Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kilichojificha matukio ya watoto kujinyonga

Mauaji DRC Crime Scene Kilichojificha matukio ya watoto kujinyonga

Tue, 11 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katika siku 12 zilizopita, kuna matukio matatu ya watoto kudaiwa kujinyonga nchini. Sababu za uamuzi huenda zisiwe na maana kwa mtu mzima, labda kwa watoto kutokana na uwezo mdogo wa kufikiri.

Wasaikolojia tiba na malezi wamesema kukosa malezi ya wazazi ni sehemu ya mambo yanayoweza kusababisha watoto kujiua - wanakosa mahitaji yao ya kihisia na stadi nzuri za kutatua matatizo yao ikiwamo uvumilivu, kujiamini na subira.

Wataalamu hao pia wamesema wazazi au walezi wanapopuuza mahitaji madogo ya watoto ambayo huendana na umri wao na kuwatimizia makubwa ambayo hayana msaada kulingana na umri wao, ni sababu nyingine inayoweza kuchangia uamuzi huo wa kujiua.

Mtazamo huo umeangaziwa na mwandishi baada ya kuripotiwa kwa matukio ya hivi karibuni ya watoto kudaiwa kujitoa uhai kutokana na sababu mbalimbali.

Yanaporejewa matukio matatu yaliyoripotiwa ndani ya siku 12 zilizopita kuanzia Juni 27, yanajumuisha la mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Mother Kelvin iliyoko Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, Alex Mgonja, alidaiwa kujinyonga kwa madai ya kukataliwa kupanda basi la shule wiki iliyopita.

Juni 27, mwanafunzi wa darasa la nne katika Kijiji cha Ikengwa, mkoani Dodoma, Zamada Jafari (13) alifariki dunia baada ya kudaiwa kujinyonga kwa kutumia mtandio, chanzo kikidaiwa kukosa nguo ya sikukuu.

Tukio lingine ni Jafari Mwashitete, mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Lumbira ya wilayani Mbozi, mkoani Songwe, anayedaiwa kujinyonga kwa kutumia tai huku akidaiwa kuacha ujumbe kwamba uamuzi huo wa kujitoa uhai umetokana na kutofurahishwa na kitendo cha wazazi wake kumhamishia katika shule hiyo.

WATAALAMU WANENA

Msaikolojia tiba, Dk. Saldeen Kimangale, kutoka Hospitali ya Somedics Polyclinic Health Centre ya jijini Dar es Salaam, alisema hivi karibuni kumekuwapo na matukio mengi ya watoto wadogo kukatisha uhai wao kwa sababu ambazo katika hali ya kawaida mtu hawezi kuchukua uamuzi kama huo.

Alisema ufuatiliaji wake umebaini watoto wengi wanaoripotiwa kujiua, hawaishi na wazazi wao, bali walezi ikiwamo bibi, babu na shangazi.

Mtaalamu huyo analitaja ni jambo linalosababisha watoto kukosa mahitaji yao ya kihisia kama inavyostahili, kukosa njia bora za kuwasilisha mahitaji yao na kukosa stadi nzuri za kutatua matatizo yao kama vile subira, uvumilivu, ujasiri na kujiamini.

Vilevile, aliwanyooshea kidole wazazi na walezi wengi wana majibu mepesi kwa mahitaji madogo ya watoto wao na kutimiza mahitaji makubwa ambayo wakati mwingine siyo ya msingi kulingana na umri wa mtoto.

“Kwa mfano, pipi kwa mtoto wa miaka minne au mitano ni bora sana kuliko simu ya iPhone 13. Sasa mzazi badala ya kumpatia mtoto pipi anayoihitaji anampa iPhone,” alifafanua.

Msaikolojia tiba huyo alisema hali hiyo wakati mwingine inasababishwa na wazazi kutowasikiliza na kuyafanyia kazi mahitaji na changamoto wanazopitia watoto wao na kuyachukulia kama jambo la kawaida kwa kuwa tu haijawatokea wao au iliwatokea na wakakabiliana nayo.

“Jambo lisilokuwa la maana au jambo la kawaida kwako wewe mtu mzima au tu mtu mwingine, huenda likawa muhimu sana kwa mtoto au mtu mwingine.

“Dhana hii imefanya tunayapuuza mahitaji ya msingi sana ya watoto wetu na hitaji kubwa kuliko yote ni kusikilizwa kwa umakini na kuwaelewa kile walichokusudia na kisha kukifanyia kazi,” alisema Dk. Saldeen.

Mtaalamu huyo pia alitaja sababu nyingine ni wazazi kutofuatilia mienendo na hisia za watoto wao. Anasema ni tabia inayochangia matukio ya kujiua.

“Mpaka mtoto anafikia hatua ya kujitoa uhai wake, alishafanya majaribio kadhaa ya kufanya tukio kama hilo huko nyuma,” alisema.

Dk. Saldeen anashauri wazazi na walezi wawe na muda wa kukaa na watoto wao kusikiliza mahitaji yao na wawasaidie kuufurahia utoto wao bila kuingiliwa na kupewa bughudha.

“Wazazi wajitahidi kuwatimizia watoto wao mahitaji yao ya msingi bila kupuuza, na pale panapokuwapo na ugumu, wawashirikishe watoto ili wasijenge dhana kuwa wamepuuzwa, wamekataliwa au hawana thamani au hawapendwi,” alisema.

Msaikolojia tiba huyo pia anashauri watoto wajengee uwezo kifikra na kufundishwa stadi mbalimbali za maisha ikiwamo kuwasiliana katika kuleta maana, stadi za kutatua matatizo na stadi za kukabiliana na msongo wa mawazo badala ya kuacha majukumu hayo kwa shule.

Mchungaji mstaafu wa KKKT, Richard Hananja, aliwataka wazazi na walezi kulea watoto wao katika misingi ambayo itawaondolea utegemezi ili kutengeneza kizazi ambacho kisichokata tamaa na kupambana na maisha hata pale wazazi wao watakapokuwa hawapo duniani.

“Kwa hiyo, sisi tunapanda nini? Watu wengi sasa wanatunza na sio kulea. Tunamwachia nini mtoto yule hata leo unapoondoka duniani? Unamwachia nini?

“Anaachiwa hali ya kujitegemea, kuona kuwa hata wazazi wakiwa hawapo wanaweza kuishi? Macho yake yanaona ushindi au anaona akifa mzazi, naye (mtoto) amekwisha?” Kiongozi huyo wa kiroho alihoji.

Alisema malezi maana yake ni kujenga au kupandikiza tabia mpya kwa mtoto na kuitaka jamii inapokuwa inapandikiza mambo hayo, kuzingatia malezi shirikishi na wajibu na kuachana na malezi telekezi na dekezi ya kuwapa watoto kila wanachohitaji kwa kuwa yanasababisha kujenga vijana wasiojiamini na waoga wa maisha.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: