Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uliona tofauti ya Diarra na Onana?

Onana X Diarra Uliona tofauti ya Diarra na Onana?

Wed, 31 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kumbe hata Taifa Stars ingeweza kuchukua taji la Afcon! Kila nikitazama Fainali za Mataifa ya Afrika 2023, zinazoendelea Ivory Coast, nagundua kila timu inafungika na kila timu inaweza kuwa bingwa. Wakubwa wamepungua sana Afrika. Soka la Afrika kwa sasa ni kama halina mwenyewe.

Afrika hakuna tena wachezaji wakubwa. Tunaishi kama kambale kwa sasa. Baba na mtoto wote wamejaa ndevu!

Natazama viwango vya timu kubwa na timu ndogo, nashindwa kuona tofauti kubwa, viwango vya wachezaji wanaocheza Ulaya na Afrika, sioni tofauti kubwa.

Kuna muda hujui ni mchezaji gani anacheza PSG ya Ufaransa na nani anacheza Simba SC ya Tanzania. Anachofanya Djigui Diarra anayechea Tanzania pengine hakuna tofauti na Andre Onana wa Manchester United.

Kuna kitu hakipo sawa kwenye Soka la Afrika. Ukitazama Afcon unachoweza kuona ni familia ya kambale. Baba ndevu. Mtoto ndevu. Hakuna wakubwa tena.

Karibu timu zote zinaungaunga tu. Historia na uzoefu kidogo ndiyo vinaonekana kuleta wasiwasi.

Kwa ninachokiona kwenye fainali hizi, hata Stars ingeweza kutwaa ubingwa.

Zamani ilikuwa ni nadra sana kuona wachezaji wa ndani ya Afrika wanaitwa kwenye vikosi vya mataifa yao na hasa Afrika ya Magharibi.

Siku hizi wanaitwa na wanaanza kwenye vikosi vya kwanza. Zamani wachezaji wengi wanaocheza timu kubwa za Ulaya ndiyo walikuwa wafalme.

Siku hizi hakuna majina makubwa kutoka Arsenal, Manchester United, Bayern Munich, Manchester City yanayokuja kutamba Afcon. Hii michuano haina mwenyewe kwa sasa. Yotote ni bingwa. Hata Stars ingeweza kutwaa Ubingwa.

Kabla ya robo fainali, bingwa mtetezi Senegal tayari katupwa nje ya mashindano! Misri katupwa nje, Tunisia, Algeria, Cameroon. Sio kawaida.

Hata hao wakubwa wachache waliosalia, nao vyao ni vilevile vya Stars. Nilichogundua ni kama umejengeka vizuri Kisaikolojia, unafanya vizuri kwenye michuano hii.

Hakuna wakubwa tena Afrika. Yamebaki majina tu na historia. Ukisikia Misri katwaa taji la Afcon mara saba unaogopa lakini ukimwona uwanjani, hakuna maajabu yotote.

Algeria yule, sio Algeria wa leo. Waarabu wale wa Afrika, sio hawa wa leo. Siku hizi wanapigwa tu kama ngoma. Hakuna anayeonyesha utofauti wowote uwanjani. Sioni tena ukubwa wa timu za Magharibi kwenye Afcon hii.

Hakuna tena utemi. Cameroon, Senegal, Nigeria, Ghana walikuwa wababe kweli kweli enzi hizo lakini ukitazama viwango vyao msimu huu, hakuna ukubwa ule. Historia na uzoefu tu wa majina yao ndiyo mkubwa. Viwango uwanjani ni kawaida sana.

Morocco wamekuja kwenye michuano kama miongoni mwa timu zinazopigiwa chapuo na kutwaa ubingwa, lakini ukiangalia mechi zao zote, unabaki kushika kichwa!Afrika Maisha yetu ya soka kwenye Afcon hii ni kama kambale.

Baba, mama na mtoto, wote wana ndevu. Siku hizi hakuna tena wachezaji wakubwa kutoka Ulaya. Siku hizi hakuna tena wababe wa Kaskazini.

