Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Anayedaiwa kuzaa na bintiye asomewa mashtaka

Mabula Masunga Jiumbi Pic Anayedaiwa kuzaa na bintiye asomewa mashtaka

Wed, 25 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baba anayedaiwa kuzaa watoto watatu na binti yake wa kumzaa, amepandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka yanayomkabili.

Mshtakiwa huyo, Mabula Masunga Jiumbi, mkazi wa Kitongoji cha Mbambe, Kijiji cha Mbunju-Mvuleni, Kata ya Mkongo, Wilaya ya Rufiji, mkoani Pwani, amepandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka hayo katika Mahakama ya Wilaya ya Rufiji, jana Jumanne, Oktoba 24, 2023.

Katika kesi hiyo, Mabula anakabiliwa na shtaka moja la kufanya ngono na maharimu, kinyume cha kifungu cha 158 (1) (b) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Penal Code -PC).

Akisoma mashtaka hayo, Mwendesha Mashtaka wa Serikali Mkaguzi wa Polisi (Insp) Justine Sanga amesema kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo kuanzia mwaka 2019 mpaka 2023.

Inspekta Sanga amesema kuwa katika kipindi hicho mshtakiwa huyo alikuwa akifanya ngono na binti yake wa kumzaa.

Hata hivyo mshtakiwa amekana kutenda kosa hilo na Inspekta Sanga ameieleza Mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo umeshakamilika na akaiomba Mahakama kuendelea na hatua inayofuata ya usikilizwaji wa awali yaani kumsomea mshtakiwa hoja za awali (maelezo ya muhtasari wa kesi).

Hakimu anayesikiliza kesi hiyo Flora Mujaya amekubaliana na ombi hilo la upande wa mashtaka na akaruhusu upande wa mashtaka kumsomea mshtakiwa maelezo hayo ya awali ya kesi hiyo.

Katika maelezo hayo Inspekta Sanga amesema kuwa mshtakiwa huyo, Mabula Masunga Jiumbi mwenye umri wa miaka 45, mpagani, na mkulima mkazi wa Mkongo na kwamba alimuoa Holo Seleli Rupile na kuzaa naye watoto 6; wavulana wanne wa wasichana wawili.

Mshtakiwa ameulizwa na Hakimu Mujaya kama maelezo hayo ni ya kweli naye akajibu kuwa ni kweli.   Inspekta Sanga pia amesema kwamba kuanzia mwaka 2019 alianza kufanya tendo la ngono na binti yake aitwaye Mwashi Mabula Masunga, lakini mshtakiwa baada ya kuulizwa na Hakimu amekana maelezo hayo akisema kuwa si kweli.

Inspekta Sanga vilevile amesema kwamba mshtakiwa huyo aliweza kumpa ujauzito mara tatu binti yake huyo na kumzalisha watoto watatu, maelezo ambayo pia mshtakiwa ameyakana kuwa siyo ya kweli.

Akiendelea kusoma maelezo ya kesi, Inspekta Sanga amesema kuwa baada ya taarifa kufika kituo cha Polisi Ikwiriri, mshtakiwa alikamatwa na kuhojiwa na upelelezi kufanyika, maelezo ambayo amekiri kuwa ni kweli alikamatwa na kupelekwa Polisi Ikwiriri.

"Baada ya upelelezi kukamilika ameletwa leo kwa ajili ya mashtaka," amehitimisha Inspekta Sanga na mshtakiwa pia akakubali kuwa ni kweli.

Kisha Inspekta Sanga ameieleza mahakama kuwa upande wa mashtaka watakuwa na mashahidi 6 na kielelezo kimoja na kwamba kwa leo wanaye shahidi mmoja.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Mujaya ameahirisha kesi hiyo kwa muda mfupi kabla ya kurejea kusikiliza ushahidi wa shahidi wa kwanza.

Mabula amefikishwa mahakamani hapo saa 4:09 asubuhi akiwa ndani ya gari ya Polisi aina ya Toyota Landcruiser PIckup, rangi ya Samawati lenye namba PT3718, akiwa pamoja na watuhumiwa wengine.

Baada ya kufikishwa mahakamani hapa yeye pamoja na watuhumiwa wenzake wengine wameshushwa na kuingizwa katika mahabusu ya mahakama hiyo wakiwa wamefungwa pingu wawiliwawili, ili kusubiri taratibu za kusajiliwa kwa kesi zao kisha wapandishwe kizimbani kusomewa mashtaka yanayomkabili.

Baada ya dakika 51, yaani saa 5:00 adhuhuri mtuhumiwa huyo na wenzake hao wamechukuliwa kutoka mahabusu na kupakizwa ndani ya gari hilo la Polisi lililowafikisha mahakamani hapo na kisha kuondoka nao.

Hata hivyo baadaye yeye peke yake akarudishwa tena mahakamani saa 8:23 na akiwa na mwenzake mmoja huku wakiwa wamefungwa pingu kwa pamoja na kupelekwa mahabusu ya mahakamani hapo hadi saa 9:30 alipopandishwa kizimbani na kisha kusomewa mashtaka hayo.

Mabula amepandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka hayo leo baada ya kutiwa mbaroni na Jeshi la Polisi Mkoa wa Polisi Rufiji Oktoba 17, baada ya gazeti la Mwananchi kuibua kashfa hiyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: