Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yasaka heshima, noti kwa Ahly

Ntibazonkiza Ahly .png Simba yasaka heshima, noti kwa Ahly

Tue, 24 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kitendo cha Simba kupata matokeo mazuri yatakayowavusha kuingia nusu fainali ya mashindano ya African Football League dhidi ya Al Ahly kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Cairo,Misri leo kuanzia saa 11 joni, sio tu yataifanya imalize unyonge dhidi ya Wamisri hao bali itawahakikishia kiasi cha Dola 1.7 milioni (Sh 4.2 bilioni).

Simba inayohitaji ushindi wa aina yoyote au sare ya mabao kuanzia 3-3 ili isonge mbele, haijawahi kuitoa Al Ahly wala kupata ushindi dhidi yao wakiwa Misri katika shindano lolote walilowahi kukutana na hii itakuwa mara ya kwanza iwapo wakifanya hivyo.

Katika ardhi ya Msiri, Simba imekutana na Al Ahly mara tatu ambapo imepoteza zote pasipo kufunga bao hata moja huku ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara nane.

Na ikiingia nusu fainali, maana yake Simba itakuwa na uhakika wa kupata Dola 1.7 milioni (Sh 4.2 bilioni) ambazo timu inayofika hapo ina uhakika wa kupata kutoka waandaaji wa mashindano hayo.

Simba inapaswa kuwa na nidhamu kubwa hasa ya kujilinda ili kuhakikisha Al Ahly hawana madhara makubwa kwao na wao waweze kupata matokeo mazuri yatakayowavusha.

Uimara wa hali ya juu unapaswa kuwepo katika safu ya kiungo ambayo imekuwa ikifanya makosa ya mara kwa mara ya kuruhusu wapinzani kumiliki mpira na kutengeneza nafasi, jambo linalopelekea safu ya ulinzi ishambuliwe mara kwa mara.

Mchezo wa leo utachezeshwa na refa Jean Jacques Ndala kutoka DR Congo ambaye atasaidiwa na Jerson dos Santos wa Angola na Arsenio Marengula wa Msumbiji huku refa wa akiba akiwa ni Messie Nkounkou wa Congo.

Refa Ndala amekuwa na historia nzuri na Simba ambapo katika mechi tatu alizoichezesha, imeibuka na ushindi mara mbili na kupoteza mchezo mmoja.

Kocha Roberto Oliveira wa Simba alisema kuwa ingawa wanafahamu watacheza mechi ngumu leo, upande wake hauna wasiwasi na jambo la muhimu ni wachezaji wake kutimiza yale waliyofanyia kazi mazoezini.

"Ahly ni timu kubwa. Tukirudia makosa kama ya mchezo uliopita yatatuweka kwenye wakati mgumu. Tutaendelea kukumbushana wakati wa mchezo.

Tunahitaji kufunga mabao lakini lazima tuwe na kasi. Huu ni mchezo wa soka na nafasi ya kuwatoa Al Ahly tunayo kama tutacheza vizuri na kufanya vitu vya msingi uwanjani," alisema Robertinho.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: