Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

EURO 2024: Kwamba mzee? Pepe ni mtu na nusu

Pepe 41 Pepe uwanjani si mchezo

Thu, 27 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kivumbi cha Fainali za Euro 2024 kinaendelea kutimka kule Ujerumani na sasa michuano hiyo ya Mataifa ya Bara Ulaya imemalizika katika hatua ya makundi na inaingia 16 Bora.

Hatua hii inayoanza keshokutwa ndiyo yenye msisimko wa kipekee kwani timu zote zimekuwa na historia nzuri katika soka wakiwamo wenyeji Ujerumani, England, Ufaransa, Hispania na Ureno.

Katika mashindano haya bado watu wanamtazama zaidi staa wa soka duniani, Cristiano Ronaldo anayekipiga timu ya taifa ya Ureno ambaye nayo imekata tiketi ya kuingia hatua ya 16 bora.

Lakini kuna mwamba mmoja wa Kireno anaijulikana zaidi kwa jina lake fupi, si mwingine bali ni Pepe, ndie mchezaji mwenye umri mkubwa kwa sasa kucheza mashindano hayo akiwa na miaka 41.

Pepe ambaye jina lake kamili ni Kepler Laveran Lima, anashiriki mashindano hayo akiwa na umri huo na anaichezea nchi yake mechi ya 135 akiwa na utimamu wa kimwili wa hali ya juu.

Utimamu wake umeendelea kudumu kwa miaka mingi akiwa ni mmoja wa mabeki wakakamavu anayecheza kwa ubabe na kuwakabili kwa nguvu washambuliaji anaokumbana nao.

Katika mchezo mkali dhidi ya Uturuki Jumamosi, beki huyo alikuwa kinara katika kuondoa mipira ya hatari langoni mwao na kusaidia kuibuka na ushindi wa nguvu wa bao 3-0.

Pepe alionyesha uwezo mkubwa licha ya kuwa na umri wa miaka 41 akicheza takribani kwa dakika 85 na huku akiwa ameisaidia timu yake katika mipira ya hatari katika nyanja zote ikiwamo mipira ya juu ya krosi.

Mara nyingi mechi zinapoisha huwa mashabiki wanamkimbilia Ronaldo kupiga naye picha kutokana na umaarufu mwingi. Lakini nyuma yake mafanikio yake timu ya taifa kuna Pepe.

Beki huyu ambaye huweza kunyumbulika na kucheza hata nafasi ya kiungo wa kati, huweza kuzimudu nafasi hizo huku akiwa na umri mkubwa wa kisoka.

Pale alipoulizwa na wanahabari wa Euro 2024 ni lini anafikiria kustaafu soka alijibu ni pale tu Ronaldo atakapotangaza kuachana na soka ndipo na yeye ataamua kustaafu.

Anaeleza yeye yupo kuhakikisha anamsaidia Ronaldo kuendelea kuleta mafanikio katika timu yao ya taifa kwa kuwa ni mmoja wa wachezaji bora duniani ambaye anamhusudu.

Utimamu wake Pepe si mchezo, kila idara ya mwili wake imekamilika vyema. Mwili mkakavu ulioshiba vyema kwa mazoezi na ana mkubwa uwezo wa kunyumbulika akiwa na nguvu na kasi.

Ni mchezaji anayekipiga FC Porto ambayo ilikuwa inashiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku akiendelea kuitwa timu ya Taifa.

Utimamu wa mchezaji wa soka hauji hivi hivi, unahitajika kutengenezwa na kulindwa kila wakati ili kudumu kwa muda mrefu na kucheza kwa kiwango.

Pepe anacheza soka la kimataifa kwa muda wa miaka 22 akiwa mkakamavu asiyepatwa na majeraha ya mara kwa mara. Na ana historia nzuri ya majeraha.

Mtakumbuka moja ya kihatarishi cha mchezaji kuharibika utimamu wake ni kupata majeraha mara kwa mara, kukaa nje muda mrefu, umri mkubwa na kutumika sana.

Utimamu wa Pepe kudumu muda mrefu akiwa fiti na kuepukana na vihatarishi vyote vinavyoweza kuharibu ubora huu ni jambo la kushangaza.

Maisha ya kisoka ya ndani na nje ya uwanja ya beki huyu yanapaswa kuigwa na wachezaji ambao wanapenda kufika mbali. Hana hekaheka za anasa kama walivyo mastaa wenye majina makubwa duniani.

Anasifika kama mchezaji kiongozi ambayo yuko makini na mkali anapokuwa katika majukumu yake uwanjani. Hii imemfanya kuwa nahodha Porto.

Ukali wake na tabia ya kuwa msumbufu na aina ya ukabaji wake amejikuta akilimwa kadi nyekundu mara 17 na njano 212, lakini hiyo haijawahi kumwondolea sifa ya kuitwa timu ya taifa.

Siri ya kudumu na utimamu huo ni hii

Kanuni kuu ya mwanamichezo kudumu na kulinda utimamu wake ni kuzingatia mazoezi na mafunzo, lishe, kupumzika na kulala.

Ili kuyatekeleza mambo hayo hapo juu inahitajika juhudi za hali ya juu na huku ukiwa na nidhamu ya hali ya juu. Inahitajika kuwa na ari na hamasa kutekeleza hayo kwa kiwango.

Pepe anasifika kuwa kinara mazoezi asiyechoka wala kuona kadhia anapofanyishwa mazoezi au mafunzo. Ni mchezaji asiye goigoi katika muda wa mazoezi ya pamoja na yale binafsi.

Mazoezi ya klabu na binafsi ni lazima yazingatie kanuni za wataalam wa afya na sayansi ya michezo. Yapo mazoezi yanayoweza kuharibu utimamu kutokana na kuupa mwili majeraha.

Utimamu unalindwa kwa kuwa na mienendo na mitindo bora ikiwamo kula lishe iliyozingatiwa kanuni za wataalam wa lishe na kufuata ratiba yake.

Kupumzika, kulala na kuburudika kunaupa mwili nafasi ya kujisahihisha na kujikarabati na vijeraha vya ndani kwa ndani. Kuburudika kunaupa mwili utulivu wa kiakili ikiwamo kuondoa mkazo wa kiakili na uchovu wa mwili. Vitu hivi vikiwepo vinaharibu utimamu.

Adui wa utimamu wa mwili wa mchezaji ni ulevi, matumizi yaliyokithiri ya tumbaku, ulaji holela wa vyakula na kutozingatia kupumzika ikiwamo kutumia muda mwingi kuponda raha.

Mchezaji kama Pepe anadumu na kuwa vile kutokana na kuwa katika mikono salama ya bechi la ufundi la kisasa likiwa na idara bora ya afya ambayo ina jukumu la kulinda afya za wachezaji.

Pepe amewahi kucheza Real Madrid moja ya klabu kubwa duniani ambayo ina mfumo bora wa kulinda, kuboresha utimamu wa wachezaji, ndiyo maana hata alipohama aliendelea kuwa bora.

Lakini mwili wa binadamu nao una maajabu yake, kila mtu ana vina vya urithi ambavyo wengine wana vya ziada inavyowafanya kuwa na miili imara yenye ustahimilivu wa hali ya juu.

Ubora wa kinga ya mwili inawawezesha kukabiliana na majeraha yatokanayo na michezo hatimaye kupona kwa wakati.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: