Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nafasi nyingine kwa Yanga

YANGA KIMATAFA M Kikosi cha Yanga

Sat, 26 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya kucheza mechi tano mfululizo bila kuruhusu bao, ni nafasi nyingine kwa safu ya ulinzi ya Yanga kuthibitisha ubora wake dhidi ya ASAS ya Djibouti katika mchezo wa marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye Uwanja wa Azam Complex, saa 11 jioni.

Chini ya kocha Miguel Gamondi, Yanga haijaruhusu bao lolote katika dakika 90 za mchezo ikianzia na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, Siku ya Mwananchi, kisha ikaibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Azam FC na suluhu na Simba kwenye Ngao ya Jamii.

Baada ya hapo ikaichapa ASAS mabao 2-0 katika mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika na mchezo wa tano ikaitandika KMC 5-0 kwenye Ligi Kuu msimu huu.

Ushindi wa mabao 2-0 ambao iliupata katika mechi ya kwanza iliyochezwa uwanjani hapo Jumapili iliyopita, ambao ilihesabika ipo ugenini, unaiweka Yanga katika hali ya kutokuwa na presha katika mechi ya leo.

Lakini pia inaamini ushindi mbele ya ASAS utaiweka katika hali nzuri kisaikolojia katika hatua inayofuata ambayo ni ya mwisho kabla ya makundi inayosaka kuingia kwa mara ya kwanza baada ya miaka 25, mara ya mwisho ilikuwa 1998.

Presha kubwa ipo kwa ASAS, ambayo inahitajika kuibuka na ushindi utakaokuwa na utofauti wa mabao mawili au zaidi ili isonge mbele, jambo ambalo halionekani kuwa na nafasi ya kutokea kutokana na ubora.

Kiwango bora kilichoonyeshwa dhidi ya KMC kinaonekana kutatoa fursa kwa kundi kubwa la wachezaji waliokuwemo kikosini katika mechi hiyo ya Ligi Kuu kuwamo katika mpango wa mchezo wa leo ingawa kuna uwezekano mkubwa kipa Djigui Diarra akarejea kikosini.

Historia inaonyesha kuwa hakuna msimu wowote ambao Yanga ilishinda mechi ya kwanza ugenini ya mtoano ya mashindano ya klabu Afrika na kisha wapinzani wakapindua meza na kupata ushindi.

Na pia awamu zote ambazo Yanga imecheza mechi mbili za nyumbani na ugenini za mashindano ya klabu Afrika katika ardhi ya Tanzania, haijawahi kupoteza, kutoka sare wala kuruhusu bao.

Wawakilishi hao wa Tanzania ikiwa watasonga mbele, watakutana na mshindi wa mchezo baina ya El Merrikh ya Sudan na Otoho ya Congo, ambazo katika mchezo wa kwanza zilitoka sare ya bao 1-1.

Kocha wa Yanga, Gamondi alisema kuwa pamoja na ushindi waliopata katika mechi ya kwanza, hawataidharau ASAS leo na amewataka wachezaji wake kuwa na umakini katika dakika zote 90 za mchezo.

"Tulishamaliza dakika 90 za mwanzo na mbele yetu tuna nyingine za kumalizia raundi hii huku tukiwa na mtaji wa ushindi katika mchezo uliopita. Pamoja na kufanya vizuri mwanzo, hatutakiwi kubweteka na badala yake tunapaswa kufanya vizuri katika mchezo huu ili tupate ushindi na pia tuwape furaha mashabiki wetu," alisema Gamondi.

Kocha msaidizi wa ASAS, Mohamed Kader Daher Ahmed alisema wana kibarua kigumu dhidi ya Yanga ingawa watajitahidi kupambana nao.

"Ukiangalia nafasi yetu ya kusonga mbele ni finyu na Yanga ndio wapo katika nafasi nzuri lakini huu ni mpira na lolote linaweza kutokea. Mchezo wa kwanza ulituonyesha baadhi ya udhaifu wa kufanyia kazi kabla ya mechi ya kesho (leo), hivyo tunasubiria kuona itakuaje," alisema Ahmed.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: