Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, Yanga nusu fainali hii hapa

Simba X Yanga CAF Simba, Yanga ramani hii hapa kutoboa nusu Fainali

Thu, 14 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Hizi ndizo mechi za kibabe na Simba, Yanga wote wamesisitiza wako tayari kukiwasha Kwa Mkapa maarufu kama Lupaso. Mechi za kuonyesha ukubwa wa Simba na Yanga katika anga la kimataifa. Mechi za kuleta heshima Afrika.

Ndio, juzi jioni jijini Cairo, Misri ilifanyika droo ya mechi za robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na vigogo hivyo kupangwa na mabingwa wa Afrika.

Yanga imepangwa kukutana na mabingwa wa michuano mipya ya soka Afrika, African Football League (AFL), Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, ilihali watani wao wa jadi, Simba wakipewa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Ahly ya Misri.

Droo nyingine zilihusisha TP Mazembe ya DR Congo itakayokutana na Petro Atletico ya Angola wakati Esperance ya Tunisia itaumana na Asec Mimosas ya Ivory Coast.

Tangu kufanyika kwa droo hiyo, kumekuwa na mijadala na maoni tofauti kutoka kwa wadau wa klabu hizo mbili juu ya nafasi ya timu hizo kwenda nusu fainali.

Wapo wanaoamini Simba ina njia nyepesi kulingana na Yanga inayokutana na Mamelodi ambayo kwa misimu ya hivi karibuni imekuwa tishio zaidi katika soka la Afrika.

Hata hivyo, bado Simba na Yanga hazitakiwi kubweteka au kujikatia tamaa kutokana na kupangwa na vigogo hivyo vya soka la Afrika.

Soka ni mchezo wa maajabu na pia una matokeo ya kushangaza, ukibebwa zaidi na sayansi inayohusisha maandalizi mzuri, mbinu za kupambana ndani ya dakika 90 za kila pambano na bila ya kuisahau bahati. Ndio, bahati katika soka huzaa matokeo yasiyotarajiwa.

Pia soka la kisasa limeifuta ile dhana kwamba ni lazima timu wenyeji ipate matokeo mazuri nyumbani na kupoteza zile za ugenini na badala yake mambo yapo kinyume.

Maandalizi mazuri na mbinu bora zitazibeba timu bila kujali kama zinacheza ugenini au nyumbani, kitu ambacho Simba na Yanga lazima ziishi katika dhana hiyo ili kupenya mbele ya Mamelodi na Al Ahly na hapa chini Mwanaspoti linakuletea dondoo ambazo timu hizo zikiamua kukomaa nazo basi zina nafasi kubwa ya kuishangaza Afrika na kufuzu nusu fainali.

SIMBA KWA MKAPA

Rekodi zinaonyesha kuwa Simba imekuwa na matokeo mazuri kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa mechi za CAF tangu iliporejea kwenye michuano ya kimataifa msimu wa mwaka 2018-2019.

Simba imepoteza mechi moja tu ikiwa nyumbani tangu iliporejea mechi za CAF kwa hatua za awali, lakini haijawahi kupoteza katika hatua ya makundi wala mtoano ikiwa nyumbani, kitu kinachoibeba mbele ya Al Ahly.

Achana na mechi za timu nyingine, lakini rekodi baina ya Simba na Al Ahly katika michuano ya kimataifa tangu wakati huo inaonyesha zimeshakutana mara sita, huku mara mbili kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Simba imeshinda mechi zote za nyumbani na kupoteza ugenini.

Lakini hata katika michuano mipya ya AFL, zimekutana mara mbili na mechi zote baina yao ziliisha kwa sare, tena ni Al Ahly waliolazimisha sare baada ya kukomboa walipotanguliwa kwa bao Kwa Mkapa na hata kule Misri. Kwa Mkapa Oktoba 20, 2023: Al Ahly ilitangulia kupata bao kupitia kwa Reda Slim katika dakika ya 45+1, lakini Simba ikakomboa kupitia kwa Kibu Denis dakika ya 53 na Sadio Kanoute akaweka chuma cha pili katika dakika ya 59. Kuanzia hapo Al Ahly ilionekana kama inaenda kufa 2-1, lakini ikapambana kujiokoa na ikasawazisha kupitia kwa Kahraba katika dakika ya 69 na hivyo kulazimisha sare ya 2-2.

Hali ilikuwa hivyo hivyo kule Misri, Kanoute tena aliifungia Simba bao la kuongoza katika dakika ya 68 kabla ya Kahraba tena kuikoa Ahly isilale nyumbani zikiwa zimesalia dakika 14 mechi kumalizika. Ikaisha 1-1. Al Ahly ikatinga nusu fainali ya AFL kwa faida ya mabao ya ugenini.

Simba ilipoteza ugenini kwa mabao 5-0 mbele ya Al Ahly mechi iliyopigwa Februari 2, 2019 kisha ikalala 1-0 Aprili 9, 2021, lakini ilishinda 1-0 kwenye mechi ya Februari 12, 2019 kisha ikaipasua tena Ahly 1-0 Februari 23, 2021, michezo yote ya makundi ya Ligi ya Mabingwa.

Kutokana na hali hiyo ya kuwa na matokeo mazuri nyumbani, Simba ya Abdelhak Benchikha inatakiwa kuhakikisha inapata matokeo mazuri nyumbani yatakayoirahisishia katika pambano la marudiano ugenini ili kuvuka kwenda nusu fainali.

Kama ilivyofanya katika mechi za nyumbani dhidi ya Asec Mimosas, Jwaneng Galaxy na Wydad CA katika hatua ya makundi, ndivyo Simba inatakiwa kufanya mbele ya Al Ahly ambayo haina matokeo mazuri ugenini katika mechi zao za hivi karibuni, zikiwamo za makundi, ikilazimishwa sare ya 1-1 na Yanga Kwa Mkapa, ikitoka suluhu na CR Belouizdad ya Algeria na kushinda mchezo mmoja pekee dhidi ya Medeama ya Ghana.

Katika mechi za AFL, Al Ahly haikushinda mechi yoyote ya ugenini, kwani ililazimishwa sare ya 2-2 na Simba kisha kufungwa bao 1-0 na Mamelodi katika hatua ya nusu fainali na kutolewa.

KAZI MOJA TU

Simba ili iwe na kazi rahisi mbele ya Al Ahly ni kutumia vyema mechi ya nyumbani kwa kupata matokeo mazuri ya ushindi mnono, ili iwe na kibarua chepesi ugenini, kwani Al Ahly ina rekodi tamu katika michuano ikifika hatua hiyo ya robo fainali, rekodi ikionyesha ni msimu mmoja tu kati ya mitano iliyopita ndio iling’olewa robo fanali.

Al Ahly ilitolewa msimu wa 2018-2019 kwa kufungwa na Mamelodi kwa jumla ya mabao 5-1, lakini misimu mingine iliyofuata imefika fainali na mara tatu imetwaa ubingwa na mara moja ilipoteza, hii ni kuonyesha Simba inapaswa kutobweteka na kudhani inakutana na timu nyepesi. Wapo wanaosema ukitaka kuizidi Al Ahly ni kuing’oa katika hatua ya makundi tu na sio kuiruhusu iingie hatua ya mtoano, kwani huko juu huwa haina kuremba.

Kitu kizuri ni kwamba kocha Benchikha anaijua vilivyo Al Ahly na ameitoa nishai mwanzoni mwa msimu huu kwa kuifumua mabao 2-1 katika mechi ya CAF Super Cup dhidi ya USM Alger ya Algeria aliyokuwa akiinoa kabla ya kuja Msimbazi.

Aina ya wachezaji waliopo Simba kuanzia kwa kipa Ayoub Lakred, Clatous Chama, Saido Ntibazonkiza, Fondoh Che Malone, Henock Inonga, Sadio Kanoute wakiongezewa nguvu na Babacar Sarr, Freddy Michael na Pa Omar Jobe na wengine mwenye uzoefu wa mechi za CAF kuna uwezekanao mkubwa wa Mnyama kutoboa wakiamua.

Katika misimu mitano kati ya sita mfululizo, Simba imekuwa ikiishia robo fainali zikiwamo nne za Ligi ya Mabingwa Afrika na moja ya Kombe la Shirikisho, kitu ambacho safari hii Benchikha na jeshi lake lazima wakomae ili kuvuka hapo kuifikia rekodi ya mwaka 1974 ilipocheza nusu fainali wakati michuano hiyo ikifahamika kama Klabu Bingwa Afrika.

Katika nusu fainali hiyo, Simba ilikwamishwa kwenda fainali na Wamsiri wa Ghazl El Mahalla (Mahalla Al Kubra) kwa mikwaju ya penalti 3-0 baada ya matokeo ya jumla kuwa sare ya 1-1, kila timu ikishinda nyumbani bao 1-0.

YANGA NJIA HII

Yanga inakutana kwa mara ya pili na Mamelodi baada ya mwaka 2001 zilipovaana katika mechi ya raundi ya pili na Wasauzi kushinda jumla ya mabao 6-5. Yanga ilifungwa 3-2 ugenini na kutoka sare ya 3-3 nyumbani enzi hizo ikiwa na kocha Charles Boniface Mkwasa.

Kwa hesabu za haraka ni kwamba Yanga ina mlima mrefu wa kuupanda kulinganisha na Simba kutokana na rekodi tamu za Mamelodi kwa miaka ya hivi karibuni.

Hata hivyo, kwa aina ya kikosi ilichonacho Yanga kwa sasa chini ya kocha Miguel Gamondi na kama itacheza soka kama ililocheza dhidi ya CR Belouizdad nyumbani, kuna nafasi kubwa kwa vijana wa Jangwani kuishangaza Afrika.

Katika mechi dhidi ya miamba hao wa Algeria, Yanga iliupiga mpira mwingi mno kwa kumiliki mchezo kwa asilimia kubwa ikitengeneza nafasi nyingi, japo ugenini ilipoteza 3-0 na kushinda nyumbani mabao 4-0 yaliyoivusha robo fainali.

Licha ya Mamelodi kuonekana tishio, lakini inafungika kwani katika mechi sita za makundi ilipoteza mechi moja ugenini dhidi ya TP Mazembe, na ilifunga jumla ya mabaao saba ikiwa na wastani wa kufunga bao moja tu kwa kila mechi, lakini tishio jingine kwa wababe hao ni kwamba hawaruhusu mabao. Walifungwa bao moja tu katika mechi sita za hatua ya makundi, kitu ambacho Yanga ni lazima ijipange kwelikweli kuikabili timu hiyo.

Yanga ni kati ya timu zilizomaliza na mabao mengi kwenye makundi ikifunga tisa sawa na Simba, lakini ni timu iliyoruhusu mabao sita yakiwa ni mengi miongoni mwa timu Nane Bora zilizotinga robo fainali kwa msimu huu.

IJIPANGE

Kwa kuwa timu iliyoruhusu mabao mengi zaidi katika hatua ya makundi kulinganisha na timu nyingine zote zilizotinga robo fainali, Yanga inapaswa kusuka upya ukuta wa timu yake kabla ya kukabiliana na Mamalodi yenye washambuliaji tishio kama Peter Shalulile, Lucas Costa, Thembinkosi ‘Nyos’ Lorch na wengine ambao wanajua kufunga.

Ibrahim Bacca, Dickson Job, Bakar Mwamnyeto na mabeki wa pembeni, Joyce Lomalisa, Nickson Kibabage, Yao Kouassi na kipa Diarra Djigui ni lazima wahakikishe wanacheza kwa nidhamu na kuwaheshimu Mamelodi kama walivyofanya mbele ya Belouizdad au Al Alhy kwa mechi za nyumbani ili kupata matokeo mazuri mbele ya Wasauzi.

Kocha Gamondi aliyewahi kuinoa timu hiyo ya Afrika Kusini, ni wazi kwa sasa atakuwa anaisoma upya Mamelodi kuona anatumia mbinu zipi za kuidhibiti nyumbani na ugenini.

Kitu cha muhimu ni kulitengeneza jeshi lake kuhakikisha kila nafasi wanazotengeneza uwanjani wanazitumia ili kupata ushindi mnono na kwenda kukomaa ugenini, ambako kwa msimu huu imekuwa haina rekodi nzuri kulinganisha na msimu uliopita iliposhiriki Kombe la Shirikisho Afrika na kufika hadi fainali.

Msimu huu Yanga imeshinda mechi mbili za ugenini hatua ya awali, lakini kwenye makundi imeambulia sare moja tu mbele ya Medeama ya Ghana, lakini ikapoteza mara mbili kwa Belouizdad na Al Ahly bila kufunga bao lolote, hivyo kama Gamondi hatajipanga vyema mbele ya Mamelodi huenda ikapata wakati mgumu.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: