Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Noti za Waarabu zaitibulia Simba

Mabululu Agostinho Cristovao Paciencia 'Mabululu'

Thu, 15 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Simba kabla ya kumsajili Leonel Ateba ilikuwa imepiga hodi kwa Al Ittihad ya Misri kuulizia uwezekano wa kumsajili straika tishio wa Angola, Agostinho Cristovao Paciencia 'Mabululu', lakini ghafla mpango wao ukatibuliwa na fedha za kumwaga za Al Ahli Tripoli ya Libya ambayo ndio imefanikiwa kumnasa mshambuliaji huyo.

Mpango wa Simba kumsajili Mabululu ulianza tangu baada ya kumalizika kwa fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 yaliyofanyika Januari huko Senegal ambapo nyota huyo alikuwa moto wa kuotea mbali akifumania nyavu mara tatu.

Mahitaji ya kocha Fadlu Davids ya mshambuliaji mpya aliyoyatoa hivi karibuni, yaliifanya Simba kuwasiliana na viongozi wa Al Ittihad ili kuona uwezekano wa kumsajili Mabululu lakini Walibya wakawazidi ujanja kwa kutoa kiasi kikubwa cha fedha ambacho kimemfanya achague kwenda Libya badala ya kuja Tanzania.

Mwandishi wa habari wa habari za michezo wa Misri, Lotfi Wada amefichua kuwa imeilazimu Al Ahli Tripoli kulipa kiasi cha Dola 1.8 milioni (Sh 4.9 bilioni) ili kupata huduma ya mshambuliaji huyo ambaye amesaini mkataba wa miaka mitatu.

Wada amefichua kuwa ipo timu kutoka nchi inayozungumza lugha ya Kiswahili ambayo pia ilikuwa inawania huduma ya Mabululu lakini mchezaji huyo amechagua kwenda Libya.

“Vita kali kati ya Al Ahli Tripoli na Swahili ya kumsajili lakini Ahli imefanikiwa. Ittihad Alexandria itapata Dola 1.2 milioni. Mkali huyo wa Angola mwenye miaka 32 muda mfupi atasaini mkataba wa kubadilisha maisha yake,” aliandika Wada.

Licha ya Wada kutoitaja timu kutoka ukanda unaozungumza lugha ya Kiswahili, inafahamika kuwa ni Simba ndio ilionyesha nia ya kumtaka Mabululu.

Kwa mujibu wa Wada, Al Ahli Tripoli italipa kiasi cha Dola 600,000 kwa Mabululu mwenyewe ikiwa ni ada ya binafsi ya kusaini mkataba ya mshambuliaji huyo.

Kumkosa Mabululu hapana shaka kumechangia kwa kiasi kikubwa Simba kugeukia Algeria na kumsajili kwa haraka mshambuliaji wa kati na ikaamua kutua kwa nyota wa Cameroon, Lionel Ateba aliyekuwa akiichezea USM Alger ya Algeria.

Simba imetumia kiasi cha Dola 200,000 (zaidi ya Sh 500 milioni) kuishawishi USM Alger iwauzie Ateba ambaye aliingia nchini jana tayari kwa kuanza kibarua cha kuitumikia timu hiyo.

Ateba ana kibarua kigumu cha kuifungia Simba mabao muhimu ambayo pengine yanaweza kufuta nuksi ambayo imewakabili washambuliaji tofauti wa kati kwenye kipindi cha misimu mitatu mfululizo.

Kuanzia msimu wa 2021/2022 hadi uliopita wa 2023/2024, washambuliaji wa kati wa Simba wameonekana kuwa na ubutu jambo ambalo limeilazimisha timu hiyo kuingia sokoni kusajili mchezaji wa nafasi hiyo katika kila dirisha la usajili.

Kwa misimu mitatu iliyopita, hakuna mshambuliaji wa kati wa Simba ambaye alifanikiwa kufunga zaidi ya mabao 10 kwenye Ligi.

Katika msimu uliopita, mshambuliaji wa kati wa Simba aliyepachika mabao mengi alikuwa ni Jean Baleke ambaye alifumania nyavu mara nane na alipoondoka katika dirisha dogo, aliletwa Koublan aliyefunga mabao sita.

Msimu wa 2022/2023, mshambuliaji wa kati wa Simba aliyefumania nyavu mara nyingi alikuwa ni Moses Phiri aliyemaliza akiwa na mabao 10 akifuatiwa na John Bocco aliyefunga mabao tisa.

Katika msimu wa 2021/2022, Meddie Kagere ndiye alimaliza akiwa kinara kwa upande wa washambuliaji wa kati ambapo alifunga mabao saba.

Msimu wa mwisho kwa washambuliaji wa kati wa Simba kutamba ulikuwa ni 2020/2021 ambao John Bocco alipachika mabao 16 na aliyemfuatia alikuwa ni Chris Mugalu aliyefunga mabao 15.

Ikumbukwe msimu huo, Bocco alimaliza akiwa kinara wa ufungaji kwenye Ligi Kuu kwa mabao hayo 16.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: