Miamba miwili ya soka barani Afrika, Nigeria na wenyeji Ivory Coast imemalizana usiku wa kuamkia leo katika fainali ya michuano ya Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 iliyotarajiwa kuwa ya aina yake huko mjini Abidjan.
Mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Olympique Alassane Ouattara, imehitimisha makala ya 34 ya fainali za Afcon ambazo hadi sasa zimetoa mabingwa 14 tofauti.
Misri inaendelea kushikilia rekodi ya kuwa taifa lililobeba taji hilo mara nyingi zaidi (7) ikifuatiwa na Cameroon (5) na Ghana (4). Kabla ya fainali ya jana, Nigeria ilikuwa imelibeba mara 3 (1980, 1994, 2013) na Ivory Coast ilikuwa imebeba mara 2 (1992, 2015), hivyo baada ya mechi ya jana kuna mmoja kaongeza taji.
Baada ya juzi, Afrika Kusini kuizima DR Congo kwa penalti 6-5 baada ya dakika 120 kumalizika kwa ma-tokeo ya 0-0, Bafana Bafana imevaa medali ya shaba kwa kumaliza washindi wa tatu wa fainali hizi za Ivory Coast.
Historia ya michuano hiyo iliyoanzishwa mwaka 1957 inaonyesha bado mfungaji bora wa muda wote ni Samuel Eto’o wa Cameroon mwenye mabao 18, akifuatiwa na Laurent Pokou wa Ivory Coast mwenye mabao 14.
Fainali zijazo zitafanyika nchini Morocco 2025 na baada ya fainali hizo, Tanzania itaandaa fainali za 36 kwa kushirikiana na Kenya na Uganda.
Wakati fainali ya jana ilitarajiwa kujaa ushindani, lakini kuna wakali hao wenye uraia pacha ambao wangeweza kuwapo uwanjani kule Abidjan na kuifanya mechi hiyo iwe ya kutisha zaidi kama wan-gechagua kuyatumikia mataifa yao ya asili. Hawa hapa ni mastaa 14 ambao katika mazingira tofauti wangeweza kucheza fainali ya AFCON ya jana.
BUKAYO SAKA (NIGERIA) Staa wa Arsenal, Saka amekuwa akiifuatilia Afcon kwa ukaribu na aliipongeza Nigeria iliposhinda mechi yake ya nusu fainaIi dhidi ya Afrika Kusini katika ukurasa wa mtandao wa kijamii.
Ingawa Bukayo alizaliwa Ealing, London magharibi, wazazi wake Adenike na Yomi wote wanatokea Ni-geria.
Kabla ya kuchagua kuitumikia timu ya taifa ya England mwaka 2020, winga huyo alikiri ulikuwa ni uamuzi mgumu kuufanya, na baada ya kuchagua alifafanua: “Najivunia asili yangu ya Nigeria. Daima naangalia mechi za Nigeria kwa kadri niwezavyo, na nawatakia mafanikio na ninawasapoti kila waendako.
“Lakini nimeshuhudia namna ambayo England inakua kisoka, na nadhani huko mbele watafanya ma-kubwa. Naona ulikuwa ni uamuzi sahihi kwangu kuchagua England.”
JAMAL MUSIALA (NIGERIA) Ilikuwa ni England ambayo ilikikosa kipaji spesho cha Musiala, ambaye aliamua kuchagua kuitumikia timu ya taifa ya Ujerumani.
Kama ilivyotokea kwa England, kinda huyo wa Bayern Munich pia aliitosa Nigeria walipomfuata kum-shawishi awatumikie mwaka 2020. Baba yake ni Muingereza mwenye asili ya Mnigeria na mama yake ni Mjerumani.
Akifafanua uamuzi wake mwaka 2023 kupitia tovuti ya TeamNigeriaUK3, Musiala alisema: “Ningeweza kuitumikia Nigeria kwa sababu ilipita akilini mwangu, na nikaitafakari sana. Nilikuwa na mazungumzo mazuri na Nigeria na Ujerumani.
Hivyo kilichobaki ilikuwa ni juu yangu mimi kuamua na kuona ni wapi nitajisikia amani zaidi. Hivyo nikaamua kuichagua Ujerumani.”
DAVID ALABA (NIGERIA) Ishu ya Alaba ni kisa cha kuvutia na angeweza kuitumikia Nigeria. Nyota huyu wa Real Madrid alizaliwa na mwana wa mfalme wa Kinigeria mjini Vienna, Austria, na baadaye akataka kuitumikia timu ya taifa la baba yake, lakini Wanigeria hawakumfuata.
Sasa akiwa ni mchezaji wa kimataifa wa Austria, beki huyo anafunguka kwamba alitaka kujiunga na ti-mu ya watoto ya Nigeria 2007 lakini akajikuta njia yake imezuiwa. “Nilitaka kuitumikia Nigeria lakini niseme ukweli, hapakuwa na mtu aliyenifuata rasmi,” alibainisha mwaka 2013.
“Skauti mmoja aliwahi kuzungumza nami. Nikapata taarifa kwamba Nigeria itawapa nafasi wale waliopo nchini humo tu kwa sababu ya ugumu wa kusafiri, na ishu yote ikaishia hapo.”
SERGE GNABRY (IVORY COAST) Nyota mwingine wa Bayern Munich ambaye alizaliwa mjini Stuttgart ni Gnabry, ambaye baba yake mu-Ivory Coast na mama yake ni Mjerumani.
Ivory Coast ilijaribu kumpata winga huyo aje kuitumikia nchi hiyo mwaka 2014 wakati akiwa bado ni mchezaji wa Arsenal, lakini akafafanua miaka saba baadaye kwamba anajiona yuko karibu sana na nchi aliyozaliwa kuliko iliko asili yake.
“Chama cha soka cha Ivory Coast kiliwasiliana nami kuomba tukutane ili kiunishawishi nichezee timu ya wakubwa,” Gnabry aliiambia GOAL. “Lakini ilikuwa iko wazi kwangu: nilizaliwa na kukulia hapa Uje-rumani, nimechezea timu zote za vijana za Ujerumani, hivyo nikataka nichezee timu ya taifa ya wakubwa ya Ujerumani pia.
“Kule pia ni nyumbani kwangu. Baba yangu anatokea kule na ndugu zangu wengi bado wanaishi kule. Nimewahi kutembelea kule mara chache, na ikiwezekana, nataka kutembelea mara kwa mara.”
TAMMY ABRAHAM (NIGERIA) Straika wa AS Roma, Tammy Abraham amekuwa muwazi kuhusu kuishabikia Nigeria katika fainali hizo za Afcon, akijumuika na Saka katika kuisapoti ‘Super Eagles’ kwenye mitandao ya kijamii.
Moja ya vipaji vikubwa vya soka vilivyoibukia London kusini, baba wa straika huyo Mnigeria na rafiki wa rais wa zamani wa Shirikisho la Soka la Nigeria, Amaju Pinnick. Mwaka 2017, Pinnick alikurupuka na kuongea mapema kwamba straika huyo wa Chelsea kwa wakati huo alichagua kuitumikia Nigeria, jam-bo ambalo Tammy Abraham wakati huo alikuwa na umri wa miaka 19 tu alilazimika kulikanusha.
Alipoitwa kwa mara ya kwanza kwenye kikosi cha timu ya taifa ya England miaka michache baadaye, Abraham alisema: “Nilikuwa nimejiandaa kuitumikia England. Kwa kucheza kwenye Ligi Kuu England, itakuwa vyema zaidi kama nitachezea timu ya taifa ya England pia. Ni jambo la heshima ya kipekee (kwamba Nigeria imenihitaji), lakini kwangu dhamira kuu ni kucheza hapa.”
FIKAYO TOMORI (NIGERIA) Rafiki wa karibu wa Tammy Abraham na ambaye walihitimu pamoja Chelsea, Tomori familia yake pia inatokea Nigeria, ikipitia Canada.
Beki wa kati huyo wa AC Milan, alikiri kwamba ‘anajiona ni Mnigeria sana’, akisifu alipokulia. Hata hivyo, alichagua kuitumikia England, akicheza mechi yake ya kwanza mwaka 2020 – jambo ambalo alilitaja ka-ma uamuzi “mgumu zaidi aliolazimika kuufanya”.
MANUEL AKANJI (NIGERIA) Kama Alaba, beki wa Manchester City, Akanji amedai kwamba hakuwahi kupata mwaliko wa Nigeria licha ya kwamba angeweza kuitumikia timu ya taifa la baba yake.
Beki huyo alizaliwa Neftenbach, Uswisi, mama yake akiwa ni Mswisi na alikuwa akitajwa kwamba an-geweza kuitumikia Nigeria kama kuichagua nchi ya mama yake.
Akizungumza mwaka 2018, alisema: “Nigeria haikuwahi kuniita ili nikaitumikie. Hapakuwa na maswali kuhusu wapi nilipaswa kuchezea kwa sababu Uswisi iliniita niitumikie. Sikusikia chochote kutoka Nige-ria. Hivyo uamuzi wangu ukawa ni huo.”
CURTIS JONES (NIGERIA) Mchezaji mwingine ambaye bado anaweza kuitumikia Nigeria ni Jones, licha ya kwamba nafasi hiyo inazidi kupotea kutokana na moto anaouwasha akiwa na Liverpool msimu huu.
Jones, mama yake ni Mnigeria, lakini amechezea timu za taifa za vijana zote za England na huenda akaitwa kwenye timu ya wakubwa kwa ajili ya mechi zao za kirafiki dhidi ya Ubelgiji na Brazil zitakazo-chezwa mwezi Machi.
WESLEY FOFANA (IVORY COAST) Nyota wa Chelsea, Fofana angeweza kuitumikia Ivory Coast. Alizaliwa Marseille, Ufaransa. Lakini baba yake ni wa Ivory Coast. Akizungumzia kuichagua Ufaransa bada ya Ivory Coast ambayo ilipambana kumpata, alisema: “Ufaransa imenipa elimu.
Ndio chaguo la moyo wangu. Nilizungumza na kocha wa Ivory Coast, lakini mimi ni Mfaransa, nimezaliwa, nimepata elimu yangu hapa. Hivyo kwa uhakika, chaguo ni jepesi. Nimechagua Ufaransa kwa sababu ndio ipo ndani ya moyo wangu.”
EBERECHI EZE (NIGERIA) Mzaliwa mwingine wa London kusini ni Eze, ambaye wazazi wake ni Wanigeria. Mwaka 2019 alizima uvumi kwamba angechezea Nigeria alipoichagua England akisema: “Nimezungumza na watu walioni-zunguka, familia yangu, mke wangu, nikapata ushauri kwa watu wa karibu. “Tukaona hili ni chaguo sa-hihi.”
NONI MADUEKE (NIGERIA) Staa wa Chelsea, Madueke ni mmoja wa ambao bado anaweza kuichezea Nigeria kwani bado hajaitwa na timu ya wakubwa ya England japo aliichezea England U-21. Amesema: “Niko wazi kuchezea England au Nigeria. Ngoja tuone itakuwaje.”
DOMINIC SOLANKE (NIGERIA) Mchezaji mwingine ambaye bado anaweza kuichezea Nigeria ni Salonke mwenye miaka 26 sasa.
Straika huyo wa Bournemouth aliye katika kiwango cha juu aliichezea timu ya wakubwa ya England lakini ilikuwa katika mechi ya kirafiki dhidi ya Brazil mwaka 2017, ikimaanisha anaweza kuitumikia Nige-ria. Hata hivyo, akizungumza Aprili mwaka jana, alisema hajawahi kufuatwa awatumike.