Siku za nyuma Kidogo, timu za Morocco, Tunisia, Algeria na Misri ilikuwa ni mpaka wakutane wao kwa wao. Siku hizi wanafungwa tu na yoyote.

Hawana Jipya. Wanarukaruka tu uwanjani. Hata klabu zao zimeanza kupungua ubora. Watu wanajipigia tu.

Kama Tanzania tutakuwa na kina Novatus Dismas 10 tu Afcon za 2027, tutaisumbua sana Afrika. Kama tutafanikiwa kuwapeleka nje watu kama Clement Mzize, Abdul Soup na wengine wa kizazi hiki, 2027 ni ya kwetu.

Kule Daraja la kwanza Ufaransa, Ubelgiji, kunafufaa sana kutuandalia vijana. Ghana, Senegal, Misri, Algeria sio wa kutolewa mapema kiasi hiki.

Hawana wachezaji bora zama hizi wanaotikisa Ulaya. Misri walau bado wana Mohamed Salah ambaye anamalizia.

Maana hata salah namwona yuko jua la utosi. Kwa sasa Afrika haina tena mfalme. Usishangae best losers mmoja akaenda kutwaa ubingwa. Afrika haieleweki. Hakuna mkubwa wala mdogo siku hizi. Kila aliyejiandaa kisaikolojia vizuri anaweza kuwa bingwa.

Ukiona hadi wachezaji wa kutoka ligi yetu ya Tanzania wanatamba Afcon, ujue wakubwa hawapo tena. Ukiona ligi ya Tanzania kwa sasa inapeleka wachezaji wengi Afcon, jua tunaenda pazuri.

Thamani ya ligi yetu inazidi kusonga mbele. Tukipata mchanganyiko mzuri wa vijana wa nje na ndani, 2027 ni yetu. Hakuna tofauti kubwa sana kati yetu na wao. Afrika haina wakubwa tena. Afrika haina mfalme tena wa soka. Viwango vinaonekana ni vile vile . Tofauti kubwa ipo kwenye historia na uzoefu kidogo.

Suala la kupeleka wachezaji wetu nje ya nchi, linapaswa kuwa la kinchi sasa. Sula la kusaka wachezaji wenye asili ya Tanzania wanaocheza soka, linapaswa kuwa ajenda yetu muhimu.

Ni muda wa kutumia vyema balozi zetu kusaidia. Ni muda wa wadau kukaa chini pamoja na kuwa na ajenda ya kitaifa.

Tukipata wachezaji 10 wa uhakika wenye asili ya Tanzania na kupeleka wengine 10 Ulaya, ndani ya miaka mitano kuna mahali pakubwa tutakuwa tumesonga mbele.

Mambo ya kuanzisha akademi hapa nchini na kuandaa miundombinu ni njia isiyotekelezeka. Nchi yetu michezo bado sio kipaumbele. Tumeimba sana huo wimbo na haijawahi kusaidia.

Njia rahisi ni kupeleka watoto wetu mapema kwenye nchi ambazo tayari zina miundombinu ya soka. Njia rahisi ni kupata wachezaji ambao tayari wameshaandaliwa.

Serikali,TFF na klabu zishirikiane tupeleke vijana wengi nje. Zishirikiane tupate vijana wengi wenye asili ya Tanzania kurudi nyumbani na hata kuwapa uraia wachezaji wazuri wasio na asili ya Tanzania.

Duniani kote inafanyika na hakuna tatizo lolote. Soka la Afrika halina wakubwa kwa sasa. Kila mtu anapambana na hali yake. Ni muda wa Tanzania na wadau wake kijipanga vizuri.

Kuwa mambo ya kuanzisha akademi hapa nyumbani ni mpango unaohitaji muda mrefu sana. Hata hizo akademi zenyewe baada ya kuzalisha vijana, watatakiwa pia kupelekwa Ulaya na sehemu nyingine kwenda kukua.

Mambo makubwa na ya uhakika ni mawili tu. Tupeleke wachezaji wengi nje na pili, mchakato wa kurudisha wachezaji wenye asili ya Tanzania nyumbani na kuwapa uraia wengine tunaowaona wana uwezo wa kusaidia Taifa Stars upewe kipaumbele.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: