Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Staa mpya Simba aonywa

Mutale Mnyama Joshua Mutale

Sun, 7 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Hapa wamelamba dume. Ndivyo anavyosema straika wa zamani wa Simba, Felix Sunzu akizungumzia usajili wa kiungo mshambuliaji mpya wa timu hiyo, Joshua Mutale kutoka Zambia, huku akimuonya asimezwe na presha ya mashabiki ambayo itampoteza na kuangusha matumaini ya timu hiyo.

Mutale ambaye ni miongoni mwa nyota wapya waliotambulishwa na Simba, akisajiliwa kutoka Power Dynamos ya Zambia kwa mkataba wa miaka mitatu, msimu uliopita alifunga mabao matano na asisti tatu kupitia mechi 26 alizocheza.

Wengine waliotambulishwa Simba ni Charles Ahoua, Lameck Lawi, Abdulrazak Hamza, Valentino Mashaka na Steven Mukwala sambamba na benchi jipya la ufundi chini ya Fadlu Davids kutoka Afrika Kusini aliyetua na wasaidizi wanne akiwamo Riedoh Beirden aliyewahi kuitumikia Yanga.

Wengine waliotua na Fadlu ni Wilken Darian, Mueez Kajee na Wyne Sandilands wote kutoka Sauzi, huku wachezaji waliotemwa ni Luis Miquissone, Clatous Chama, Saido Ntibazonkiza, Henock Inonga, John Bocco, Kennedy Juma na Idd Shaaban Chilunda, ilhali Kramo Aubin akitolewa kwa mkopo Al Hilal, Sadio Kanoute, Babacar Sarr, Pa Omar Jobe wakielezwa wapo njiani kuachwa.

Sunzu ambaye naye ni Mzambia aliyeweka makazi jijini Mwanza, alisema Mutale ana sifa kama za Emmanuel Okwi kwani ana kasi, uwezo wa kumiliki mpira na kuingia kwenye boksi la wapinzani, hivyo ataweza kupika mabao mengi msimu ujao kama atajiamini.

Alisema mashabiki wa Simba wana shauku na matarajio makubwa kwa mastaa wapya baada ya kupoteza nyota muhimu, hivyo anapaswa kujiamini na kuonyesha uwezo katika mechi tatu za kwanza ili wasimgeuke na kumtoa njiani.

“Unajua mpira wa Tanzania ni mgumu unatakiwa kuchukua gemu tatu kucheza vizuri, akifikiria na kusikiliza mashabiki atapotea, asipowasikiliza ataendelea na mpira wake. Yule dogo anajua mpira. Usipocheza vizuri mechi nne itakuwa ni shida inapoteza kujiamini,” alisema Sunzu aliyeshiriki ‘mauaji’ ya Yanga ilipopigwa mabao 5-0 katika mechi ya kufungia msimu ya Dabi ya Kariakoo iliyopigwa Mei 6, 2012.

“Ana kasi, uwezo wa kucheza namba saba na 11, anakimbia kwa kasi kuingia maeneo ya hatari ana sifa kama Emmanuel Okwi vile alikuwa anaweza kutoka pembeni na kuingia ndani. Ana kasi na uwezo wa kupiga chenga, ndivyo alivyo huyu dogo (Mutale).”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: