Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtikisiko Sungusungu sita wakihukumiwa kunyongwa Manyara

Pingu Law Mtikisiko Sungusungu sita wakihukumiwa kunyongwa Manyara

Thu, 7 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ni mtikisiko Kiteto, ndivyo unavyoweza kusema baada ya Mahakama Kuu masjala ndogo ya Manyara, kuwahukumu kifo walinzi wa jadi ‘Sunsusungu’ sita kwa kumuua kikatili mtu waliyemtuhumu kuwa mwizi wa mifugo.

Maelezo ya onyo ya kukiri kosa ya washtakiwa wote sita waliyoyaandika polisi kwa hiyari yao, ndio ushahidi mzito uliowatia hatiani kutokana na maelezo hayo kueleza hatua kwa hatua tangu wanamkamata marehemu na kisha kumuua.

Waliohukumiwa kunyongwa ni pamoja na aliyekuwa mshtakiwa wa kwanza, Samwel Mgomelwa aliyekuwa kamanda wa Sungusungu na ambaye washirika wake walimtaja katika maelezo hayo kuwa ndiye aliyetoa amri ya kuua.

Wengine ni Ramadhan Idd, Manda Ulinje, Amini Masilimu, Elia Lendama na Andarson Chuyo na Jaji akawaambia wana haki ya kukata rufaa kama hawajaridhika na hukumu.

Katika hukumu hiyo iliyotolewa Machi 5, 2024 na Jaji Gladys Barthy na nakala ya hukumu kupatikana katika mtandao wa Mahakama leo Alhamisi, Machi 7, 2024, Mahakama iliwaachia huru sungusungu watatu kwa kukosekana ushahidi dhidi yao.

Walioachiwa huru ni George Kaonwa, Yasin Ally na Lameck Paulo ambao Jaji amesema ushahidi pekee uliowagusa ni maelezo hayo ya onyo ya washtakiwa ya kukiri kosa, lakini hapakuwa na ushahidi huru kuunga mkono ushahidi huo.

Kulingana na maelezo, imedaiwa Septemba 2, 2020 katika eneo la Kazingumu lililopo Kijiji cha Laalaa katika wilaya ya Kiteto mkoa wa Manyara, washtakiwa walimuua Njokuti Moringe maarufu kama Mbaazi na kisha kuchimba shimo na kumzika.

Ili kuthibitisha mashitaka hayo, upande wa mashitaka uliita mashahidi 11 na kuwasilisha vielelezo nane yakiwamo maelezo ya washtakiwa na simu ya marehemu aina ya Itel iliyokutwa nyumbani kwa mmoja wa washtakiwa hao.

Maelezo ya ungamo Miongoni mwa maelezo hayo ya kukiri kosa ni ya aliyekuwa mshtakiwa wa nane, Elia Lendama anasema siku ya mauaji hayo alisikia filimbi na alipofika aliwakuta Sungusungu wenzake aliowataja kwa majina ya Rama, Lameck Yasin na wengine.

“Pia nilimkuta mwenye nyumba Samwel Mgomelwa (mshitakiwa wa kwanza). Tulikuta kelele za Masai anayejulikana kwa jina la Mbaazi akiwa amelewa pombe ya kienyeji aina ya Kangala ambayo inauzwa hapo nyumbani kwa kiongozi wetu”.

“Baadhi ya sungusungu nikiwamo mimi Rama, Yasin, Amini, George, Mandan a Lameck tukaanza kumsukuma Masai. Tulianza kumpiga, ili aondoke ambapo mimi nilimpiga kwa kutumia fimbo kwenye mgongo,”anaeleza katika maelezo hayo.

“Ramadhan alimpiga kwa kutumia nondo kichwani akaanguka moja kwa moja na alimrudishia tena nondo ya utosini na damu ikaanza kumwagika chini tena nyingi. Tukagundua kuwa amefariki,” ameendelea kueleza na kufafanua kuwa;-

“Tukamfunga shingoni kwa sababu alikuwa mtu mnene na mfupi pia damu nyingi ilimwagika ndipo alifungwa shingoni tukaanza kumburuza kisha tukamweka kwenye shimo na kumfukia,” anaeleza katika sehemu ya maelezo yake hayo.

Ulinje yeye alieleza,“Tukiwa kwenye doria tulifika kwa mwenyekiti wa Sungusungu na kutuambia kuna Mmasai. Kwamba huyo Mmasai ni mwizi wa ng’ombe na mbuzi na kusema ni msumbufu pale kijijiji. Akaagiza tumuue.”

Maelezo ya mshitakiwa wa tisa, Andason Chuyo anaeleza “…Tuliitwa na Kamanda wetu wa Sunsunsungu aitwaye Samwe; Mgomelwa nyumbani kwake. Akatuambia inatakiwa (Mmasai) apigwe kwani inaonekana ni mwizi wa mbuzi”

“Samwel Mgomelwa alitoa amri ya kimkamata Mbaazi na kutuambia tumpeleke bondeni na kummaliza… Wakati tunampiga mimi nilikuwa na fimbo na nilimpiga mgongoni. Baada ya kuona Mbaazi amekufa mimi nilikimbia,” aliekeza Chuyo.

Maelezo ya ungamo kukiri kosa ya washtakiwa wengine hayatofautiani kimaudhui na maelezo ya washitakiwa hao isipokuwa ya mshtakiwa Mgomelwa, anayetajwa kuwa kamanda wa Sungusungu na aliyetoa amri ya kuua.

Yeye anaeleza kuwa ”Tulimpekua (baada ya kufa) na Ramadhan alichukua Sh20,000 na kuamua tugawane pesa hizo. Amin Masilimu yeye alichukua simu. Nikawaambia waende nyumbani kuchukua majembe tuchimbe shimo tumzike”.

Hukumu ya Jaji ilivyokuwa Katika hukumu yake, Jaji Gladys Barthy amesema kwa kuchukua ushahidi uliopo katika maelezo ya onyo ya washtakiwa, ni ushahidi walieleza kwa kina nini hasa kilitokea na walichokifanya usiku wa siku ambayo Mbaazi anauawa.

“Ushahidi huu uliunganika na ule wa mashahidi wengine wa Jamhuri kuhusiana na tarehe ya kosa lilipotendeka, sababu ya washtakiwa kukamatwa na makachero wa Polisi na kukikiri kwao kuhusika katika kumuua marehemu,” amesema Jaji.

“Sio tu kwamba washtakiwa walikiri kutenda kosa hilo, lakini pia waliwaunganisha na wauaji wengine kutokana na maelezo yao yanayofanana kimaudhui kutoka mshtakiwa mmoja hadi mwingine,”alisema Jaji Barthy na kuongeza kusema:-

“Mahakama imefanyia kazi madai ya washtakiwa kuwa walilazimishwa kutoa maelezo hayo, lakini hata hivyo Mahakama haikuona hoja yenye mashiko kutilia mashaka kuacha kuyapokea maelezo hayo kama kielelezo cha kesi hii.”

Kuhusu washitakiwa watatu walioachiwa huru, Jaji amesema ushahidi pekee uliojaribu kuwaunganisha na mauaji hayo unatokana na maelezo ya kukiri kosa ya washtakiwa wengine, ambao hata hivyo haukuungwa mkono na ushahidi huru.

Kwa hiyo Jaji akasema anawatia hatiani mshitakiwa wa 1,2,3,4,8 na 9 ambao ni Mgomelwa, Idd, Ulinje, Masilimu,Lendama na Chuyo kwa kosa la mauaji na kwamba kisheria kwa kosa la mauaji ya kukusudia, adhabu ni moja tu nayo ni kifo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: