Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Daraja la Simba, Yanga CAF

Simba Vs Yangaaaaaaa Daraja la Simba, Yanga CAF

Mon, 9 Sep 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Raundi ya kwanza ya mashindano ya klabu Afrika itaanza mwishoni mwa wiki hii ambapo Tanzania itawakilishwa na timu mbili ambazo ni Yanga na Simba na zote zitaanzia ugenini katika mechi ya kwanza na wiki moja baadaye kucheza nyumbani.

Baada ya kuitupa nje Vital’O ya Burundi katika raundi ya kwanza kwa ushindi mnono wa mabao 10-0 ilioupata katika mechi mbili za raundi ya kwanza, Yanga inayocheza Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu itakabiliana na CBE ya Ethiopia ambapo mchezo wa kwanza utachezwa huko Addis Ababa kisha zitarudiana visiwani Zanzibar hapo baadaye.

CBE ambayo itacheza na Yanga, ilitinga katika raundi ya pili baada ya kuitupa nje SC Villa ya Uganda kwa mabao 3-2.

Wapinzani hao wa Yanga, hawana historia yoyote kubwa kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwani ndio wanashiriki kwa mara ya kwanza lakini wamewahi kucheza Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2005 na 2010 ambapo waliishia raundi ya kwanza.

Simba yenyewe itakuwa ugenini huko Libya ikikabiliana na Al Ahli Tripoli ya huko katika mchezo wa raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika ambao utachezwa jijini Tripoli.

Ahli Tripoli ilitinga raundi ya pili baada ya kuitupa nje Uhamiaji ya Zanzibar kwa ushindi wa mabao 5-1 wakati Simba yenyewe ilipata mchekea baada ya kutinga raundi ya pili bila kucheza mechi yoyote.

Timu hiyo ya Libya imekuwa na historia nzuri kwenye Kombe la Shirikisho Afrika kwani imewahi kutinga hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo mwaka 2022 ambapo ilikwaa kisiki mbele ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini ambapo ilipoteza kwa mabao 2-1 katika mechi mbili baina yao.

Chati ya Caf inatamanisha

Kufanya vizuri katika mechi hizo kutazifanya Yanga na Simba zijihakikishie kutinga hatua ya makundi kwenye kila shindano ambalo kila moja ipo kwa upande mwingine ikiziweka katika nafasi nzuri ya kuongeza idadi ya pointi kutokana na ushiriki wao kwenye mashindano hayo ya klabu na hivyo kuzidi kupanda katika chati za ubora za klabu za Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf).

Yanga itakuwa katika nafasi nzuri ya kukusanya idadi kubwa ya pointi kwa vile timu inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika inapata idadi kubwa ya pointi kutokana na mafanikio inayofikia kuanzia hatua ya makundi kulinganisha na zile za Kombe la Shirikisho Afrika ambazo hazipati pointi nyingi labda tu zinapofanikiwa kuingia nusu au fainali.

Kwa chati ya sasa ya Caf, Simba iko nafasi ya saba ikiwa imekusanya pointi 39 na Yanga iko nafasi ya 13 ikiwa imevuna pointi 31.

Timu bingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika inapewa pointi sita wakati inayotwaa taji la Kombe la Shirikisho Afrika inavuna tano. Mshindi wa pili wa Ligi ya Mabingwa Afrika anapata pointi tano na kwenye Kombe la Shirikisho anapata pointi nne.

Inayoishia hatua ya nusu fainali katika Ligi ya Mabingwa Afrika inapata pointi nne na kwa upande wa Kombe la Shirikisho Afrika inapata pointi tatu.

Timu inayoishia robo fainali katika Ligi ya Mabingwa Afrika inavuna pointi tatu na katika Kombe la Shirikisho Afrika inakusanya pointi mbili huku inayomaliza katika nafasi ya tatu kwenye kundi katika Ligi ya Mabingwa Afrika inapata pointi mbili na kwa upande wa Kombe la Shirikisho Afrika inavuna pointi moja.

Pointi moja inapata timu ambayo inamaliza katika nafasi ya nne kwenye kundi katika Ligi ya Mabingwa Afrika na katika Kombe la Shirikisho inapata pointi 0.5.

Msako wa fedha

Kuingia hatua ya makundi ni zaidi ya kusaka heshima ya uwanjani kwani pia kutazifungulia milango ya fedha Yanga na Simba kupitia njia tofauti.

Njia ya kwanza ni fedha zitokazo Caf kama zawadi kwa kila hatua ambayo timu inaingia kuanzia ile ya makundi hadi fainali.

Kitendo cha kutinga tu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kinaihakikishia timu kiasi cha Dola 700,000 (Sh 1.8 bilioni) na ile inayoingia hatua ya robo fainali inavuna Dola 900,000 (Sh 2.3 bilioni).

Bingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika anapata kiasi cha Dola 4 milioni (Sh10 bilioni), mshindi wa pili anapata kitita cha Dola 2 milioni (Sh 5 bilioni) na inayoishia nusu fainali inapata Dola 1.2 milioni (Sh3.2 bilioni)

Timu inayotwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika inapata kiasi cha Dola 1.5 miliono milioni (Sh4.1 bilioni) na inayoshika nafasi ya pili inapata Dola 1.4 milioni (Sh3.8 bilioni), Dola 600,000 (Sh1.6 bilioni) kwa inayoishia nusu fainali, kiasi cha Dola 300,000 (Sh816 milioni) kwa robo fainali, Dola 200,000 (Sh544 milioni) kwa nafasi ya nne kwenye kundi na inayoshika mkia katika kundi inapata Dola 100,000 (272 milioni) mtawalia.

Fedha nyingine ambazo Simba na Yanga zinaweza kuvuna ni zile za bonasi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ambaye anatoa Sh 5 milioni kwa kila bao linalofungwa na klabu ya Tanzania inayoshiriki mashindano ya klabu Afrika.

Makocha hesabu za ushindi

Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alisema kuwa anafahamu wanakutana na timu nzuri na imara ingawa ana imani wataweza kufanya vizuri.

“Tayari nimeshaanza kupata taarifa za wapinzani wetu ikiwemo mikanda ya video ya mechi ya kwanza dhidi ya Villa ya Uganda hivyo tunajipanga,” alisema Gamondi.

Kocha wa Simba, Fadlu Davids alisema kuwa wanakabiliana na Al Ahli Tripoli wakiwa wamekamilisha sehemu kubwa ya maandalizi yao.

“Al Ahli Tripoli ni timu nzuri na imekuwa na historia ya kufanya vizuri katika mashindano haya huko nyuma. Hata hivyo sisi ni timu kubwa na tunataka kuonyesha kwa kuvuka dhidi yao,” alisema Davids.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: