Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yaanza kutesti mitambo Misri

Simba Test Simba yaanza kutesti mitambo Misri

Sun, 21 Jul 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya kujifua kwa muda wa wiki mbili sasa katika kambi iliyopo Ismailia, Misri kikosi cha Simba chini ya kocha mpya, Fadlu Davids kesho jioni kitashuka uwanjani kutesti mitambo dhidi ya El Qanah ya nchini humo.

Mechi hiyo ya kwanza ya kimataifa ya kujipima ngumu itapigwa kuanzia saa 11:30 jioni kwenye uwanjani uliopo kwenye kambi hiyo, ikiwa sehemu ya maandalizi ya msimu mpya wa mashindano na nafasi ya kocha Fadlu kuwasoma vyema mastaa wa timu hiyo na kurekebisha makosa mapema kabla ya kurudi nchini.

Kocha huyo alinukuliwa na mtandao wa klabu ya Simba, akijivunia kikosi alichoancho kwa jinsi kilivyo na ushindani unaompa picha ya kufanya vizuri msimu ujao, ingawa itakuwa mara ya kwanza kwake kufanya kazi Ligi Kuu Bara.

Fadlu alisema ameuona uwezo wa mchezaji mmoja mmoja na alishaanza kuwapa mazoezi ya kimbinu, ufundi ili kupata timu itakayokuwa na uwezo wa kufanya vizuri wakati wa mashindano mbalimbali.

Kocha huyo aliyasema hayo, wakati anafanya mahojiano na mitandao ya kijamii ya Simba, alisema "Ushindani ni mkubwa, kila mchezaji anajituma, nimefanikiwa kuona uwezo wa mchezaji mmoja mmoja, hilo ni jambo muhimu, kwani nakuwa najua jinsi ya kuwatumia. Ninachokifanya kwa sasa ni mazoezi ya mbinu na ufundi, ili kupata timu itakayokuwa na uwezo mkubwa wa kupata matokeo katika mashindano mbalimbali."

Kocha huyo alisema ni kazi yake kuona kila mchezaji anafanya vizuri na kufurahia kuitumikia klabu hiyo kwa mafanikio makubwa.

"Ni kazi yangu kila mchezaji kushaini katika nafasi yake, ndio maana kila mmoja namuelekeza katika nafasi yake jinsi ya kutekeleza majukumu yake, pia nitaendelea kuwaona katika mechi mbalimbali ambazo tutacheza hapa zinaweza zikawa tatu," alisema kocha msaidizi huyo wa zamani wa Raja Casablanca ya Morocco.

MSIKIE ABEL

Katika hatua nyingine, kipa wa Simba, Hussein Abel amesema kwa usajili uliofanywa na mbinu wanazopewa kambini Misri, zinamfanya aamini msimu ujao itakuwa zamu ya Mnyama kuwapa tabasamu mashabiki baada ya kuukosa ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho kwa misimu mitatu mfululizo.

Abel alisema kinachompa kujiamini kujiona watakuja na nguvu mpya ni aina ya vipaji vikubwa, anavyoviona katika mazoezi ya kambi iliyowekwa nchini Misri.

"Simba imesajili vijana wenye vipaji vikubwa, ambavyo naamini vitawashangaza wengi pindi ligi itakapoanza, hivyo mashabiki wetu wakae mkao wa kufurahia kuiona burudani kutoka kwa wachezaji wao. Ushindani ni wa juu, kila mchezaji anapambana kumshawishi kocha ili kumpa nafasi kikosi cha kwanza, jambo linaloongeza uwezo mkubwa kwa mchezaji mmoja mmoja."

Simba ina makipa Ayoub Lakred, Ally Salim na Aishi Manula ambaye bado hajaruipioti kambini na Abel alisema hana presha wala kuogopa ushuindani, kwani kocha ndiye atakayeamua nani ampe nafasi.

Uwepo wa benchi la ufundi jipya la Simba, chini ya kocha mkuu Fadlu Davids, linampa nguvu Abel kuona milango ipo wazi kwa kila atakayeonyesha uwezo wake.

"Uzuri wa maandalizi ya msimu kila mchezaji anakuwa na nafasi ya kuonyesha ushawishi wake, kocha ni mgeni ana jicho lake la kuona nani atamtumia kulingana na mechi husika za mashindano mbalimbali ya msimu ujao," alisema kipa huyo wa zamani wa KMKM ya Zanzibar na Tanzania Prisons.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: