Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kocha mpya Simba atoa dira

Cadena Simba Nm Kocha mpya Simba atoa dira

Wed, 8 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kipigo cha mabao 5-1 ilichokipata Simba dhidi ya Yanga Jumapili ilyopita, kimemuondoa aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ baada ya kusitishiwa mkataba wake wa mwaka mmoja uliosalia kwa makubaliano ya pande mbili, huku kocha mpya akisema watafanya kazi kuhakikisha timu inapata matokeo mazuri.

Kipigo hicho kilihitimisha ubabe wa Simba kucheza siku 373, ikiwa ni sawa na mwaka mmoja na siku tisa kucheza mechi 28 mfululizo bila kupoteza, ikivuna pointi 74, ikishinda mechi 23 na kudroo tano, huku ikifunga mabao 76 na kuruhusu 17.

Katika mechi 28 ambazo Simba ilicheza mfululizo bila kupoteza, 22 ni za msimu uliopita ambapo ilikusanya pointi 56, zilizotokana na ushindi katika michezo yake 17 huku mitano ikienda sare, ikifunga pia mabao 60 na kufungwa 12.

Katika michezo saba msimu huu imekusanya pointi 18 baada ya kushinda sita huku ikichezea kichapo mara moja. Msimu huu kabla ya Yanga kuitibulia imefunga mabao 16 na kufungwa matano.

Robertinho kabla ya kutua Msimbazi ilikuwa chini ya Juma Mgunda aliyekabidhiwa kufuatia kocha mkuu, Zoran Maki, raia pacha wa Serbia na Ureno kuondoka Septemba 6, mwaka jana kwa makubaliano ya pande mbili. Kabla ya Robertinho kuchukua kikosi, Mgunda alikiongoza katika michezo 16 ya ligi ambapo kati ya hiyo alishinda 11, sare nne na kupoteza mmoja akiiwezesha timu hiyo kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kuondoka kwa Mbrazili huyo, timu hiyo imekabidhiwa kwa kocha wa makipa, Dani Cadena akisaidiana na Selemani Matola aliyerejeshwa kwa mara nyingine baada ya Mei 31, mwaka huu kuteuliwa kuwa kocha mkuu wa soka la vijana la timu hio.

CADENA NI NANI?

Cadena ni kocha wa zamani wa makipa wa klabu za Ligi Kuu Hispania (La Liga) Sevilla na Real Betis, akiwahi pia kufanya kazi China na Saudi Arabia huku akiwa na uzoefu na elimu ya juu ya Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA).

Kocha huyo (45), alijiunga na Simba msimu huu baada ya kuachana na Azam FC alikodumu kwa mwaka mmoja akichukua nafasi iliyoachwa na Chlouha Zakaria, raia wa Morocco aliyeondoka kikosini.

MATOLA KIBOKO

Nyota huyu wa zamani wa Simba aliyefundisha timu mbalimbali kama Polisi Tanzania na Lipuli anaendeleza rekodi ya kukaa katika benchi la ufundi la kikosi hicho baada ya makocha wakuu kutimuliwa kutokana na matokeo mabovu kikosini.

Baadhi ya makocha ambao amefanya nao kazi ni Zoran Maki, Pablo Franco, Didier Gomes Da Rosa, Sven Vandenbroeck Mgunda na Patrick Aussems.

Matola anatajwa kama kocha anayeaminika zaidi Simba akirudi sasa akiwa na wasifu mkubwa zaidi baada ya kumaliza kozi ya Leseni A ya Ukocha ya CAF, lakini akiwa kati ya makocha walioichapa Yanga mara mbili akiwa kocha wa Lipuli na sare ya 3-3 akiwa na Polisi Tanzania.

MSIKIE MATOLA

Baada ya kurejeshwa kusaidiana na Cadena, Mwanaspoti lilimtafuta Matola ambapo alieleza kwa ufupi watakachofanyia kazi kwa sasa ni kuangalia upungufu uliojitokeza na kuurekebisha.

“Ni mapema sana kuongea. Hii ni kazi ngumu ingawa inawezekana kutokana na ushirikiano uliopo wa benchi la ufundi pamoja na juhudi za wachezaji. Sisi binafsi tunatambua timu inahitaji matokeo chanya na tutapambana kadri ya uwezo wetu,” alisema.

Makocha hao walitakiwa kuanza kazi jana jioni kujiandaa na mchezo dhidi ya Namungo utakaopigwa leo jioni kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: