Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mabao yaliyofungwa mapema zaidi Euro 2024

APTOPIX Euro 2024 Soccer Italy Albania 37836 Mabao yaliyofungwa mapema zaidi Euro 2024

Tue, 18 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Raha ya mechi bao wanasema. Sheria nyingi zimekuwa zikifanyiwa mabadiliko ili tu kulifanya soka kuwa mchezo wa mabao mengi ili kuwapa raha mashabiki wanaokuja viwanjani na kulipa pesa zao nyingi kuangalia mechi.

Mashabiki wanakuja viwanjani wanataka kushangilia mabao. Na kinakuwa kitu cha furaha zaidi kwa mashabiki hao ikitokea kuwapo kwa mabao ya mapema sana kwenye mechi za soka. Hakuna mechi inayokwaza mashabiki kama ile ya matokeo ya 0-0.

Wakati huu mashabiki wa soka huko Ulaya wakiburudika na mikikimikiki ya fainali za Euro 2024, kitu wanachopenda kukiona ni kuona nyavu zikitikiswa, huku raha zaidi endapo ikitokea mabao hayo yanafungwa mapema zaidi.

Jumamosi iliyopita, kwenye mchezo wa Italia na Albania, uliishudia rekodi ya kufungwa kwa bao la mapema zaidi kwenye fainali hizo za Euro 2024 na hivyo kuingia kwenye rekodi ya mabao ya haraka yaliyowahi kufungwa kwenye historia ya michuano hiyo ya ubingwa wa Ulaya.

Haya hapa, mabao 10 yaliyongia kwenye rekodi ya kufungwa mapema kwenye michuano ya kusaka ubingwa wa Ulaya.

10.Michael Owen

Dakika 2, sekunde 25 (England vs

Ureno)

Baada ya kinda wa miaka 18, Wayne Rooney uliweka jina lake juu kwenye soka la dunia, England ilivuka kwenye hatua ya makundi ya michuano ya Euro kabla ya kwenda kuwakabili Ureno kwenye hatua ya robo fainali. Michael Owen aliwahi vyema mpira mrefu wa kipa David James na kumzidi ujanja beki Costinha na hivyo kwenda kufunga kwa kichwa mpira ukimpiga kipa Ricardo kwenye sekunde 145. Rooney akaumia na kutoka nje na baada ya hapo, kila kitu kilitibuka kwa England, ambapo Ureno ilisababisha mechi kwenda dakika 120 na kisha kushinda kwa penalti 6-5.

9.Alan Shearer

Dakika 2, sekunde 14 (England vs Ujerumani)

England iliandaa Euro 1996 na kwa muda mrefu mashabiki wao waliamini huo ni wakati wao wa kunyakua tahi hilo. England ilitamba kwenye hatua ya makundi, ikaichapa Hispania kwa penalti kwenye robo fainali na kwenda kuwakabili Ujerumani katika nusu fainali. Katika mechi hiyo, kikosi hicho cha Terry Venables kilianza vyema kwa bao la mapema kabisa la Alan Shearer, aliyefunga kwa kichwa kwenye sekunde ya 134 na kuamini ni wakati wao, lakini Ujerumani ilisawazisha na kisha kuisukuma nje ya michuano England kwa mikwaju ya penalti 6-5.

8.Petr Jiracek

Dakika 2, sekunde 14 (Czech Republic vs Ugiriki)

Baada ya Russia kuwafanya vibaya kwenye mechi yao ya kwanza ya makundi kwenye Euro 2012, kulikuwa na presha kubwa kwenye kikosi cha Czech Republic na kilihitaji kufanya kweli dhidi ya Ugiriki kuweka hai matumaini yao ya kutinga hatua inayofuatia na hapo kiungo wao Petr Jiracek alifanya jambo, alipowahi krosi ya Tomas Hubschmann na kufunga bao kwenye sekunde ya 134 tu ya mchezo. Wakichagizwa na bao hilo la Jiracek, Czech ilipambana hadi mwisho wa mchezo na kwenda kushinda mchezo huo kwa mabao 2-1 kabla ya kwenda kukomea kwenye robo fainali.

7.Robbie Brady

Dakika 2, sekunde 0 (Jamhuri ya Ireland vs Ufaransa)

Baada ya kuvuka kwenye hatua ya makundi, Jamhuri ya Ireland ilikwenda kukutana na wenyeji Ufaransa kwenye mechi ya hatua ya 16 bora kwenye Euro 2016. Katika mchezo huo, kikosi hicho cha Jamhuri ya Ireland cha kocha Martin O’Neill kilifunga bao la mapema kabisa kwenye sekunde ya 120 tu kupitia kwa Robbie Brady. Hata hivyo, maji yalizidi unga kwa Ireland ilikuwa ngumu kumdhibiti mshindi wa Kiatu cha Dhahabu kwenye fainali hizo, Antoine Griezmann, ambaye alifunga bao la kusawazisha dakika 57 kabla ya kufunga la ushindi dakika nne baadaye. Ufaransa 2-1.

6.Luke Shaw

Dakika 1, sekunde 56 (England vs Italia)

England ilifanikiwa kufika fainali yao ya kwanza ya michuano ya Euro 2020 na kukutana na Italia kwenye mchezo huo wa fainali iliyopigwa uwanjani Wembley. Ikicheza nyumbani, England iliamini itanyakua ubingwa huo, hasa baada ya beki wao, Luke Shaw kufunga bao la mapema kabisa kwenye sekunde 116. Mashabiki wa England walikuwa wakimshinikiza kocha wao Gareth Southgate amalize mechi, lakini ilishindwa kutumia nafasi na Italia ikasawazisha kufanya mechi hiyo kufikia kwenye hatua ya kupigiana penalti na Italia ilishinda 3-2 na kunyakua ubingwa wa Euro 2020.

5.Robert Lewandowski

Dakika 1, sekunde 40 (Poland vs Ureno)

Poland itaringa na nafasi yao ya kutinga nusu fainali ya kwanza kwenye Euro 2016 baada ya kuvuka hatua ya makundi kirahisi na kwenda kuichapa Uswisi kwenye raundi ya 16 bora. Ilipokutana na Ureno kwenye robo fainali, supastaa wao Robert Lewandowski aliweka rekodi ya kufunga bao la mapema, wakati alipohitaji sekunde 100 kutikisa nyavu alipounganisha krosi ya Kamil Grosicki. Hata hivyo, kikosi hicho cha kocha Adam Nawalka kilishindwa kulinda ushindi wake, ambapo Renato Sanches alisawazisha kabla ya Ureno kwenda kushinda kwa mikwaju ya penalti. Mechi iliisha 1-1.

4.Yussuf Poulsen

Dakika 1, sekunde 39 (Denmark vs Ubelgiji)

Denmark ilikumbana na janga kwenye mechi yao ya kwanza Euro 2020, ambapo supastaa wao Christian Eriksen alipatwa na mshtuko wa moyo na kuanguka uwanjani na kusababisha mechi hiyo kusimama kwa dakika kadhaa kabla ya kuendelea na Finland kuibuka na ushindi wa kushtua wa bao 1-0 uwanjani Parken Stadium. Denmark ilihitaji kubadilika na kufanya kweli kwenye mechi zilizofuatia, ndipo hapo staa wao Yussuf Poulsen alipoweka rekodi ya bao la sekunde 99 dhidi ya Ubelgiji. Hata hivyo, mechi hiyo iliishia kwa Denmark kuchapwa 2-1.

3.Emil Forsberg

Dakika 1, sekunde 22 (Sweden vs Poland)

Yussuf Poulsen alidhani kwamba amefunga bao la mapema zaidi kwenye Euro 2020. Lakini, Emil Forsberg, ambaye alifunga kabla ya kufika sekunde 90 kwenye mechi ya makundi baina ya Sweden na Poland kwenye fainali hizo za Euro 2020. Forsberg alimchambua kipa Wojciech Szczesny na kushuhudia mpira wake ukitinga nyavuni kwenye sekunde ya 82 ya mchezo. Kipute hicho kilikuwa cha Kundi E, ambapo ushindi huo, ambapo Sweden ilishinda 3-2 uliwawezesha kuongoza kundi na hivyo kukata tiketi ya kuingia kwenye hatua ya mtoano.

2.Dmitri Kirichenko

Dakika 1, sekunde 7 (Russia vs Ugiriki)

Rekodi ya bao la mapema kwenye hatua ya makundi ya michuano ya Euro ilikuwa ikishikiliwa na Dmitri Kirichenko, aliyefunga baada ya dakika 1 na sekunde 7 katika mchezo baina ya Russia na Ugiriki kwenye Euro 2004. Bao hilo lilikuwa linashikilia rekodi hiyo, hadi hapo staa wa Albania, Nedim Bajrami, alipoamua kuandika rekodi yake kwa kufunga bao la mapema zaidi kwenye historia ya fainali za Euro. Fowadi huyo wa kipindi hicho wa CSKA Moscow, Dmitri Kirichenko alikutana na mpira uliokuwa unazagaazagaa na kutumbukiza nyavuni sekunde ya 67. Russia ilishinda 2-1.

1.Nedim Bajrami

Sekunde 23 (Italia vs Albania)

Ni nzuri kiasi gani kuliweka jina lako kwenye vitabu vya kihistoria ndani ya muda uziozidi sekunde 30. Fainali za Euro 2024 zimeshuhudia rekodi kadhaa, lakini hii ya mkali wa Albania, Bajrami itabaki kwenye kumbukumbu za milele baada ya kuwa mchezaji aliyefunga bao la mapema zaidi katika histotia ya mikikimikiki ya Euro. Bajrami alihitaji sekunde 23 tu kufunga bao la kwanza la Albania huko Ujerumani, ambapo alimzidi ujanja beki Alessandro Bastoni kabla ya kupiga mpira uliomzidi kipa Gianluigi Donnaruma. Hata hivyo, Albania ilichapwa 2-1.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: