Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waarabu watua kumng'oa Benchikha

Benchikha Mapinduzi.jpeg kocha Abdelhak Benchikha

Wed, 31 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Taarifa ambayo mabosi wa Simba na mashabiki wao watachekelea kuliko ni hii ya kocha Abdelhak Benchikha kuchomoa kwa mara ya pili ofa ya kuifundisha timu ya taifa lake, yaani Algeria.

Amekataa fungu la maana kwa kile kinachodaiwa kwamba analinda kesho yake dhidi ya mastaa jeuri na wasioambilika wa nchi hiyo. Mwanaspoti linajua kwasasa analipwa zaidi ya Sh80 milioni kwa mwezi ndani ya Simba nje ya posho ndogondogo zinazoambatana na matokeo ya michuano tofauti.

Shirikisho la Soka la Algeria linataka kurudisha nidhamu ya kikosi likiamini baadhi ya mastaa wake wanaocheza nje ni kama wamekuwa juu ya makocha likihitaji mtu atakayerudisha nidhamu.

Algeria inaona mtu muafaka ni Benchikha na baada ya kocha huyo kugoma kwa mara ya kwanza wakaamua kumpandishia mshahara ili akubaliane na ofa hiyo.

Awali Benchikha angekwenda kuchukua kiasi Cha Euro 208,000 sawa na Sh571 milioni kwa mwezi mshahara ambao ndio alikuwa analipwa kocha wa sasa aliyebwaga manyanga, Djamel Belmadi.

Benchikha ni kocha chaguo la rais wa shirikisho la nchi hiyo, Walid Sadi ambaye alikuwa tayari kumlipa mshahara wa Euro 211,275 (takriban Sh580 milioni) ambazo zingemfanya kuwa kocha anayelipwa zaidi Afrika.

“Tungependa kuwa na kocha anayeijua zaidi Algeria lakini kubwa ni kuja kuwarudishia ufanisi wachezaji wa timu ya Taifa. Sote tunafahamu kwamba Benchikha ni mmoja wa makocha bora sio tu Algeria, bali hata Afrika,” alisema Sadi ambaye yupo kwenye presha kubwa baada ya timu ya Taifa hilo kuishia hatua ya makundi kwenye fainali za Mataifa Afrika (Afcon) zinazoendelea nchini Ivory Coast.

Nyuma ya Belmadi ambaye amewahi kuchukua taji la Afrika msimu wa juzi, makocha wanaofuatia kwa kulipwa pesa nyingi ni Rui Victoria wa Misri anayepokea Euro 200,000 (Sh 549 milioni) na Jean Luis Gasset wa Ivory Coast aliyetimuliwa akichukua Euro 108,000 ( Sh 297 milioni).

Taarifa zinaelezaBenchikha anakubali fedha hizo, lakini hakutaka kukubaliana na presha kubwa iliyopo kwa sasa katika timu ya taifa hilo ambayo ingeweza kuporomosha heshima yake na kumpoteza ndani ya muda mfupi.

Benchikha ameona ni bora abaki na Simba ili kuweza kufanya kazi zake kwa utulivu kuliko kukimbilia ofa hiyo kubwa ambayo ingemfanya kuwa kocha anayelipwa zaidi Afrika na mmoja wa watu wake wa karibu ameliambia Mwanaspoti kwamba anadhani kwa kusalia Simba anaweza kufanya vizuri kimataifa na kupata dili ya maana zaidi kwani atacheza mechi nyingi ambazo zinaangaliwa na watu wengi zaidi. Simba ipo kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambako Benchikha amepania kufanya vizuri zaidi.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: