Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lamine Yamal na hadithi ya mastaa 21 Euro 2024

Lamine Yamal Spain 2024 (4) Lamine Yamal na hadithi ya mastaa 21 Euro 2024

Fri, 21 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Lamine Yamal alizaliwa Julai 2007 na ndiye mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kwenye fainali za Euro 2024. Wakati michuano hiyo inaanza huko Ujerumani, kinda huyo alikuwa na umri wa miaka 16.

Kinda huyo kutokea akademia ya Barcelona ameikamata dunia kwa sasa kutokana na kiwango cha soka anachokionyesha uwanjani na kwenye fainali hizo za Euro 2024 yupo kwenye kikosi cha Hispania.

Shughuli wa kinda huyo ni balaa. Lakini, usichokifahamu, Yamal yupo kwenye Euro 2024, ambako kuna wachezaji 21 wao walianza kucheza mechi ya kwanza kabla ya kinda huyo hajazaliwa na sasa atakwenda kuchuana nao huko Ujerumani.

1. Pepe: Beki huyo wa Ureno ndiye mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kwenye Euro 2024 na amemzidi Yamal kwa miaka 25. Kama Hispania itapata nafasi ya kucheza na Ureno, basi vita ya Pepe na Yamal itakuwa kwenye mvuto mkubwa duniani. Pepe mechi yake ya kwanza alikuwa Maritimo B mwaka 2001, miaka sita kabla ya winga huyo wa Hispania kuzaliwa.

2. Cristiano Ronaldo: Yamal atahitaji kufunga mabao 44 kwa msimu kwa miaka 20 ijayo kama anataka kufikia rekodi ya mabao ya supastaa huyo wa Ureno. Hakuna namna kama Yamal ataweza kufikia rekodi hiyo ya mabao ya Ronaldo, ambaye wakati anacheza mechi yake kwanza huko Sporting Lisbon, kipindi akiwa na miaka 16 mwaka 2002, Yamal alikuwa bado hajazaliwa.

3. Manuel Neuer: Kipa huyo Mjerumani amekuwa kwenye kiwango bora cha soka lake tangu mwaka 2005 na bado anatamba, akiwamo kwenye kikosi cha Ujerumani kinachoshiriki michuano ya Euro 2024. Neuer wakati anacheza mechi yake ya kwanza, Yamal alikuwa hajazaliwa.

4. Luka Modric: Akiwa na umri wa miaka 38, kiungo Modric bado anawasha moto uwanjani, akicheza kwa kiwango bora kabisa ndani ya uwanja na kwenye Euro 2024 yupo na kikosi cha Croatia. Alianza soka la kulipwa mwaka 2003, kabla Yamal hajazaliwa na sasa wapo wote Euro 2024.

5. Jesus Navas: Staa huyo Mhispania, ambaye amecheza mechi nyingi zaidi Sevilla bila ya shaka atakuwa na maneno ya busara kwa Yamal wakati watakapokuwa kwenye Euro 2024 huko Ujerumani. Ni kitu kinachoshangaza Yamal na Navas wanacheza pamoja, kwa sababu wakati Navas anacheza mechi yake ya kwanza kwenye soka, ilikuwa miaka minne kabla ya Yamal kuzaliwa.

6. Giorgi Loria: Kipa huyo wa timu ya taifa ya Georgia umri wake ni miaka 38 na alicheza mechi yake ya kwanza mwaka 2005. Tangu wakati huo hadi sasa ameitumikia timu yake ya taifa mara 70, lakini wakati anacheza mechi yake ya kwanza, Yamal alikuwa bado hajazaliwa.

7. Kasper Schmeichel: Ndiyo hivyo, kipa Schmeichel umri wake wa sasa ni miaka 37 na ni miongoni mwa wachezaji wenye umri mkubwa kwenye fainali za Euro 2024. Mechi yake ya kwanza kwenye soka ilikuwa mwaka 2006, mwaka mmoja kabla ya Yamal hajazaliwa.

8. Olivier Giroud: Bila shaka, Euro 2024 itakuwa fainali za mwisho kwa mshambuliaji Giroud kutokana na sasa kuwa na umri wa miaka 37. Mechi yake ya kwanza kwenye soka alicheza mwaka 2005, miaka miwili kabla ya Yamal hajazaliwa. Lakini, wako wote Euro 2024.

9. Jan Vertonghen: Bado anacheza akiwa na umri wa miaka 37, na Vertonghen ndiye mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kwenye kikosi cha Ubelgiji kilichopo kwenye Euro 2024. Beki huyo mechi yake ya kwanza alicheza mwaka 2006 – mwaka mmoja kabla ya Yamal hajazaliwa.

10. Peter Pekarik: Staa huyo wa kimataifa wa Slovakia mwenye umri wa miaka 37 alicheza mechi yake ya kwanza 2004 na kikosi cha Zilina. Amekuwa kwenye kikosi cha Hertha BSC tangu mwaka 2012 na umri wake ni zaidi ya mara mbili ya umri wa Yamal.

11. Juraj Kucka: Kucka anafanya kikosi cha Slovakia kilichopo kwenye Euro 2024 kuwa na utajiri mkubwa wa uzoefu. Mechi yake ya kwanza kwenye soka alicheza mwaka 2006, mwaka mmoja kabla ya Yamal hajazaliwa. Kucka amecheza mechi zaidi ya 100 kwenye kikosi cha Slovakia.

12. Kamil Grosicki: Akiwa na umri wa miaka 36, Grosicki bado ana nguvu ya kukimbizana ndani ya uwanja. Staa huyo alicheza mechi yake ya kwanza kwenye soka la kulipwa, mwaka mmoja kabla ya Yamal kuzaliwa. Grosicki amecheza mechi zaidi ya 650 katika klabu na timu yake ya taifa.

13. Florin Nita: Kipa wa Romania mwenye uzoefu mkubwa na mechi yake ya kwanza ya soka alicheza akiwa Concordia Chiajna mwaka 2006 kipindi hicho alipokuwa na umri wa miaka 19. Umri wake wa sasa ni miaka 37, hivyo mechi yake ya kwanza, Yamal alikuwa bado hajazaliwa.

14. Guram Kashia: Amecheza 113 kwenye soka la kimataifa, Kashia anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji aliyecheza mechi nyingi Georgia. Mechi yake ya kwanza kwenye soka alicheza mwaka 2006 akiwa Dinamo Tbilisi, ambapo ilikuwa mwaka mmoja kabla ya Yamal kuzaliwa.

15. Rui Patricio: Si chaguo la kwanza tena kwenye goli la Ureno, lakini Patricio yupo kwenye Euro 2024 kama chaguo la pili nyuma ya Diogo Costa. Kipa Patricio alicheza mechi yake ya kwanza mwaka 2006, mwaka mmoja kabla ya Yamal kuzaliwa.

16. Domagoj Vida: Croatia ni moja ya timu yenye wastani wa umri mkubwa kwenye Euro 2024 ikiwa na wastani wa miaka 27.7. Vida ni moja ya wachezaji wenye uzoefu mkubwa, akicheza zaidi ya mechi 100 kwa nchi yake. Umri wake wa sasa ni miaka 35 na alicheza mechi yake ya kwanza akiwa na miaka 17 huko Osijek. Hiyo ilikuwa kabla ya Yamal kuzaliwa.

17. Dusan Tadic: Kiungo mshambuliaji wa Serbia mechi yake ya kwanza kwenye soka kimataifa alichezea Vojvodina mwaka 2006 wakati huo alipokuwa na umri wa miaka 18. Kwa mwaka ambao ameanza soka Yamal alikuwa bado hajazaliwa na watakuwa wote huko Euro 2024.

18. Robert Lewandowski: Kwenye orodha hii ya wakali walianza soka kabla ya Yamal hajazaliwa ni Lewandowski pekee yake ambaye amepata nafasi ya kucheza kwenye klabu moja na kinda huyo. Lakini, wakati Lewandowski anaanza soka la kulipwa, Yamal alikuwa bado hajazaliwa.

19. Axel Witsel: Umri wake wa sasa ni miaka 35 na bila shaka hizi zitakuwa fainali za mwisho za Ulaya kwa mchezaji Witsel akiwa na kikosi cha Ubelgiji. Kiungo huyo alianza soka la kulipwa mwaka 2006 na ilikuwa mwaka mmoja kabla Yamal kuzaliwa.

20. Matteo Darmian: Unaweza kubisha kwamba Darmian alianza kucheza soka la kulipwa tangu mwaka 2006, lakini huo ndiyo ukweli. Alicheza mechi ya kwanza akiwa na umri wa miaka 16 huko AC Milan na bado anacheza soka hadi sasa. Wakati anaanza soka, Yamal alikuwa hajazaliwa.

21. Andriy Yarmolenko: Winga huyo wa Ukraine alianza maisha yake ya soka kwenye klabu ya soka ya Desna Chernihiv mwaka 2006, ambapo ilikuwa mwaka mmoja kabla ya Yamal kuzaliwa. Hadi sasa bado anakipiga na yupo kwenye fainali za Euro 2024, ambazo Yamal pia anashiriki.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: