Mambo ni moto. Real Madrid imeripotiwa kuanza mpango wa kwenda kunasa saini ya mshambuliaji wa Manchester City, Erling Braut Haaland wakati dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi litakapofunguliwa.
Los Blancos ilihusishwa na straika huyo wa kimataifa wa Norway tangu alipokuwa akikipiga Borussia Dortmund, lakini Man City ndio waliofanikiwa kunasa saini yake na kumsainisha mkataba wa miaka mitano.
Haaland ameendelea kuonyesha ubora mkubwa ndani ya uwanja tangu alipochuka Man City, ambapo amefunga mara 33 katika mechi 34 za michuano yote aliyotumikia miamba hiyo ya Etihad. Straika, Haaland, 22, tayari ameshafunga mabao 27 kwenye Ligi Kuu England msimu huu na amefunga mfululizo katika mechi tano alizocheza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.
Licha ya Haaland kuwa kwenye kiwango bora kabisa, lakini inaelezwa Man City si mahali sahihi zaidi kwa mshambuliaji huyo kuonyesha ubabe wake ndani ya uwanja.
Kwa mujibu wa The Independent, Real Madrid inaaminika kwamba kuna nafasi kubwa wakanasa saini ya Haaland kwenye dirisha lijalo kutokana na mabingwa hao wa Ulaya kuonekana ndiyo hasa mahali ambako mchezaji huyo anataka akacheze.
Real Madrid wanamtazama Haaland kuwa mtu sahihi wa kwenda kuchukua mikoba ya Karim Benzema, ambaye bado hajasaini mkataba mpya wa kubaki Bernabeu, huku msimu ujao atakuwa amefikisha umri wa miaka 36.
Haaland alifunga mabao 86 na kuchangia mabao 23 katika mechi 89 alizocheza Dortmund kabla ya kuhamia Etihad.
Sambamba na Benzema wachezaji wengine wa Real Madrid ambao dili zao za mikataba zitaisha mwishoni mwa msimu huu ni Marco Asensio, Toni Kroos, Luka Modric, Dani Ceballos, Nacho na Mariano Diaz.
Kwenye La Liga, Real Madrid ipo nafasi ya pili ikiwa imezidiwa pointi tisa na vinara Barcelona na wamecheza mechi 24.