Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wenye ndoo yao AFCON hawa hapa

Bryan Teixera Cape Verde Egypt Africa Cup Of Nations Wenye ndoo yao AFCON hawa hapa

Wed, 31 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya waliokuwa mabingwa watetezi Senegal kutolewa kwa penalti 5-4 na wenyeji Ivory Coast, taji la Mataifa ya Afrika sasa halina mwenyewe na imepita miaka 14 bila ya taifa moja kutwaa Afcon mfululizo.

Matumaini ya Senegal kutwaa taji hilo kwa mara ya pili katika historia ya michuano hiyo iliyoasisiwa mwaka 1957, yalizimwa na mtoakea benchini Franck Kessie aliyefunga penalti ya 5 katika hatua ya kupigiana matuta wakati wenyeji wakifunga penalti zote huku beki wa Nottingham Forest ya Ligi Kuu ya England, Moussa Niakhate akikosa penalti pekee kati ya tano za Senegal.

Wachezaji wanne wa Ivory Coast waliofunga penalti zao waliingia kutokea benchini -- Nicolas Pepe, Christian Kouame, Sebastian Haller na Kessie -- wakati nahodha Serge Aurier pekee aliyeanza katika kikosi cha kwanza pia alifunga penalti yake kati ya tano za wenyeji.

Kessie, ambaye sasa anachezea Al Ahli ya Saudi Arabia baada ya kutamba katika klabu kubwa kadhaa za Ulaya kama Atalanta, AC Milan na Barcelona, ndiye aliyefunika katika mchezo huo akifunga penalti ya bao la kusawazisha la Ivory Coast zikiwa zimesalia dakika nne mechi kumalizika. Senegal ilitangulia mapema dakika ya nne kupata bao lililofungwa na straika wa klabu ya Al Shabab FC ya Saudi Arabia, Habibou Diallo kwa asisti ya kibabe sana kutoka kwa supastaa wao Sadio Mane.

Kutolewa kwa Senegal kunamaanisha kwamba miaka 15 itapita bila ya timu yoyote kutwaa taji la Afcon mara mbili mfululizo, tangu Misri ilipotwaa mara tatu mfululizo mwaka 2006, 2008 na 2010.

Kiujumla, wakati mwaka huu fainali hizo zinafanyika kwa mara ya 34, ni mara nne tu ilitokea kwa taifa moja kutwaa taji la Afcon mfululizo.

Misri ilibeba mara mbili mfululizo zilipoasisiwa fainali hizo mwaka 1957 na 1959, kisha Ghana ikabeba mara mbili mfululizo 1963 na 1965, halafu Cameroon ikabeba 2000 na 2002 na kabla ya Misri kuweka rekodi ya kuwa taifa pekee kupiga ‘hat-trick’ ya ubingwa wa Afcon mwaka 2006, 2008 na 2010.

Michuano hiyo ilipofanyika kwa mara ya kwanza mwaka 1957, ilishirikisha mataifa matatu tu – Misri, Ethiopia na Sudan, na Mafarao wakatwaa ubingwa huo kwa kuifunga Ethiopia 4-0 katika fainali.

Tangu hapo, mataifa 14 tofauti yametwaa taji la Afcon, huku Misri ikiongoza kwa kutwaa mara 7 ikifuatiwa na Cameroon iliyolibeba mara tano, Ghana (4) na Nigeria (3).

Gwiji wa Cameroon, Samuel Eto’o ndiye mfungaji bora wa muda wote wa Afcon akitupia mabao 18, akifuatiwa na Laurent Pokou wa Ivory Coast (mabao 14).

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: