Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga, Simba zijipange raundi ya kwanza CAF

Simba Vs Yanga Mkwakwani Yanga, Simba zijipange raundi ya kwanza CAF

Mon, 28 Aug 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Raundi ya awali ya mashindano ya klabu Afrika imekamilika ambapo Tanzania tumefanikiwa kuingiza timu tatu katika raundi ya kwanza na ya mwisho kabla ya ile ya makundi ambayo ni lengo la msingi kwa timu nyingi ndani ya bara hili.

Na sio kufuzu tu bali pia wawaikilishi hao watatu tayari wameshafahamu wapinzani wao ambao watakutana nao kwenye raundi hiyo muhimu ya kuwaingiza kwenye makundi ambayo kila timu inayofuzu hapo inajihakikishia kupata fedha kulingana na nafasi ambayo itamaliza na aina ya mashindano inayoshiriki.

Simba ambayo yenyewe ilipata bahati ya kutoanzia raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, katika hatua ya kwanza itakutana na Power Dynamos ya Zambia ambayo imefanikiwa kuingia hatua hiyo baada ya kuitupa nje African Stars ya Namibia

Yanga ambayo nayo inashiriki mashindano hayo, imefanikiwa kutinga raundi ya kwanza kibabe baada ya kuitupa nje ASAS ya Djibouti kwa ushindi wa mabao 7-1 katika mechi mbili baina yao na itakutana na Al Merrikh ya Sudan ambayo imeitupa nje Otoho ya Congo, Brazzaville.

Wawakilishi wengine wa Tanzania waliotinga raundi ya kwanza ni Singida Big Stars ambao wameitoa JKU ya Zanzibar na wamepangwa kukutana na Future ya Misri ambapo wakipenya hapo wataingia katika hatua ya makundi.

Mambo hayakuwa mazuri kwa Azam FC, KMKM na JKU ambazo zenyewe hazikupata bahati ya kusonga mbele kwa kuishia katika hatua ya awali.

Baada ya kutamatika kwa raundi ya awali, muda umebakia mfupi kwa wawakilishi watatu waliobakia wa Tanzania kucheza raundi ya kwanza kama kalenda ya mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf) inavyoonyesha.

Katika Ligi ya Mabingwa Afrika, mechi za kwanza za raundi ya kwanza zitachezwa kati ya Septemba 15 hadi 17 na zile za marudiano zitafanyika kati ya Septemba 29 na Oktoba Mosi kama ilivyo katika Kombe la Shirikisho Afrika.

Ukiondoa Singida Big Stars ambayo inashiriki mashindano ya klabu Afrika kwa mara ya kwanza, Simba na Yanga zina uzoefu wa kutosha wa kucheza raundi ya kwanza na wengi wana matumaini kwamba zitafanya vizuri na kutinga hatua ya makundi.

Na ukiondoa uzoefu, zinakutana na timu ambazo hazionekani kuwa tishio sana kwao kiubora wa mchezaji mmojammoja na ule wa kitimu kulinganisha na baadhi ya miamba ya soka Afrika ambayo haijapangwa kukutana na timu hizo za Tanzania.

Hata hivyo pamoja na kwenye makaratasi kuonekana zina nafasi nzuri ya kutinga hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa Afrika, Yanga na Simba zinapaswa kuchukua tahadhari ya hali ya juu kwa wapinzani wao wajao ambao ni Al Merrikh na Power Dynamos.

Zinapaswa kufanya tathmini ya kina ya uimara na udhaifu wa wapinzani wao hao na kisha kuandaa mipango mikakati mizuri ambayo itazifanya zizitupe nje timu hizo na kuingia katika hatua inayofuata.

Katika upande huu wa maandalizi hakupaswi kuhusu benchi la ufundi na wachezaji tu bali pia hata uongozi na mashabiki kila upande kwa nafasi yao.

Viongozi wanapaswa kuhakikisha wanaandaa mazingira bora na mazuri ambayo yatawaweka wachezaji na makocha katika hali nzuri kisaikolojia itakayowapa ari ya kupambana ili wapafe matokeo mazuri.

Soka la Afrika limekuwa likitawaliwa na matukio mengi ya hujuma hasa ambayo timu zilizo ugenini zinafanyiwa ili kuvunjwa nguvu na kunufaisha upande mwingine, ambayo hufanyika kwa namna tofauti.

Ili kuepuka hayo, kunahitajika kazi kubwa kufanywa na viongozi ambayo itaendana na utengaji wa bajeti nzuri kifedha ya kuziwezesha timu hizo kujitegemea kwa kiasi kikubwa pindi zitakapokuwa ugenini ili kuondoa au kupunguza uwezekano wa kufanyiwa vitendo visivyofaa ambavyo vinaweza kuziweka katika wakati mgumu mashindanoni.

Mashabiki nao wanapaswa kuwa karibu na timu zao kwa sasa hadi pale muda wa mechi za raundi ya kwanza utakapowadia ili kuwapa deni wachezaji wao la kuhakikisha wanavuja jasho kusaidia timu zao ziweze kusonga mbele.

Mpira wa miguu umekuwa na matokeo mengi ya kushangaza yakiwemo yale ya timu ambazo hazipewi nafasi, kuchomoza na kutamba mbele ya zile ambazo wengi kwa jicho la kawaida waliona zingeweza kutamba.

Hazipaswi kubweteka na kuona zina kazi rahisi mbele yao kwani zinaweza kujikuta zikiwapa fursa wapinzani wao kuziadhibu na kuacha majonzi kwa nchi.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: