Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kwa Camara Simba imelamba dume

Pin Pin Camara Mousa Camara

Thu, 15 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Tumekuwa tukiinyooshea sana kidole Simba pindi inapochemka kufanya usajili lakini ni nadra sana kuona wachambuzi tukiipongeza pale inapopatia.

Pale kwa yule kipa Mousa Camara, Simba imefanya usajili mzuri sana na kama watamtuza vizuri wataliweka lango lao salama katika idadi kubwa ya mechi msimu ujao.

Kwanza ni kipa ambaye anajiamini akiwa katika milingoti mitatu ya lango, sifa ambayo ni ya muhimu kwa kipa kuwa nayo kwani kama akiwa hajiamini maana yake atakuwa katika hatari ya kufanya makosa binafsi.

Ameonyesha uwezo mkubwa wa kucheza mpira kwa miguu yake yote miwili kwa ufasaha, sifa ambayo makocha wengi wa kisasa wamekuwa wakihitaji makipa wao wawe nayo ili waweze kuanzisha mpira kuanzia nyuma.

Lakini ni kipa mtulivu, anaweza kuipanga vyema safu yake ya ulinzi na amekuwa na maamuzi sahihi ya kujua asimame wapi katika muda gani na bila kusahau kwamba ameonyesha uwezo wa kuokoa mashambulizi ya mbali na yale ya karibu.

Hapana shaka kabla ya kuamua kumsajili Camara, Simba ilifanya tathmini ya kina juu ya uwezo wake na hilo ndilo ambalo inapaswa kulifanya hata kwa wachezaji wa nafasi nyingine ili isiwe inaingia mkenge.

Kipa kama Camara ujio wake maana yake unazidi kupunguza nafasi kwa makipa wazawa lakini hautakiwi kuchukuliwa vibaya na badala yake utazamwe kwa mapokeo chanya ili uwe wenye faida kwa soka letu.

Tuangalie kinachowapa fursa makipa kama akina Camara ni kipi na tuwageukie makipa wetu kwa kuwapa maandalizi mazuri kuanzia wakiwa kwenye umri mdogo ili waweze kuhimili ushindani mbele ya safari.

Wanasema kama huwezi kushindana nao basi ungana nao. Hawa kina Camara ni wa kukaa nao karibu ili tunufaike na sisi.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: