwanamke Dar

Fri, 17 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iwape muda ili wazifanyie kazi barua za maombi ya kukiri mashtaka iliyoandikwa na washtakiwa wa kesi ya unyang'anyi wa kutumia silaha na kumteka mwanamke na kisha kumuibia vitu mbalimbali inayowakabili Assad Abdulrasur (43) na wenzake sita.

Ombi hilo limetolewa jana, Novemba 16, 2023 na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga wakati kesi hiyo ya jinai namba 196/2023 ilipoitwa kwa ajili ya kuanza kusikilizwa ushahidi wa upande wa mashtaka.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni unyang'anyi wa kutumia silaha na kumteka na kumshikilia mwanamke aitwaye, Han Nooh Hussein, kinyume cha Sheria.

Itakumbukwa kuwa Oktoba 30, 2023 washtakiwa hao walimuandikia barua Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) wakiomba kukiri mashtaka yao na kupunguziwa adhabu.

Wakili Mwanga alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Aaron Lyamuya kuwa upande wa mashtaka umepokea barua za washitakiwa hao waliomba kukiri mashitaka yao, hivyo aliiomba mahakama iwape muda waweza kufanyia kazi maombi yao, wawape majibu.

Kutokana na hali hiyo, Hakimu Lyamuya alikubaliana na ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi Novemba 30, 2023 kwa ajili ya kutajwa.

Mbali Abdulrasur, ambaye ni mkazi wa Msasaani Village;  washtakiwa wengine ni Fahad Mussa (32) mkazi wa Airport Dodoma; Nathan Jothan (27)mkazi wa Sinza na Nicolas Nilahi (39) mkazi wa Wazo Hill.

Wengine ni Fredu Chahoza (49) mkazi wa Dodoma; Ifan Saleh (41) mkazi wa Kisemvule na Hassan Nur (39) mkazi wa Msasani Village A.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, katika shtaka la kwanza ambalo ni unyang'anyi wa kutumia silaha, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kutenda kosa hilo, Oktoba 16, 2023 katika eneo la Msasani Beach.

Inadaiwa siku hiyo ya tukio, washtakiwa kwa pamoja waiiba simu aina ya iPhone yenye thamani ya Sh3.5 milioni; miwani moja ya macho yenye thamani ya Sh300, 000; pea moja hereni za dhahabu zenye thamani ya Sh500, 000; saa ya mkono yenye thamani ya dola za kimarekani 120.

Vingine ni pochi moja iliyokuwa na fedha taslimu Sh100, 000, vyote vikiwa mali ya Han Nooh Hussein na kwamba washtakiwa hao kabla ya mlalamikaji huyo kwa bastola aina ya Glock 19, ili waweze kujipatia vitu hivyo bila kikwazo.

Shtaka la pili ni kuteka na kumzuia mlalamikaji kwa siku nne, ambapo washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kutenda kosa hilo, Oktoba 16, 2023 eneo la Msasani Beach, lililopo wilaya Kinondoni.

Siku hiyo washitakiwa hao walimteka Hani kwenda Mtaa wa Ujirani, Mbezi Beach ambapo kwa siri na nia ovu, walimteka na kumzuia kwa siku nne ndani ya nyumba ya Haidary Waziri.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: