Matatizo yote ya Taifa Stars katika mechi ya ufunguzi wa Kundi F la Afcon ilipolala 3-0 dhidi ya Morocco juzi yalisababishwa na kijana mwenye miguu ya dhahabu Azzedine Ounahi.
Kiungo huyo wa ushambuliaji wa klabu ya Olympique Marseille ya Ligi Kuu ya Ufaransa mwenye umri wa miaka 23 na urefu wa futi 6, aliivuruga safu ya ulinzi ya Stars akifunga bao moja, kuhusika na jingine na kumsababishia kadi nyekundu beki Novatus Dismas Miroshi.
Licha ya mwili mwembamba, Onuahi aliendelea kuonyesha kipaji kikubwa alichonacho akiwanyima utulivu wachezaji wa Taifa Stas juzi na haikushangaza aliposhinda tuzo ya nyota wa mchezo baada ya mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Laurent Pokou uliopo San Pedro, Ivory Coast.
Bao alilofunga juzi dhidi ya Stars, ndio bao lake la kwanza kwenye michuano ya Mataifa ya Afrika, ambayo kwa mara ya kwanza aliitwa katika fainali zilizopita za 2021 na hizi ni fainali zake za pili.
Onuahi alifanya makubwa katika fainali zilizopita za Kombe la Dunia 2022 kule Qatar ambako Morocco iliandika historia mpya kwa kuwa timu ya kwanza ya Afrika kufika nusu fainali, ambako ilifika kibabe ikiwamo kuyafunga mataifa makubwa ya soka kama Hispania na Ureno. Walikuja kutolewa na Ufaransa katika nusu fainali, kabla ya kufungwa na Croatia katika kuwania mshindi wa tatu.
Baada ya kuonyesha kiwango cha kutisha katika mechi ya hatua ya 16-Bora ambayo Morocco iliing'oa Hispania kwa 'matuta', kocha wa Hispania, Luis Enrique alionyeshwa kupagawishwa na Ounahi akisema: "Mungu wangu, huyu mtu ametokea wapi? Nilishangazwa sana na Namba 8 wao. Sikumbuki jina lake, samahani…".