Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kwa Awesu hata Hans Pope kafurahi huko alipo

Hans Pope X Awesuuuuuuuuuuuu Kwa Awesu hata Hans Pope kafurahi huko alipo

Sun, 21 Jul 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Chini ya futi sita ambazo zilichimbwa na mwili wake ukapumzika pale Kihesa Mkimbizi mkoani Iringa, kuna namna mwili wa Zacharia Hans Poppe ulifurahi kutokana na ndoto aliyokuwanayo kwa muda mrefu enzi za uhai kutimia.

Hadi kufikia mwisho wa mwezi huu Julai, Hans Poppe atakuwa amefikisha siku 943 tangu alipovuta pumzi yake ya mwisho katika moja ya vitanda vya Hospitali ya Aga Khan, jijini Dar es Salaam kabla ya kutamatisha safari yake kwenye uso huu wa dunia.

Hans Poppe alifariki dunia Septemba 10, 2021 kisha akazikwa katika kijiji hicho na stori yake iliyojaa mambo mengi ikawa imefungwa rasmi.

Japo hayupo tena duniani, lakini ni wazi Hans Poppe anakumbukwa na watu wengi hasa wanazi wa Simba hususan inapotokea mambo hayaendi ndani ya timu hiyo kama ilivyo katika misimu mitatu hii ambayo Simba imekaa bila ya kutwaa taji la Ligi Kuu Bara.

Enzi zake Hans Poppe alikuwa anapenda kuona Simba ikienda mbele na kubwa zaidi ni namna alivyokuwa fundi wa kufanya usajili, ndiyo maana haikushangaza kupewa aongoze kamati ya usajili ya timu hiyo mara kwa mara. Alikuwa anazijua fitina za usajili na ndiyo maana kuna muda aliwaleta wachezaji waliokuwa wanaonekana kwenda kwa wapinzani wao wakiwemo Yanga.

Kando ya hapo, pia Hans Poppe alikuwa na jicho la kuona wachezaji na hapa nitakurudisha nyuma hadi Machi 19, 2017 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.

Katika mechi hiyo Simba ilikuwa ugenini ikichuana mchezo wa Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya wenyeji wao, Madini FC na ulimalizika kwa Simba kushinda bao 1-0 lililofungwa na straika Mrundi, Laudit Mavugo.

Ushindi huo wa Simba wala haukuwa stori kubwa sana katika mchezo huo kwa kuwa ilikuwa inapewa nafasi ya kushinda kwa ukubwa wao mbele ya wapinzani wao hao ambao hawakuwa na nguvu kubwa hivyo. Stori baada ya mechi hiyo alikuwa kiungo wa Madini FC, Awesu Awesu ambaye wengi walimtambua kama Rasta kutokana na mwonekano wa mtindo wa nywele aina ya rasta ambazo alikuwa nazo.

Awesu katika mechi hiyo alionyesha kiwango cha juu sana akiwa mwiba mkali kwa viungo na mabeki wa Simba kiasi kwamba baada ya mechi kwisha, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zakaria Hans Poppe kumvuta pembeni na kufanya naye mazungumzo. Wengi wa mashabiki ambao walikuwa uwanjani hapo walijua kabisa bw'na mdogo huyo angeweza kuvaa jezi ya Simba baada ya msimu kumalizika kutokana na kazi nzuri ya usajili iliyokuwa inafanywa na Hans Poppe.

Lakini hakuna ambaye alijua nini kilitokea baada ya hapo, kwani Awesu hakujiunga na Simba kama wengi walivyofikiria na badala yake akaenda mahali pengine na maisha kuendelea.

Ajabu ni kwamba baada ya miaka tisa tangu Awesu afanye mazungumzo na Hans Poppe na miaka mitatu tangu kiongozi huyo afariki dunia, ndoto ya wawili hao imetimia baada ya nyota huyo kutangazwa na Simba kama mchezaji wao kwa msimu ujao.

Inawezekana usajili huu ungemfurahisha zaidi Hans Poppe kama angekuwepo wakati huu kwa kuwa alikuwa mtu wa kwanza kuongea naye lakini ndiyo hivyo aliitikia muito wa Mwenyezi Mungu.

Usajili wa Awesu ndani ya Simba kwa ajili ya msimu ujao ni sehemu ya mapendekezo ya timu ambayo inajipanga upya baada ya kufanya vibaya kwa misimu mitatu na kuwaacha wapinzani wao Yanga wakitawala. Awesu ana sifa za kucheza eneo la kiungo mchezeshaji, mshambuliaji wa pili lakini kama winga na kote huko akafanya vizuri.

Jambo zuri zaidi ni kiungo huyo ametua Simba akiwa amekomaa zaidi tofauti na mwaka 2017 ambao alionekana na Hans Poppe na alikuwa bado chipukizi. Kwa sasa Awesu ana uzoefu wa kutosha wa Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa kwa kuwa amepita baadhi ya klabu ambazo zimempa muda mrefu wa kujiimarisha kiwango chake. Kuanzia pale Mwadui FC, Kagera Sugar, Azam FC ambayo ilimsajili baada ya kuwa na msimu mzuri na Kagera hadi KMC ambayo hadi anaachana nayo sasa ndiye alikuwa nahodha wao. Kwa namna fulani hapo unaona kwa namna kiungo huyo alivyokiboresha kiwango chake na kama akapewa muda wa kuaminiwa basi anaweza kuifanyia makubwa Simba msimu ujao.

Inawezekana Simba ingemsajili Awesu kwa wakati ule kama alivyofanya mazungumzo na Hans Poppe, lakini angefeli kwa kuwa hakuwa na uzoefu mkubwa na tungemuweka katika kundi la wachezaji vijana ambao walifeli kikosini hapo.

Hali hiyo iliwahi kuwatokea mastaa wengi waliowahi kusajili na timu hiyo wakiwa na umri mdogo kama Ibrahim Twaha 'Messi wa Tanga' lakini kwa sababu ya kukosa uzoefu na presha ya timu husika akaishia kuwa mchezaji wa kawaida tu.

Kama ulivyo msemo maarufu wa watu ambao wanafariki dunia tunakuwa nao katika nafsi japo hatuwaoni, inawezakana pia hatumuoni Hans Poppe kwa sasa kutokana na kulala ardhini katika nyumba yake ya milele pale Kihisa Mkimbizi, Iringa, lakini huenda akawa amefurahi kwa usajili huu wa Awesu ndani ya Simba kwa ajili ya msimu ujao. Awesu kazi kwako sasa, piga kazi ili uendelee kumfurahisha Hans Pope huko alipo kama ulivyomfurahisha katika mechi ile ya robo fainali ya Kombe la ASFC pale Sheikh Amri Abeid!

Wasifu

Jina: Awesu Ally Awesu

Kuzaliwa: Okt 4, 1997

Mahali: Zanzibar

Nchi: Tanzania

Urefu: Mita 1.66

Nafasi: Kiungo

Klabu: Simba

Alikopita: Arizona, Madini, Singida Utd, Mwadui, Azam, Kagera Sugar, KMC

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: