Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kortini wakituhumiwa kujifanya maofisa wa Tigo

Ceo D . Law Kortini wakituhumiwa kujifanya maofisa wa Tigo

Thu, 20 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakazi wa Kashai wilayani Bukoba Mkoa wa Kagera, Anicet Kamugisha (27) na Deodatus Tarazias (24) wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka 10 yakiwemo ya kujipatia Sh463,725 kwa njia ya udanganyifu.

Washtakiwa wanadaiwa kujipatia fedha hizo kwa kuwapigia simu watu mbalimbali na kujitambulisha kuwa wao ni maofisa watoa huduma kutoka kampuni ya Tigo na kisha kuwadanganya watumiwe pesa hizo ili wapokee gawio la Sh2.3milioni, wakati wakijua kufanya hivyo kosa.

Kamugisha na Tarazias wamesomewa mashtaka yao leo, April 19, 2023 na Wakili wa Serikali Ashura Mnzava mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ramadhani Rugemarila.

Ktika shtaka kwanza washitakiwa hao kwa pamoja kati ya Januari Mosi na Januari 10, 2023, katika eneo lisilofahamika ndani ya Tanzania kupitia namba za simu za mkononi walikula njama ya kutenda kosa la kujitambulisha isivyohalali nafasi zao isivyohalali.

Shtaka la pili na la tatu, Inadaiwa Februari 12, 2023 kupitia simu za simu ambazo zipo aina tatu, Washtakiwa hao waliojitambulisha kwa Zuhura Ally kama maofisa watoa huduma wa Tigo wakati akijua sio kweli.

Mnzava amedai shtaka la nne hadi la nane, inadaiwa Kamugisha na Tarazias wakiwa katika eneo la Kashai, Bukoba mkoani Kagera waliitumia namba za simu zilizosajiliwa kwa majina ya Benezeti Kaboyo, Alicia Laulent, Adolosta Kokusima, Monika Kahauza na Claudia Mkanyiganya bila kutoa taarifa kwa watoa huduma.

Shtaka la tisa, Kamugisha na Tarazias wanadaiwa Februari 12, 2023 kwa nia ovu walijipatia Sh201,225 kutoka kwa Zuhura Salum Ally kwa kumdanganya kwamba atapokea Sh1.5 milioni kama gawio kutoka katika huduma za Tigo, jambo ambalo walijua ni uongo.

Wakili Mnzava aliendelea kudai katika shtaka la 10, washtakiwa hao wanadaiwa Februari Mosi 2023 katika eneo hilo la Kashai, kwa nia ovu walijipatia Sh262,500 kutoka kwa Pili Mohammed Bakari kwa madai kwamba atapokea Sh800,000 kama gawio kutoka katika huduma za Tigo, jambo ambalo walijua ni uongo.

Baada ya kusomewa mashtaka yao, washtakiwa wamekana kutenda makosa hayo na upande wa mashtaka umedai kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuwasomea hoja za awali (PH).

Kwa kuwa mashtaka yanayowakabili yana dhamana kwa mujibu wa sheria, Hakimu Rugemalira ametoa masharti ya dhamana ambayo ni kila mshtakiwa anatakiwa kusaini hundi ya Sh500,000.

Pia wanatakiwa wawe na wadhamini wawili wanaotambulika kisheria na wawe na barua ya utambulisho utoka Serikali za Mitaa.

Hata hivyo, Washtakiwa hao wameshindwa kutimiza masharti ya dhamana na kurudishwa rumande. Hakimu Rugemarila ameahirisha kesi hiyo hadi Mei 2, 2023.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: