Mchezaji wa zamani wa Chelsea na New Castle United za Uingereza, Christian Atsu amepatikana akiwa hai na anaendelea kupatiwa matibabu hospitalini baada ya kuokolewa kutoka kwenye vifusi kufuatia matetemeko mawili mabaya ya ardhi yaliyokumba Uturuki na Syria.
Kulingana na ripoti nchini Ureno, staa huyo wa Hataysport ambaye ni raia wa Ghana bado aliokolewa kufuatia mkasa huo uliotokea mwendo wa saa 10 alfajiri ya jana, Jumatatu, Februari 6, 2023 wakati watu wakiwa wamelala.
A Bola inaripoti kuwa Mghana huyo alipatikana hai na kusafirishwa hospitalini baada ya kupata majeraha kwenye mguu wake wa kulia na kushindwa kupumua.
Winga huyo mwenye umri wa miaka 31, alikuwa amewafungia bao la ushindi waajiri wake wapya Hayatspor katika mechi yao ya Jumapili, Februari 6, muda mfupi tu kabla ya tetemeko la ardhi kutokea nchini humo.
Mwandishi wa habari Saddick Adams pia amethibitisha kwamba amekuwa akiwasiliana na uongozi wa Atsu na kwamba wamethibitisha kuwa winga huyo yuko salama.
Wachezaji wenzake wawili wa Hatayspor pamoja na watalaam wa ushauri pia walisemekana kuokolewa kutoka kwenye vifusi hivyo mapema Jumatatu.
Kufuatia tukio hilo video imeibuka kwenye mitandao ya kijamii ikimuonyesha sogora huyo wa zamani wa Newcastle alivyochanja bao hilo huku mashabiki wakisisimka kwa shangwe.
Tetemeko la ardhi Uturuki
Kufikia sasa zaidi ya watu 4,800 wamepoteza maisha nchini Uturuki na Syria baada ya matetemeko hayo na kusababisha uharibifu katika maeneo ya kusini mwa Uturuki na Kaskazini mwa Syria.
Tetemeko la kwanza lilikuwa na ukubwa wa Richter scale 7.8. Idadi ya waliofariki sasa inatarajiwa kuongezeka huku juhudi za kuwaokoa zikiendelea.