Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mapya yaibuka binti aliyedaiwa kubakwa

Jumanne Muliro Dsm Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro.

Fri, 9 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mapya yameibuka kuhusu tukio la unyanyasaji wa kingono binti, mkazi wa Yombo Dovya, Temeke, mkoani Dar es Salaam, ambaye baada ya ukatili uliofanyika dhidi yake, ameondolewa katika nyumba aliyokuwa amepanga.

Wakati hayo yakiibuka, wadau mbalimbali wa haki za binadamu na wanasaikolojia, wameendelea kujitokeza na kulaani kitendo alichofanyiwa binti huyo na kutaka sheria zichukuliwe dhidi ya wahusika na kwa uwazi.

Bintu huyo anadaiwa kufanyiwa ukatili huo na vijana watano na video yake kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii, kwa kile walichodai kuwa walitumwa na bosi wao kwamba alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mume wake. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Anna Henga, alipoulizwa jana na Nipashe walikofikia kuhusu kumfuatilia binti huyo ili kumsaidia kisheria, alisema baada ya kwenda wameambiwa nyumba aliyokuwa akiishi ameondolewa.

“Hatujampata. Timu yangu iliyokwenda kule Yombo Dovya, ilifika hadi ofisi ya serikali ya mtaa alikokuwa anakaa, wakasema binti huyo ameondolewa na hawajui yuko wapi. Alikuwa mpangaji kwenye moja ya nyumba huko.

“Alikuwa anakaa na mama yake ambaye alikuwa mgonjwa sana. Licha ya kwamba hatujampata, tunasubiri kesi itakapofikishwa mahakamani tutamsaidia msaada wa kisheria,” alisema.

WAZIDI KULAANI  Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania, Sheikh Alhad Mussa Salum, alisema tukio hilo ni la kinyama na kishenzi ambalo halijazoeleka ndani ya jamii na limebeba ukatili na udhalilishaji.

“Hata kama alitenda kosa hilo bado alilotendea ni ukatili ambao haupaswi kutendwa. Kama viongozi wa dini tunalilaani. Vijana wasitumike vibaya hapo mtu ana dhambi mara mbili ya kuzini na kumtendea mtu ukatili,” alikumbusha.

Sheikh Salim aliwasihi vijana wasikubali kuiga vitendo visivyofaa na wawe na hofu ya Mungu.

Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili na Kilutheri (KKKT), Dk. Emmanuel Mlyuka, ambaye ni mnasihi, alisema tukio hilo ni kiashiria kikubwa kuwa mmomonyoko wa maadili umeporomoka katika jamii.

“Kukosekana kwa hofu ya Mungu ambayo ni tatizo la kiroho, huondoa utu na kutomjali binadamu mwingine na kushindwa kumchukulia kama binadamu na kumwona kama mnyama. Hicho ni kitendo cha ukatili,” alisisitiza.

Pia alisema kitendo hicho kinaashiria changamoto ya afya ya akili kwa vijana kwa sababu mwenye akili timamu hawezi kufanya jambo hilo kwa kujirekodi na kutuma.

“Hili ni jambo linalopaswa kukemewa, wahusika wanapaswa kuchukuliwa hatua na umma ujue kwamba, wamechukuliwa hatua na taarifa zitolewe ili kudhibiti vitendo hivyo na kuwa fundisho kwa wengine,” alisema.

Alisema hatua zichukuliwe bila kuangalia sura ya mtu ili kutunza maadili ya taifa, kwa kuwa husambaa duniani na kuleta aibu na yana maumivu ya kisaikolojia na mwili kwa mhusika pamoja na familia.

“Huyu binti anahitaji msaada wa kisaikolojia ili kulinda afya yake ya akili vinginevyo tutampoteza. Wazazi wake wanajisikiaje? Nao wameathirika wanahitaji kusaidia kupata msaada wa kisaikolojia.

“Kama sisi tumeumia kiasi hiki unadhani wazazi, wadogo zake, wameumiaje? Wanahitaji msaada pia wa kiroho ili kuwalinda wasipate matatizo mengine,” alishauri.

Agosti 4, mwaka huu, katika mitandao ya kijamii kulisambaa video ikionesha namna vijana watano wakimfanyia ukatili huo binti huyo huku wakimrekodi.

Katika video hiyo vijana hao walisikika wakimtuhumu kutembea na mume wa mtu na binti huyo akisikika kuomba msamaha mtu aliyetambulishwa kama afande.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: