Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makocha waipa nafasi Taifa Stars

Taifa Stars AFCON Vazi Makocha waipa nafasi Taifa Stars

Fri, 19 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Licha ya Timu ya Taifa la Tanzania, Taifa Stars kuanza vibaya fainali za Kombe Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023, kwa kupoteza dhidi ya Morocco kwa mabao 3-0, bado ina nafasi ya kufanya vizuri kwenye michuano hiyo huko Ivory Coast.

Taifa Stars iliuanza mchezo huo ambao ulichezwa kwenye Uwanja wa Laurent Pokou, San Pedro ikiwa na mpango wa kujilinda zaidi kufuatia kikosi chake kuundwa na idadi kubwa (7) ya wachezaji wenye sifa ya kuzuia ambao ni Haji Mnoga, Mohammed Hussein, Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Hamad ‘Bacca’, Novatus Dismas, Himid Mao na Mudathir Yahya.

Huku idara ya ushambuliaji ikiongozwa na nahodha wa kikosi hicho, Mbwana Samatta na katika maeneo ya pembeni (winga) wakicheza Charles M’Mombwa na Tarryn Allarakhia aliyeweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa Wealdstone ya National League England kucheza fainali hizi tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo zaidi ya miaka 100 iliyopita.

Kocha wa Taifa Stars, Adel Amrouche aliingia na mfumo wa 3-4-3, wakati timu ikishambulia nyuma ilikuwa ikibaki na mabeki watatu, Novatus, Mwamnyeto na Bacca huku wakati ikishambuliwa idadi ya wachezaji ikiongezeka wawili ambao ni Mnoga na Hussein na kuwa na mabeki watano, Himid na Mudathir ambao walikuwa wakicheza eneo la kiungo nao walikuwa wakishuka chini kwa haraka kuongeza nguvu.

Licha ya Stars kuingia na mpango huo ambao ulijikita kwenye kuzuia zaidi huku ikionekana kushambulia kwa kustukiza ilijikuta ikiruhusu bao la kwanza katika dakika ya 30 baada ya Aishi Manula kutema faulo iliyochongwa na Hakim Ziyech kisha, Romain Saiss akamalizia.

Morocco ilionekana kuumiliki mchezo kiasi cha Amrouche kufanya maamuzi magumu dakika nane baada ya kuruhusu bao la kwanza kwa kumtoa Tarryn aliyeonekana muda mwingi timu kuwa nyuma na kuisidia Morocco kuielemea Stars na kumuingiza Simon Msuva.

Stars ilijikuta katika mazingira magumu zaidi katika kipindi cha pili hasa baada ya kuwa pungufu kutokana na Novatus Dismas kuonyeshwa kadi ya pili ya njano iliyofuatiwa na nyekundu katika dakika 70. Tutaliongeleza zaidi tukio hilo.

Dakika saba baadaye Morocco ilipata bao la pili kupitia kwa Azzedine Ounahi kisha kufunga la tatu katika dakika ya 80 kupitia kwa Youssef En-Nesyri.

Licha ya Stars kufanya mabadiliko kadhaa ikiwemo kuingia kwa Morice Abraham, Feisal Salum huku ikitoka Mudathir na Samatta, Stars haikuwa suluhu ya kunusurika na kipigo hicho. Haya ni mambo ambayo Stars iliyaangusha kwenye mchezo huo.

ENEO LA KIUNGO Mudathir na Himid walikuwa wakitumika kwenye eneo la kiungo, walionekana kuwa msaada zaidi kwenye kulinda licha ya washambuliaji wa Morocco kuifungua mara kadhaa ngome ya Stars hata hivyo, hawakuonekana kuwa msaada wakati ambao timu ilipotakiwa kusogea na kutengeneza mashambulizi yake.

Nyota hao walishindwa kuifanya timu kwenda mbele kupitia eneo la kati badala yake walionekana kupiga pasi nyingi za nyuma kitu ambacho hakikuwa na afya kwa timu ambayo ilitakiwa kutafuta mabao kwenye mchezo huo.

Hata hivyo, ni kama Amrouche alikumbuka kujifunika shuka wakati kumeshakucha kwa kuwaingiza Morice na Feisal Salum kwa lengo la wachezaji hao kuchezesha timu kitu ambacho tayari tulikuwa tumeshachelewa.

Morocco ilifanya kile ambacho ilikuwa ikihitaji kwenye eneo la kiungo huku ikijivunia ubora wa utatu wao kwenye eneo hilo ukiwa na Azzedine Ounahi, Selim Amallah na Sofyan Amrabat ambaye alikuwa akicheza mbele ya mabeki wa kati.

KADI NYEKUNDU Ilikuwa ni siku nyingine mbaya kazini kwa Novatus ambaye alionyeshwa kadi ya pili ya njano mara ya pili mfululizo dhidi ya Morocco, ikumbukwe pia kwenye mchezo uliopita wa Kombe la Dunia kwenye Uwanja wa Mkapa hakumaliza dakika 90 za mchezo huo ambao Stars ilipoteza kwa mabao 2-0.

Awamu hii imeonekana kuwa tofauti na ile ya kwanza jijini Dar es Salaam, pamoja na kwamba kiungo huyo alikuwa tayari na kadi ya njano kwa usaidizi wa marejeo ya picha za runinga hakuonekana kutenda madhambi lakini mwamuzi wa mchezo huo, Alhadj Allaou Mahamat  kutoka Chadi alimuadhibu mchezaji huyo.

Licha ya wachezaji wa Taifa Stars kuonekana kumsihi mwamuzi wa mchezo huo akatazame kwenye usaidizi wa teknolojia ‘VAR’ aliendelea kushikilia msimamo wake hivyo ilimbidi Novatus kutoka uwanjani.

UBORA WA MOROCCO   Kwa ujumla Morocco ambayo msimu uliopita wa Kombe la Dunia ilifika nusu fainali na kuwa timu ya kwanza Afrika kufanya hivyo kule Qatar,  ilikuwa bora mno mbele ya Stars katika maeneo yote, ukiangalia takwimu za mchezo huo inaonyesha wazi kuwa walitawala kwa kiwango kikubwa.

Ndani ya dakika 90 za mchezo huo, Taifa Stars haikupiga shuti hata moja ambalo lililenga lango la Morocco tofauti na wababe hao ambao walipiga mashuti saba huku Manula akifanya kazi nzuri ya kuokoa michomo kadhaa ya hatari.

Tofauti na Stars ambayo inajenga timu, Morocco ipo kwenye kilele cha ubora na ni miongoni mwa timu ambazo zinapewa nafasi ya kutwaa ubingwa wa fainali hizo ambazo zinafanyika kwa mara ya pili kwenye ardhi ya Ivory Coast.

WASIKIE WADAU Wadau wa soka nchini, wametoa maoni tofauti, wengine wakitoa njia ambazo zinaweza kuifanya Taifa Stars kufanya vizuri kwenye michezo miwili iliyosalia katika hatua ya makundi dhidi ya Zambia na DR Congo. Stars itacheza na Zambia Jumapili kabla ya kuivaa DR Congo Jumatano ijayo.

Kocha wa zamani wa Gwambina, Mtibwa Sugar na timu za vijana za Azam FC, Mommed Badru, alisema; “Lazima tuseme ukweli Morocco ipo mbali sana inatakiwa kusahau kilichotokea tufanye maandalizi kwa michezo ijayo, naamini mwalimu atakuwa ameona cha kukifanyia kazi, tunatakiwa kuimarika hasa kwenye eneo la kati.”

Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini, Ally Mayay Tembele naye aliona upungufu kwenye eneo la kiungo kwa kudai wachezaji ambao walikuwa wakicheza eneo hilo walikuwa wakipiga pasi nyingi za nyuma.

“Cha kufanya ni maboresho ya upungufu kwenye mchezo wetu uliopita, shida kubwa ilikuwa kwenye kiungo, wachezaji wetu walikuwa wakipiga sana pasi za nyuma,” alisema Mayay.

BADO TUMO Licha ya kuumizwa na matokeo hayo, wachezaji wa Taifa Stars wameonyesha ukomavu kwa kukubali kilichotokea huku wakiahidi mabadiliko kwenye michezo iliyosalia dhidi ya Zambia, Januari 21 na DR Congo, Januari 24 ili kuweka historia ya kuvuka hatua ya makundi.

Nahodha wa kikosi hicho, Samatta alisema; “Tumeumizwa sana na matokeo lakini hatuwezi kubadilisha ambacho tayari kimeshatokea, tunatakiwa kunyenyua vichwa juu kwa ajili ya kupambana na michezo iliyosalia, wenzetu walituzidi.”

Novatus alisema,”Sijui imekuwaje lakini kiukweli sikumgusa yule mchezaji lakini ndio hivyo mwamuzi alishaamua. Kufungwa sio mwisho, tunanafasi bado ila nimeumizwa na kilichotokea.”  

Msuva alisema: “Tunarudi mazoezini kuboresha pale tulipokosea na kuongeza tulipokuwa bora. Mashindano ni magumu lakini tutapambana hadi mwisho hatuwezi kukatatamaa hata kidogo.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: