Kikosi cha klabu ya USM Alger ya Algeria kimewasili salama Jijini Dar es Salaam Tanzania ambapo kimepata mapokezi maalum na Balozi wa Algeria nchini Tanzania, Mheshimiwa Ahmed Jalal.
Balozi Jalal amewahakikishia kuwapatia vifaa na mazingira salama kuelekea mchezo wa mkondo wa kwanza wa fainali ya kombe la Shirikisho Afrika utakaopigwa Jumapili dhidi ya Young Africans SC ya Tanzania katika dimba la Benjamin Mkapa.
Akizungumza mara baada ya kuwasili, Kocha Mkuu wa USM Alger Denis Lavagne amesema hawana shaka na hali ya hewa na wamefika kucheza na Yanga na wamefanya maandalizi ya kutosha kwa ajili ya Fainali dhidi ya Yanga SC.
Kwa upande wake, Nahodha wa USM Alger amesema wamefanya mazoezi yao vizuri na wamejiandaa na kucheza kwenye mazingira ya joto na hawakuingia kwenye Fainali kwa bahati na wamefika Tanzania kupambana kwenye mchezo wa kwanza katika Uwanja wa Mkapa Jumapili.
USM Alger watakuwa na kibarua kigumu mbele ya Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania, Yanga kwenye mchezo wa kwanza wa fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika utakaopigwa Jumapili katika dimba la Mkapa majira ya saa 10:00 jioni.