Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba Day 2024... Ni shoo ya King Kiba

King Kibaaaaaaaaaaaaaaaaa Simba Day 2024... Ni shoo ya King Kiba

Sat, 3 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kwa mara nyingine ile shoo iliyokuwa ikisubiriwa ya Simba Day inafanyika leo kuanzia saa 4 asubuhi, lakini mashabiki wa klabu hiyo watapata burudani mapema kutoka mkali wa Bongofleva, Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’ kwani ndiye kinara wa utoaji burudani katika tamasha hilo Kwa Mkapa.

Kiba alitangazwa mapema Morogoro kama mtumbuizaji mkuu wa tamasha hilo la 16 akishirikiana na Joh Makini na Chino Kidd pamoja na wengine ili kuwapa burudani mashabiki.

“Mpo tayari?” alihoji ofisa habari wa Wekundu wa Msimbazi, Ahmed Ally kabla ya kumtangaza King Kiba mjini Morogoro, huku akisema leo atatoa burudani ya ngoma zake kali ukiwemo wimbo maalumu ‘Mnyama’.

Tofauti na ilivyokuwa katika tamasha lililopita ambapo Alikiba pia alikuwa mtumbuizaji mkuu, safari hii inaelezwa kwamba ‘hit maker’ huyo wa ngoma ya Fallen Angel aliyomshirikisha Bill Nas, atapewa muda wa kutosha ili kukata kiu ya mashabiki ambao watajitokeza kutazama utambulisho wa kikosi cha Simba.

Kwa upande wa maandalizi kwa ajili ya shoo hiyo, Alikiba alisema kila kitu kipo sawa na yupo tayari kwa kazi. “Mashabiki wa Simba wanatakiwa kuja kwa wingi maana hawana sababu ya kukosa, mimi na timu yangu tupo tayari kwa ajili ya kuwapa burudani,” alisema msanii huyo ambaye 2008 alishirikiana na R Kelly na wanamuziki wengine wa Kiafrika kwenye mradi ambao ulifahamika kama One 8.

ILIYOPITA ILIBAMBA

Kama unakumbuka miongoni mwa shoo kali ambazo zimefanywa na Alikiba kwenye Uwanja wa Mkapa ni pamoja na Simba Day iliyopita. Kwanini? alikuwa na ngoma mbili kali ambazo zilikuwa zikifanya vizuri wakati huo hivyo alienda vizuri na upepo.

Ngoma ya kwanza ilikuwa Sumu ambayo alimshirikisha Marioo huku kile kibao chake cha Mnyama ndicho kilikuwa moto jambo lingine ambalo liliamsha hasama na kufanya shauku iwe kubwa ya mashabiki kuhusiana na shoo hiyo na hicho ndicho kipindi alihama upande wa pili. Ikumbukwe kuwa Kiba alikuwa shabiki wa Yanga, hivyo ni kama alipishana na mshindani wake kwenye Bongofleva, Diamond Platnumz. Kuanzia namna alivyoingia uwanjani uwanjani kwa mbwebwe za kifalme huku akiongozwa na ‘jenerali’ wake, Mwijaku ilipendeza akisindikizwa na madansa ambao waliunda majukwaa tofauti kama ilivyo katika matamasha mengine makubwa. Mashabiki wa Simba walifurahi.

NEXT LEVEL

Ndani ya msimu uliopita King Kiba alihusika katika matukio mawili makubwa yaliyoihusisha Simba, ukianza na tamasha hadi ufunguzi ya michuano mipya ya African Football League, ilikuwa ni hatua nyingine kwa msanii huyo kutoa burudani tofauti zaidi, Afrika yote ilikuwa Tanzania.

Nini alifanya? Alikuwa na dakika chache kama mtumbuizaji mkuu katika ufunguzi huo kabla ya mchezo kati ya Simba dhidi ya Al Ahly kuchezwa, lakini alizitendea haki, hakutumbuiza Mnyama ila Sumu ilipigwa na ilikuwa shoo ya kibabe ambayo ilifanywa ‘Live’ kwenye uwanja wa Benjamini Mkapa.

Kiba mwenye alikiri katika makala yake baada ya ufunguzi ule kwamba ilikuwa ni shoo ya tofauti sana kuanzia katika maandalizi hadi katika namna ambavyo alipaswa kutumbuiza.Kiba alifanya zaidi ya kile alichotoa kwenye tamasha la Simba Day wiki chache nyuma na kuacha gumzo.

SASA ITAKUWAJE

Katika shoo mbili tofauti za King Kiba zikiihusisha Simba zilikuwa na viwango. Je! safari hii kutakuwa na upekee gani? huku ikielezwa atapata muda zaidi wa kukata kiu ya mashabiki wa timu hiyo wakati wakisubiri kuona chama lao likitesti mitambo dhidi ya APR ya Rwanda. Hiki ni kitendawili ambacho Kiba na watu wake watakuwa na jukumu la kukitegua katika tamasha hilo, akifanya zaidi itakuwa ni heshima kwake na kama kiwango kikipungua basi atakuwa amewapunja mashabiki zake na wapenda burudani.

TUNDA MAN NDANI

Pamoja na kwamba kutakuwa na orodha ndefu ya wasanii ambao watatumbuiza katika tamasha la Simba, msanii ambaye amekuwa akihusika karibu kila mwaka, Tunda Man anatarajiwa kuwa sehemu ya historia.

Tunda Man ni kati ya wasanii wabunifu ambao wamekuwa wakijipambanua pale ambapo wanapata nafasi ya kufanya shoo katika majukwaa mbalimbali, mwaka jana aliingia na kufanya igizo la kunyongwa kabla ya kutumbuiza ngoma yake ya kwamba hata mfanye nini Simba hawezi kuhama.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: