Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yaiandalia Coastal dozi nene

Simba Mwesss Simba yaiandalia Coastal dozi nene

Thu, 3 Oct 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Uongozi wa klabu ya Simba umesema wanaamini kocha wa timu hiyo, Fadlu Davids, amekiandaa vizuri kikosi chao kuhakikisha wanatoa dozi kubwa kwenye mchezo wa kesho dhidi ya Coastal Union.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally, amesema kocha pamoja na kuridhishwa na kiwango cha uchezaji wake, lakini hajaridhishwa na utumiaji nafasi katika michezo miwili ya mwisho dhidi ya Azam FC na Dodoma Jiji.

Ahmed, amesema kocha Fadlu anataka wachezaji wake watumie nafasi zinazopatikana hasa kipindi cha kwanza ili kuifanya mechi kuwa rahisi na isiyo na presha kipindi cha pili.

"Tuna kazi ya kumwonyesha Coastal Union kuwa hii ni Simba mpya kwa kumwandalia dozi nene, kocha anataka nafasi zinazopatikana zitumiwe kwa ukamilifu, katika michezo yetu miwili dhidi ya Azam FC na Dodoma Jiji ameona mapungufu kwani mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika katika mechi hizo, Simba tulitakiwa tuwe mbele hata kwa mabao matatu au manne, kwa hiyo kazi yake ni kurekebisha hilo ili Wagosi wa Kaya wawe mfano," alisema.

Hata hivyo, amesema haitokuwa mechi rahisi kama wachezaji wao hawatopambana kwani mara nyingi Coastal Union huwa ni wabishi wanapocheza dhidi ya Simba.

"Itakuwa mechi ngumu, kila mtu anahitaji pointi tatu, haitokuwa nyepesi kwa upande wowote ule, ila sisi tumejipangia kumaliza mechi tano za mwanzo kwa ushindi, tumeshinda nne, bado moja ili kukamilisha robo ya malengo tuliyojiwekea na kama tukifanikiwa hilo yatakuwa maendeleo makubwa kwetu," alisema Ahmed.

Kikosi cha Simba, jana kilianza mazoezi yake rasmi kujiandaa na mchezo huo, baada ya mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati yake na Dodoma Jiji uliochezwa Jumapili iliyopita, Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

"Kikosi kinaanza mazoezi leo (jana), kuelekea katika mchezo huo, baada ya kutoka Dodoma tulikuwa tunafanya mazoezi mepesi mepesi tu kwani tangu tutoke Libya kucheza na Al Ahli Tripoli vijana hawakupumzika, kocha akaamua kuwapumzisha kwa kuwapa mazoezi ambayo si magumu, lakini leo mazoezi rasmi ndiyo yanaanza," alisema.

Simba haijafungwa mchezo wowote wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union tangu msimu wa 2019/20, ikiwa imecheza michezo 12, ikishinda michezo 10 na sare mbili.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: