Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bocco aisapraizi Simba Dar

BOCCO John Bocco

Wed, 26 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Siku chache tu baada ya kupewa 'Thank You' na Simba, aliyekuwa nahodha wa timu hiyo, John Bocco amewasapraizi Wekundu wa Msimbazi hao baada ya kupata timu mpya wakati wenyewe wakijiandaa kumuaga rasmi.

Bocco anayeshikilia rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa Ligi Kuu Bara akifunga mabao 154 katika misimu 16 akiipiku rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na Mohammed Hussein 'Mmachinga' aliyekuwa amefunga mabao 153 ndani ya misimu 13 amesajiliwa na JKT Tanzania kama kocha mchezaji.

Inadaiwa kuwa, Bocco amesajiliwa kama mchezaji na wakati huohuo akiwa pia ni kocha msaidizi wa timu hiyo, huku maafande hao wakilenga usajili huo uwabebe katika mambo matatu, ambayo ni uzoefu, nidhamu na ushawishi kwa wenzake.

Mwanaspoti linafahamu JKT Tanzania ipo hatua za mwishoni kabisa kumalizana na Bocco, wanayeamini uwepo wake katika kikosi chao, utaleta manufaa makubwa, kutokana na kuwa na asili ya uongozi ndani yake.

Mmoja wa viongozi wa timu hiyo (jina linahifadhiwa), amesema kwa asilimia kubwa mazungumzo na staa huyo yamekamilika, huenda muda wowote akasaini.

"Tuliposikia kaachwa rasmi Simba, hizo zilikuwa taarifa njema kwetu, hatukutaka kusita kuanza kufanya naye mazungumzo ya kumsajili, tuna asilimia 99 Bocco atakuwa sehemu ya JKT Tanzania," amesema kiongozi huyo na kuongeza;

"Ukizungumzia wazawa wenye thamani kubwa, mafanikio na nidhamu, jina la Bocco haliwezi kukosekana, katika mkataba wetu tumempa heshima kubwa anayostahili kulingana na jina lake."

Kiongozi huyo alisema ilikuwa ni matamanio yao kumpata Bocco kutokana na huduma nzuri aliyoitoa akiwa Azam FC na Simba na kuwa ni mfano wa kuigwa kulingana na mabao anayomiliki hadi sasa.

"Bocco amesomea ukocha, tulikuwa tunamfuatilia kwenye majukumu yake aliyokuwa amepewa na Simba kufundisha kikosi cha U-17, wachezaji wamefunga mabao mengi, ndio maana tunaona atakuwa mchezaji mzuri na kiongozi sahihi kwa wenzake," alisema.

DATA ZA BOCCO

AZAM FC

2008/2009(1)

2009/2010 (14)

2010/2011 (12)

2011/2012 (19)

2012/2013 (7)

2013/2014 (7)

2014/2015 (2)

2015/2016 (12)

2016/2017 (10)

Jumla mabao 84

SIMBA

2017/2018 (14)

2018/2019 (16)

2019/2020 (9)

2020/2021 (16)

2021/2022 (3)

2022/2023 (10)

2023/2024 (2)

Jumla mabao 70

Bocco tangu aanze kucheza Ligi Kuu Bara 2008 -2024 amefunga jumla ya mabao 154.

WASIKIE WADAU

Meneja wa zamani wa Simba, Patrick Rweyemamu alisema Bocco alijengwa katika misingi ya uongozi tangu akiwa mdogo, ambapo alifuatilia historia yake, aligundua alikuwa kiranja wakati anasoma.

"Historia ya Bocco inaonyesha namna ambavyo uongozi alianza tangu anasoma, amelelewa katika misingi ya soka, ameacha rekodi ya mabao, nidhamu na ukitaka kuamini hilo ni jinsi anavyosimamia kazi yake ya ukocha anavyoifanya na vijana anaowaongoza wanafurahia," alisema.

Rweyemamu alisema Bocco amefuata nyayo za kocha msaidizi wa Simba, Selemani Matola ambaye alijengwa katika misingi ya soka na ndio maana Simba inamwamini kumpa majukumu.

Kwa upande kocha Matola, alisema Bocco atakumbukwa kwa nidhamu yake na kwamba uwepo uwanjani ulimwakilisha kocha kulingana na ushawishi alionao kwa wachezaji wengine, hivyo alirahisisha kazi.

"Uwepo wa Bocco uwanjani ni kama kocha yupo uwanjani, alikuwa kiongozi mwenye ushawishi kwa wachezaji wenzake, kipindi cha unahodha wake alipata mafanikio ya kuchukua mataji mara nne mfululizo, pia ana rekodi nzuri ya ufungaji wa mabao," alisema Matola.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: