Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mzee aliyechukuliwa na wasiojulikana auawa kikatili

 Agostino Senga Mwez Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Agostino Senga.

Thu, 18 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kuminya Sambo (63), mkazi wa Kijiji cha Nambizo, wilayani Mbozi, mkoani Songwe, amekutwa akiwa ameshafariki dunia, akidaiwa kuuawa na watu wasiojulikana kisha mwili wake kutupwa msituni kijijini huko.

Taarifa zilizothibitishwa na ndugu pamoja na uongozi wa kijiji zinadai kuwa mzee huyo ambaye hakuwa na mke, alitoweka nyumbani kwake siku kadhaa kabla ya kukutwa akiwa ameuawa, huku viungo vya mwili wake ikiwamo mguu na mkono vikiwa vimenyofolewa.

Mmoja wa watoto wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Jose Kuminya, alisema baba yao alikutwa ameuawa baada ya kutoonekana kwa siku tatu.

Jose alisema Mzee Sambo alipotoweka nyumbani usiku wa Julai 9 mwaka huu, walianza kumtafuta kwa kushirikiana na wananchi hadi siku ya tatu Julai 11, mwaka huu walipokuta mwili wake umetelekezwa kando ya njia katika msitu kijijini huko, huku mguu mmoja na mkono vikiwa vimenyofolewa.

Alisema kuwa mazingira yaliyokutwa nyumbani kwa baba yao ambaye alikuwa akiishi peke yake, siku aliyotoweka yalizua hofu kubwa kwa kuwa walikuta hakuna dalili zilizoonyesha kama nyumba ilivunjwa.

"Mlango haukuvunjwa, hali inayoonesha watu waliomchukua baba na kwenda kumuua, waliondoka naye baada ya kumgongea na yeye kuwafungulia mlango kwani hata pombe aliyokuwa akitumia usiku ule ilikutwa kwenye kopo ikiwa pembeni," alidai Jose aliyesimulia tukio hilo kwa hisia kali.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Namanga kijijini huko, Jackson Ntembo, alithibitisha kutokea tukio hilo na kusema kuwa baada ya kupewa taarifa za kutoweka kwa Mzee Sambo, walianza msako, hatimaye kumkuta akiwa amefariki huku akiwa amekatwa kwa kitu chenye ncha kali kifuani na kichwani huku mguu mmoja na mkono vikiwa vimenyofolewa.

"Daktari aliufanyia uchunguzi mwili wa marehemu na kukuta una majeraha manne ambayo yalisababishwa na kukatwa na kitu chenye ncha kali, na mimi kama kiongozi, ninaliomba Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi zaidi kuhusu tukio hilo," alisema Ntembo. 

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Gallus Hyera, alithibitisha kutokea tukio hilo na wanaendelea na uchunguzi. Hadi jana, hakuna mtu aliyekuwa amekamatwa kuhusiana na tukio hilo.

Wilaya ya Mbozi imekuwa na matukio ya mauaji. Hivi karibuni, watu wasiojulikana walimuua aliyekuwa Mfamasia wa Kituo cha Afya cha Isansa, wilayani hapa, Daudi Kwibuja (30) na mwili wake kukutwa kando ya barabara kuu ya Mbeya-Tunduma (Tanzam) katika eneo la Mlowo.

Mwili wa mtumishi huyo ulikutwa ukiwa na majeraha. Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Agostino Senga, ilibainisha kuwa uchunguzi ulionesha majeraha katika mwili wa marehemu hayakuwa ya ajali ya kugongwa na gari. Awali ilidhaniwa kuwa mfamasia huyo alifariki dunia kwa ajali ya gari.

Kama ilivyo kwa tukio la Mzee Sambo kuuawa na kunyofolewa viungo, hadi jana hakuna mtuhumiwa aliyekuwa amekamatwa na Jeshi la Polisi dhidi ya mauaji ya mfamasia huyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: