Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TETESI: Inonga atimkia FAR Rabbat kimyakimya

Inonga Bacca Varane Mlinzi wa Simba na Timu ya DR Congo, Henock Inonga

Fri, 16 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kwa Kiswahili cha kijiweni wanasema; “Imeisha.” Beki kitasa cha Simba aliyeng’ara na DR Congo kwenye Afcon, amefanya uamuzi wake kimyakimya na akapiga kimya vilevile. Na uamuzi huo unamaanisha kwamba atakuwa ndani ya jezi ya Simba katika mechi zisizozidi 15 tu za mzunguko wa pili wa ligi, baada ya hapo ndiyo hivyo tena.

Habari za uhakika kabisa kutoka kwenye vyanzo vya Mwanaspoti ni kwamba staa huyo ambaye mkataba wake na Simba unamalizika mwishoni mwa msimu, amesaini mkataba wa awali na FAR Rabat inayoongoza Ligi Morocco.

Kumbuka hii ndiyo timu anayoichezea Bernard Morrison ikifundishwa na kocha wa zamani wa Yanga, Nasreddine Nabi.

Inonga tayari amerejea nchini akitokea kwao DR Congo baada ya kuiwezesha nchi yake kuwa mshindi wa nne wa Fainali za Mataifa Afrika (Afcon) 2023 zilizofanyika nchini Ivory Coast na mwenyeji akichukua taji hilo.

Taarifa kutoka nchini Morocco ni kwamba Inonga ameingia makubaliano ya awali na klabu ya FAR Rabat ambayo yatamfanya mwisho wa msimu kwenda kusaini mkataba wa miaka mitatu na vinara hao wa Ligi Kuu ya nchini humo maarufu kama Botola Pro. Viongozi wa klabu hiyo walikuwa wakimuwinda siku nyingi ingawa za ndaani kabisa zinadai Nabi alikuwa akimtamani zaidi Ibrahim Bacca wa Yanga.

FAR Rabat imekuwa ikimuwinda Inonga kwa miaka mitatu sasa ambapo beki huyo akiwa Ivory Coast ilikuwa inataka kumalizana naye kabisa imchukue jumla lakini ugumu ukawa kwa Simba ambapo sasa msimu ukiisha ataondoka kama mchezaji huru.

Taarifa za Inonga kusaini FAR Rabat zinachochewa zaidi na Waarabu hao ambao baada ya kushindwa kumsainisha kwenye dirisha dogo haikusajili beki yoyote huku Nabi akiliambia Mwanaspoti kuwa timu yake itasaka beki mwisho wa msimu huu.

“Tumeshindwa kupata beki kwasasa, mabeki wazuri wengi walikuwa kwenye mikataba migumu na klabu zao, nimeambiwa na uongozi wataniletea beki mwisho wa msimu huu, kwahiyo kwasasa ingawa ilikuwa muhimu kupata beki wa maana hakuna namna tutakwenda na hawahawa nilionao,” alisema.

FAR Rabat kwenye usajili wa dirisha dogo ilimsajili mchezaji mmoja pekee kiungo Tumisang Orebonye, raia wa Botswana akitokea USM Alger ya Algeria.

Kwenye fainali hizo za Afcon Inonga alikuwa nguzo muhimu akicheza jumla mechi 5 kati ya 7 huku nne akicheza mwanzo mwisho.

Inonga kwenye kikosi cha Simba ni staa muhimu ambaye takwimu pia zinaonyesha kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu amecheza mechi 6 kati ya 15 akikosa mechi 9 ambapo kati ya hizo alizokosa nne ni kutokana kuwa majeruhi huku 5 akizikosa kutokana na kuwa kwenye Afcon.

Simba yenyewe tayari imeshaanza msako wa kutafuta beki mpya ikiona wasiwasi mkubwa wa kubaki na Inonga kwa msimu ujao, mchakato ambao unafanyika kwa siri kubwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: