Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kocha Simba huko kambini ni habari nyingine, akinogesha kambi

Fadlu Davids Misriii Kocha mkuu mpya wa Simba, Fadlu Davids

Fri, 12 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kazi imeanza. Baada ya kocha mkuu mpya wa Simba, Fadlu Davids kutua kambini juzi jioni na jana kuanza rasmi kazi ya kukinoa kikosi hicho, Kibu Denis aliyekuwa anakula bata huko Marekani ameinogesha kambi hiyo baada ya kutimba sambamba na wachezaji walioondoka katika kundi la pili la msafara wa timu hiyo.

Kibu alikuwa mapumzikoni na familia yake wakati wachezaji wakikusanyika Dar kabla ya Jumatatu kundi la kwanza kusafiri kwenda jijini Ismailia, Misri kuanza kambi ya maandalizi ya msimu mpya ambapo kundi la pili la wachezaji pamoja na makocha wapya waliwasili juzi jioni, kabla ya jana kocha mkuu kuanza rasmi kazi.

Fadlu amekula shavu Msimbazi sambamba na wasaidizi wengine wanne wapya wote wakitokea Afrika Kusini walitua jioni ya juzi katika kundi la pili la msafara wa Simba baada ya awali kocha msaidizi, Seleman Matola kutangulia na sehemu kubwa ya wachezaji wapya na wa zamani wanaounda kikosi cha msimu ujao.

Simba imeweka kambi katika hoteli ya kifahari ya Mercure Ismailia Forsad Island na itakuwa hapo kwa siku zisizopungua 18 kabla ya kurejea nchini Agosti Mosi kuwahi maandalizi ya Simba Day itakayofanyika Agosti 3 na siku tano baadaye itacheza mechi ya nusu fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga kuzindua msimu mpya.

Lakini wakati kocha Fadlu akianza rasmi kibarua akiwa na Simba, Kibu Denis aliyesababisha baadhi ya mashabiki kuanza mjadala kwamba huenda asiwe na kikosi hicho licha ya kutambulishwa kuongezwa mkataba kutokana na kuonekana kula bata Marekani, amekata mzizi wa fitina kwa kutimba kambini Misri.

Sio Kibu tu, lakini wachezaji wengine wa timu hiyo waliokuwa msimu uliopita akiwamo David Kameta ‘Duchu’ na Hussein Kazi nao walikuwa ni kati ya wachezaji waliowasili kambini hapo kunogesha maandalizi hayo ya Mnyama ambayo ilimaliza katika nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu Bara msimu uliopita.

Chanzo cha uhakika kutoka ndani ya Simba, kililiambia Mwanaspoti kuwa, Kibu aliingia usiku wa juzi akitokea Marekani na kuishia kupumzika kiasi cha kushindwa kufanya mazoezi na wenzake jana asubuhi kabla ya jioni kuungana kuanza ngwe mpya akiwa na kikosi hicho.

“Kibu ameshatinga kambini, alifika jana (juzi) usiku, leo (jana) asubuhi hakushiriki mazoezi, aliachwa kwanza apunguze uchovu wa safari, lakini aliungana na wenzake na niwatoe hofu mashabiki, huyu jamaa bado tunaye,” kilisema chanzo hicho na kuongeza; “Kocha mkuu ameshaanza kazi.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: