Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba watakata kwa Mkapa kilele cha "Simba Day", waitandika APR

Simba Ubaya Ubwela APR Simba watakata kwa Mkapa kilele cha "Simba Day", waitandika APR

Sat, 3 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Simba imekamilisha tamasha lake la Simba day la msimu wa 16 kibabe, ikifanya makubwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam huku ikishinda kwa mabao 2-0 dhidi ya APR ya Rwanda.

Mabao mawili ya Debora Mavambo na jingine la Edwin Balua yalitosha kuwapa mzuka wanasimba katika hitimisho la tamasha la 16 la Simba Day, huku Steven Mukwala akipoteza penalti katika dakika yab44 ya kipindi cha kwanza.

Debora alifunga dakika ya 47 alipiga shuti kali kabla ya Kelvin Kijili alipiga krosi iliyosindikizwa na Balua dakika ya 67 na kuhitimisha pati la Simba.

KWA MKAPA KWAFURIKA

Mapema tu Saa 11 jioni nyomi iliyokuwa nje ya uwanja ilifanikiwa kuingia na kuujaza uwanja wa Mkapa ambao unajaza watazamaji 60,000.

Uwanja huo hadi saa tisa jioni ulikuwa umeingiza watazamaji wengi ukiacha magepu machache ambayo ilipofika saa 11 jioni yalizibwa na kuufanya Kwa Mkapa kuwa na rangi nyeupe na nyekundu.

MAGETI YAVUNJWA

Baada ya kuona hawaingii kwa haraka, mashabiki walijikuta wakisukukamana na kuvunja moja ya geti uwanjani hapo, lakini Polisi waliwahi na kuituliza hali hiyo kisha baadaye mageti zaidi kufunguliwa kuruhusu mashabiki kuingia na mambo kukaa sawa

ALIKIBA ATEKA SHOO

Kwa upande wa burudani jukwaa la burudani lilikuwa na wasanii wanne bapo Twanga Pepeta ndio walianza kutoa burudani na baadae akapanda Chino Kidd ambaye alitoa burudani kwa mashabiki waliojitokeza uwanjani hapo.

Baada ya Chino Kidd jukwaa likatekwa na Joh Makini ambaye licha ya kuimba nyimbo zaidi ya mbili hakuweza kupokelewa kwa shangwe kama ilivyokuwa kwa wasanii waliomtangulia.

Funga kazi ilikuwa ni kwa Alikiba ambaye aliingia kwa staili ya kipekee na kuwaacha mashabiki wa Simba wakishindwa kuelewa baada ya kutanguliza warembo.

King Kiba ameingia na gari aina ya BMW iliyo wazi juu huku wanenguaji wake wakitangulia kwa kuingia wakiwa wamevaa sketi nyeupe na kujifunika miamvuli.

Wakati wanenguaji wanawake wakiingia hivyo kwa upande wa wanaume waliingia kwa viatu vya mataili na kuzunguka nusu uwanja.

Gari aliyoingia nayo Alikiba ilikuwa ikiiendeshwa na Mwijaku imechukua dakika zaidi ya tatu staa huyo akizunguka na gari yake bila kuimba huku dereva wake akivaa vazi lenye muonekano kama spaida.

Alikiba ameanza na burudani kwa kuimba wimbo wa Sumu aliomshirikisha Marioo wimbo huo umewanyanyua mashabiki ambao wangu wa wanaimba pamoja.

AHMED ALLY KIMASAI

Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally baada ya kutinga na Mnyama Ngamia kwenye tamasha lililopita, safari hii akatinga uwanjani kitofauti akivaa vazi la kimasai na kuongozana na wamasai waliomsindikiza alipokuwa anaingia Uwanja wa Mkapa.

Ahmed ambaye ndiye aliyeanzisha msemo wa Ubaya Ubwela aliingia uwanjani kwa kuwashtukiza mashabiki wakiduwaa kumtazama baada ya kujichanganya na wamasai aliongozana nao.

Baada ya kuongozana na wamasai hao walikaa jukwaani na kutumbuiza nyimbo za kabila hilo lililoibua shangwe la mashabiki wengi uwanjani hapo.

KAJULA AAGWA RASMI

Aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Simba, Imani Kajula ameagwa rasmi katika tamasha la Simba Day, huku wakibainisha ataendelea kuitumikia timu hiyo hadi mwisho wa mwezi huu.

Kajula ambaye ni mzoefu kwenye uongozi wa mpira kwani alikuwepo kwenye Kamati ya maandalizi ya Michuano ya Afrika ya vijana chini ya umri wa miaka 17 yaliyofanyika nchini mwaka 2019 alijiunga na Simba kuzipa pengo la Barbara Gonzalez aliyejiondoa Desemba 2022.

MUTALE NA JEZI YA ONANA

Kiungo mshambuliaji wa Simba, Joshua Mutale amepokelewa kwa shangwe na mashabiki wa Simba baada ya utambulisho huku akiibuka na jezi namba saba ambayo ilikuwa inavaliwa na Willy Onana.

Onana anatajwa kuuzwa na Simba Uarabuni kwa dola 100,000 na katika utambulisho wa mastaa wapya wa Simba msimu 2024/25 jina lake halipo hivyo ni wazi sio sehemu ya kikosi cha timu hiyo.

Mutale baada ya utambulisho alisalimiana na mashabiki wa timu hiyo ambao walimpokea kwa shangwe na baadae kujiunga na wenzake hivyo kuvaa jezi yenye namba hiyo ni wazi ataitumikia msimu ujao.

Kiungo huyo, amepata jezi namba ambayo alikuwa anaitumia kabla ajajiunga na Simba akiwa Power Dynamos ya Zambia.

Onana ameitumikia Simba kwa msimu mmoja alijiunga na timu hiyo msimu 2023/24 akitokea APR ya Rwanda hatakuwa sehemu ya kikosi cha timu hiyo.

Utambulisho ulianza kwa benchi la ufundi chini ya kocha Fadlu Davids, akiwa na wasaidizi wake 11 ambapo baada ya hapo wakaanza wachezaji.

Utambulisho wa wachezaji ulianza na makipa wanne Ally Salim, Ayoub Lakred, Hussein Abel, Mussa Camara, huku kipa Aishi Manula akikosekana kwenye utambulisho huo

kabla ya kafuata mabeki tisa wakianza na Hussein kazi, Kelvin Kijili, Che Malone Fondoh, Shomari Kapombe, Abdulrazack Hamza, Valentin Nouma, nahodha Mohammed Hussein 'Tshabalala', David Kameta 'Duchu' na Chamou Karaboue.

Utambulisho huo ukaendelea kwa viungo 12 ukianza na Mzamiru Yassin, Awesu Awesu,Saleh Karabaka, Deborah Fernandez, Edwin Balua, Augustine Okejepha, Ladack Chasambi, Joshua Mutale 'SGR', Fabrice Ngoma, Omary Omary, Yusuf Kagoma, Jean Ahoua.

Wakamalizia washambuliaji wanne wakianza na Freddy Michael, Valentino Mashaka, Steven Mukwala huku akimalizia Kibu Denis ambaye alilazimika kuombewa msamaha kufuatia tukio lake la kutoroka kwenda kufanya majaribio nchini Norway na kisha kurejea klabuni hapo.

MANULA ASAHAULIKA

Aliyekuwa kipa namba moja wa Simba, Ashi Manula ametemwa kwenye kikosi cha timu hiyo msimu 2024/25 baada ya timu hiyo kutambulisha makipa wanne huku jina lake likiondolewa.

LAWI, MWENDA HAWAMO

Licha ya Simba kutangaza kuwasajili mabeki Lameck Lawi na Israel Mwenda lakini hawakutambulishwa kwenye utambulisho huo wa Jana kwenye kikosi cha msimu ujao.

RAIS SAMIA AWAPIGIA SIMU

Wakati Simba ikiendelea na tamasha lake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan alipiga simu uwanjani hapo kupitia kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo Greyson Msigwa.

Katika salamu zake Rais Samia akiwapongeza Simba kwa kuujaza Uwanja huo, huku pia akiwapongeza kwa kufanya usajili wa nguvu na kuwatakia kila la kheri.

FATAKI ZAPIGWA

Wakati timu hizo zikiingia uwanjani Simba ikawalipa watani wao Yanga kwa kupiga Fataki za kutosha na kunogesha tamasha hilo ambapo hiyo ni mara ya pili kwa wekundu hao kutumia mbwembwe hizo.

Kocha Fadlu, alianza na kikosi cha Salim, Kapombe Tshabalala, Karaboue,Che Malone, Ngoma, Mzamiru, Aweso, Mutale, Ahoua, Mukwala.

Dakika 45 za kwanza za kikosi hicho kilionyesha uwezo wa kukaba kwa nguvu na kucheza soka la haraka kwenda lango la wapinzani APR.

AWESO, MUTALE FRESHI

Ndani ya kipindi hicho cha kwanza staa wa kwanza aliyeonyesha uwezo mkubwa alikuwa Awesu aliyekuwa akisambaza vyema mpira huku Mutale akiwa mkali wa mbio.

Mutale dakika ya 42 aliisabibishia penalti Simba baada ya kutoka mbio na beki wa APR kumuangusha kwenye eneo la hatari na mwamuzi Ramadhan Kayoko kuamua iwe penalti.

Hata hivyo, penalti hiyo iliyopigwa na Mukwala ikagonga mwamba na kurudi uwanjani kisha APR kuokoa Simba ikipoteza nafasi kubwa.

ALLY SALIM DAKIKA 32

Mabadiliko ya mapema ya Simba yalifanyika dakika ya 32 alipotolewa Salim aliyeonyesha kutotulia langoni akiwa na makosa machache kisha baadaye kuonekana kupata maumivu, akatolewa na nafasi yake ikachukuliwa na Camara.

Mpaka dakika 45 za kwanza zinamalizika hakuna timu iliyofanikiwa kupata bao na Simba kurudi kipindi cha pili ikiwa na mabadiliko matatu akiwatoa Aweso, Kapombe , Ngoma na Mzamiru.

Nafasi hizo zilichukuliwa na Kijili, Okejepha, Fernandez na Balua huku wekundu hao wakabadilisha pia jezi na kurejea na jezi nyeupe badala ya zile nyekundu walizoanza nazo mchezo.

Mabadiliko hayo yakaipa bao la mapema Simba bao la kuongoza mfungaji akiwa Fernandez kwa shuti Kali la nje ya eneo la hatari.

Bado wekundu hao waliendelea kuonyesha falsafa ya kocha wao anataka timu yake ianzie kukabia juu kwa haraka na ukipata mpira ipige pasi za haraka kwenda lango la wapinzani kabla ya Balua kumalizia kazi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: