Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtoto atuhumiwa kumuua mdogo wake

Mauaji Nn.jpeg Mauaji

Sat, 2 Jul 2022 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mtoto wa kike mwenye umri wa miaka minne ameuawa wilayani Chunya mkoani Mbeya kwa kupigwa na kitu kizito kichwani na mtu aliyetajwa kuwa ni kaka yake wa kuzaliwa naye.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei ilisema mauaji ya mtoto huyo, Wile Limbe, yalifanyika Juni 29 mwaka huu nyumbani kwao katika Kitongoji cha Nselewe kilichopo Kijiji cha Mapogolo, Kata ya Chokaa wilayani Chunya.

Kamanda Matei alimtaja anayetuhumiwa kuhusika na mauaji hayo kuwa ni kaka wa Wile, Masanja Mafurahia (13) huku chanzo kikiwa hakijafahamika ingawa taarifa za awali zinadai kuwa mtuhumiwa ana tatizo la kiafya la utindio wa ubongo.

Hata hivyo, taarifa ya Kamanda Matei haikueleza walipokuwa wazazi wa watoto hao wakati wa tukio hilo.

“Tunaendelea na uchunguzi juu ya chanzo cha tukio hili na mtuhumiwa ambaye ni kaka wa marehemu amekamatwa na anaendelea kuhojiwa. Mwili umefanyiwa uchunguzi na daktari na kukabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Kamanda Matei kupitia taarifa hiyo alitoa wito kwa wazazi na walezi kuweka uangalizi makini kwa watoto wao wenye matatizo ya afya ya akili kuepuka matukio kama hayo yasitokee tena.

Alitoa pia wito kwa jamii yenye watoto, ndugu, jamaa na marafiki wenye matatizo ya afya ya akili kuwafikisha hospitali au vituo vya afya kwa matibabu zaidi.

Ulinzi na usalama wa mtoto ni miongoni mwa vipengele muhimu vinavyosisitizwa katika Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM).

Chanzo: www.habarileo.co.tz
Related Articles: