Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwamba anayewatesa mabeki AFCON

Emilio Nsue Equatorial Emilio Nsue

Mon, 29 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Victor Osimhen, Mohamed Salah na Sadio Mane ni majina makubwa ya mastraika ambao kila mmoja angeweka sarafu yake kwao kwenye upande wa kushinda Kiatu cha Dhahabu kwenye Afcon 2023, lakini ni jina lisilotarajiwa kabisa ndilo limekuwa kiboko kwa kutikisa nyavu huko Ivory Coast.

Emilio Nsue, nahodha wa Equatorial Guinea, ambayo imetinga hatua ya 16 bora na itakuwa na kipute dhidi ya Guinea leo Jumapili, amefunga mabao matano kwenye hatua ya makundi.

Na kama ataendelea kwenye kasi yake ya kufunga mabao, anaweza kuvunja rekodi ya Ndaye Mulamba, aliyefunga mabao tisa katika fainali moja za Afcon 1974.

Nsue alifunga mara mbili katika ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya wenyeji Ivory Coast katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi na alifunga mara tatu kwenye ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Guinea-Bissau, ambapo ilikuwa hat-trick ya kwanza kwenye fainali za Afcon tangu 2008.

Ikishika namba 18 kwenye ubora wa viwango vya soka la Afrika, Equatorial Guinea yenye wakati milioni 1.7 imekuwa moto kwelikweli kwenye soka.

Taifa hilo la Afrika Kati limepiga hatua kubwa kwenye soka kwa kuanzia muongo uliopita, tangu walipokuwa wenyeji wa Afcon 2012 na Afcon 2015, ambapo walikomea kwenye hatua ya nusu fainali.

Kikosi hicho cha sasa, kilichopo chini ya kocha Juan Micha, hakijapoteza mechi tangu Juni 2022.

“Kitu muhimu, nguvu yetu kubwa kwenye kundi hili ni kwa sababu tumecheza pamoja karibu miaka minane au tisa, hivyo tumekuwa ndugu,” alisema Nsue.

Aliongeza: “Hatuna supastaa yeyote, lakini timu hii nadhani ina nguvu kuliko zote Afrika.”

Nsue alizaliwa Mallorca, alikuwa sehemu ya kikosi cha Hispania kilichoshinda ubingwa wa Euro 2011 kwa timu za vijana chini ya miaka 21, alikuwa kwenye kikosi kimoja na mastaa kama David de Gea, Juan Mata na Thiago Alcantara.

Lakini, baadaye alichagua kwenda kuiwakilisha timu ya aliyezaliwa baba yake kwenye soka la wakubwa, ambapo alifanya uamuzi huo kipindi hicho alipokuwa panga pangua kweye kikosi cha Mallorca kwenye La Liga.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: